Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) ameongoza ujumbe wa
Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Kawaida wa 45 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) unaofanyika leo tarehe 28 Juni, 2024 jijini Arusha.
Mkutano huu pamoja na masuala
mengine unapitia na kujadili masuala mbalimbali ya kipaumbele katika ukanda wa
EAC ambayo ni, Maendeleo ya Miundombinu, forodha na biashara, masuala ya siasa
na kijamii, taarifa ya kamati ya rasilimali watu pamoja na kupokea taarifa ya kamati
ya ukaguzi na udhibiti wa hesabu za jumuiya kwa kipindi cha mwaka wa fedha
unaoishia Juni 2023.
Masuala mengine ni pamoja na,
jitihada za kubidhaisha Kiswahili kikanda na kimataifa sambamba na taarifa ya
Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7Julai ambayo kikanda
yatafanyika nchini Kenya na kuhudhuriwa na Nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Kadhalika, mkutano huu pia
umejadili na kusisitiza umuhimu wa kuwasilisha michango ya mwaka kwa wakati kutoka
kwa nchi zote wanachama ili kuiwezesha Sekretarieti ya EAC kujiendesha na
kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya kikanda.
Aidha, kupitia mkutano huo
Katibu Mkuu Mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Veronica Mueni Nduva
alijitambulisha kwa Baraza hilo na kueleza nia yake ya kusimamia ustawi wa
kikanda katika kukuza uchumi, uvumbuzi, biashara, ajira na amani na usalama kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa EAC.
Viongozi wengine wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na, Naibu Waziri
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki - anayeshughulikia
masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.), Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais - Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb.), Makatibu Wakuu na
Maafisa Waandamizi kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.
Mkutano huo umefanyika chini
ya Uenyekiti wa Jamhuri ya Sudan Kusini na umehudhuriwa na Nchi zote Wanachama
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, isipokuwa Somalia imeshiriki kwa njia ya
mtandao.
=====================================
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Uganda ukifuatilia Baraza la Mawaziri la EAC, aliyekaa kati ni Waziri anayeshughulia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kaganda. |
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Uganda ukifuatilia Baraza la Mawaziri la EAC, kulia ni Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Jen. James Kabarebe. |
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Burundi ukifuatilia Baraza la Mawaziri wa EAC. |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ikifuatilia mkutano. |
Ujumbe wa kamati ya ukaguzi wa hesabu kutoka nchi za EAC. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.