Thursday, August 8, 2024

MAKATIBU WAKUU WA SADC WAKUTANA JIJINI HARARE

Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana Harare, Zimbabwe kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya husika utakaofanyika tarehe 17-18 Agosti, 2024.

 

Mkutano huo unatarajia kujadili masuala mbalimbali ikiwemo, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC, usalama wa chakula na lishe kwenye kanda na Utekelezaji wa Mpango wa Manunuzi ya Pamoja ya Huduma za Afya ya SADC unaoratibiwa na Bohari ya Dawa (MSD) ya Tanzania.

Aidha, hafla ya ufunguzi wa mkutano huo imewezesha makabidhiano ya nafasi ya unyekekiti katika ngazi ya Mkutano wa Makatibu Wakuu ambapo Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Balozi Nazaré José Salvador amekabidhi nafasi hiyo kwa mwenyekiti mpya, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbambwe, Balozi Albert Ranganai Chimbindi akisisitiza kumpa ushirikiano katika nafasi hiyo.

 

Naye Balozi Chimbindi amemshukuru Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Pia ameahidi kuzingatia ushauri aliokuwa akiutoa kwa Sekretariet ya SADC na kufanya kazi pamoja ili kuyafikia malengo ya jumuiya hiyo kwa maslahi  jumuishi.

 

“Tumepiga hatua lakini bado tuna kila sababu ya kuweka bidii kwenye ujenzi wa miundombinu, usafiri na hatimaye tuweze kuifikia SADC tunayoitaka. Niwahakikishie kuwa Zimbabwe ipo tayari kufanya kazi pamoja nanyi kwa kufuata malengo, kanuni na mikataba ya SADC'', Balozi Chimbindi.

 

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali SADC utatanguliwa na mikutano ya awali kwa ajili ya maandalizi ambayo ni: Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao utapitia na kujadili hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda kwa kipindi cha Agosti 2023 hadi Agosti 2024. Mkutano huu utahusisha nchi tatu za SADC Organ TROIKA na wajumbe wake ambao ni Angola (Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama), Zambia (Makamu Mwenyekiti wa Organ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi).

 

Mikutano mingine ni: Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14 Agosti 2024 pamoja; na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 8 hadi 11 Agosti, 2024. 

===================================

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba ameshiriki katika Kikao cha Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambacho ni sehemu ya vikao vya maandalizi ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 17 na 18 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini nchini Zimbabwe, Mhe. IGP (RTD) Simon Sirro.

Mkurugenzi Idara ya Ushirikikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akifuatilia hafla ya ufunguzi katika mkutano huo wa Mkatibu Wakuu ulioanza leo tarehe 8 Agosti, 2024 Harare, Zimbambwe.

Kushoto ni Afisa Sheria Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Felister Lero na Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Joseph Haule wakifatilia mkutano.

Picha ya pamoja: Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) baada ya ufunguzi wa Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 8 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.

 

Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Balozi Nazaré José Salvador amekabidhi nafasi hiyo kwa mwenyekiti mpya, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbambwe, Balozi Albert Ranganai Chimbindi ambapo amesisitiza kumpa ushirikiano katika nafasi hiyo.

Habari katika picha 









Monday, August 5, 2024

WAZIRI KOMBO APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA MABALOZI WATEULE WA ZIMBABWE, ITALIA NA RWANDA NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Zimbabwe nchini, Mhe. Helen Bawange Ndingani, Balozi Mteule wa Italia nchini, Mhe. Giuseppe Sean Coppola na Balozi Mteule wa Rwanda nchini, Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaaam tarehe 5 Agosti, 2024.


Akipokea nakala hizo Waziri Kombo amewapongeza mabalozi hao kwa uteuzi waliuopata na pia amewaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi watakachokuwa nchini kuziwakilisha nchi zao.


Aidha, ameeleza Mabalozi hao Wateule wanatarajiwa kuwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 12 na 13 Agosti, 2024.


Akiongea na Balozi Mteule wa Zimbambwe nchini, Mhe. Ndingani, Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania na Zimbabwe zimekuwa na ushirikiano wa kihistoria na kindugu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili Hayati, Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati, Robert Mugabe wa Zimbabwe.


Vilevile, akamkaribisha Mhe. Ndingani kutembelea Maktaba ya Hayati Mwl. Nyerere iliyopo Butiama, mkoani Mara ambayo imesheheni historia yake. 


Balozi Kombo pia, akaeleza umuhimu wa kuwekeza na kurithisha historia ya ukombozi kwa vijana ili waweze kufahamu kwa kina namna waasisi hao walivyojitoa kupigania uhuru wa Bara la Afrika hususan harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.


Viongozi hao pia wamejadili juu ya umuhimu wa kufanyika kwa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zimbabwe ambapo ameeleza kuwa Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano huo. Tanzania na Zimbabwe zinashirikiana katika masuala ya biashara, uwekezaji, usafirishaji, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi, elimu, Sanaa na utamaduni, na sekta nyingine za kisiasa.


Akizungumza na Balozi Mteule wa Italia nchini, Mhe. Coppola, Mhe. Waziri Kombo amesisitiza kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kuendeleza ushirikiano na nchi hiyo ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kupitia mpango wa ushirikiano wa Italia na Afrika unaofahamika kama “Mattei Plan”. Tanzania na Italia zinashirikiana katika sekta za utalii, elimu, Maji, biashara na uwekezaji, kilimo, mifugo na uvuvi, na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na ngozi ili kukuza biashara yake kimataifa.

 

Tanzania na Italia zinatarajia kuwa na Kongamano la biashara litakalofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Desemba, 2024 kwa lengo la kukuza sekta ya biashara na za kiuchumi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili amabapo, pembezoni mwa kongamano hilo kutafanyika mashauriano ya kisiasa.


Vilevile, katika mazungumzo yake na Balozi wa Rwanda, Mhe. Jenerali, Patrick Nyamvumba, Mhe. Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Rwanda kupitia ujirani wa nchi hizo mbili sambamba na kusimamia makubaliano mbalimbali yaliyokubaliwa katika nyakati tofauti na majukwaa mbalimbali ambayo nchi hizo mbili zimekubaliana kuyatekeleza.


Tanzania na Rwanda zinashirikiana katika sekta za mawasiliano, biashara na uwekezaji, usafirishaji, elimu, utamaduni na michezo, miundombinu, kilimo na mifugo.

 

Jukumu hili la kupokea Nakala za Hati za Utambulisho limefanywa na Mhe. Waziri Kombo kwa mara ya kwanza tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.


=======================================


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Zimbabwe nchini, Mhe. Helen Bawange Ndingani (Kushoto). Mapokezi hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaaam tarehe 6 Agosti, 2024.



=======================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Italia nchini, Mhe. Giuseppe Sean Coppola (Kushoto). Mapokezi hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaaam tarehe 6 Agosti, 2024.




===========================================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Rwanda nchini, Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba (kushoto). Mapokezi hayo yamefanyka katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaaam tarehe 5 Agosti, 2024.




Friday, August 2, 2024

WAZIRI KOMBO AMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE UAPISHO WA RAIS WA IRAN


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mhe. Masoud Pezeshkian wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Tehran tarere 31 Julai, 2024; alipokwenda kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Iran.


· Afanya mazungumzo na Rais huyo

· Mikakati ya kukukuza zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi yawekwa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo alimwakilisha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sherehe za uapisho wa 14 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mhe. Masoud Pezeshkian iliyofanyika katika viwanja vya Bunge vya Nchi hiyo jijini Tehran, tarehe 30 Julai, 2024.

Waziri Kombo aliwasili nchini humo alfajiri ya tarehe 30 Julai 2024 ambapo baada ya kushiriki katika sherehe hizo za uapisho aliendelea kujumuika na maelfu ya Wanadiplomasia na Viongozi wa Nchi na Serikali kutoka sehemu mbalimbali duniani kushiriki katika dhifa iliyofanyika katika Ikulu jijini Tehran. 

Waziri Kombo, alimpongeza Mhe. Pezeshkian kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliofanyika hivi karibuni, na kuongeza kusema kuwa Iran na Tanzania zina uhusiano wa karibu wa kiutamaduni na kihistoria ambao ulianza miaka mingi iliyopita wakati kundi la Wairani kutoka Mji wa Shiraz lilipohamia Zanzibar na kueneza utamaduni wa Iran na lugha ya Kiajemi.

Mbali na kushiriki katika sherehe za uapisho huo, Waziri Kombo alifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mhe. Masoud Pezeshkian yaliyofanyika Ikulu jijini Tehran tarehe 31 Julai, 2024, akiwa ni Waziri wa Mambo ya Nje wa kwanza na pekee aliyepata fursa ya kuzungumza na Rais huyo muda mfupi baada ya kuapishwa kwake.

Mazungumzo hayo yalijikita kujadili kuhusu masuala mbalimbali ya kudumisha na kukuza zaidi ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa, kijamii, utamaduni na uchumi kati ya nchi hizo mbili. 

Kwa upande wake Rais wa Iran Mhe. Pezeshkian katika mazungumzo yaliyofanyika kwa takriban dakika 25 huku pande zote mbili zikionesha furaha, shauku na umakini, alielezea furaha yake na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuma ujumbe uliowasilisha salam za pongezi na kushikiri katika sherehe za uapisho wake. 

Mhe. Pezeshkian aliendelea kueleza kuwa Tanzania na Iran kwa muda mrefu zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali, hivyo katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha uhusiano huo unaedelea kukua zaidi na maeneo mengine mapya ya ushirikiano yanafunguliwa kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Kwa muda mrefu tumekuwa na ushikiano mzuri kati yetu katika maeneo mbalimbali, nitoe raia kuwa sasa niwakati muafaka ufanyike mkutano wa mashauriano wa tume ya uchumi ili iandae rasimu ya Hati za Makubaliano ya Ushirikiano ya pande zote mbili” alisema Rais Mhe. Pezeshkian

Kwa upande wake Waziri Kombo alieleza baadhi ya mikakati na hatua mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa na Tanzania katika kudumisha na kukuza zaidi ushirikiano na Iran ikiwemo mandalizi ya kufanyika kwa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), Kongamano la biashara kati ya Tanzania na Iran, kubadilishana ziara za viongozi kufanya mapitio ya suala la Visa rejea (referral visa). 

Vilivile, Waziri Kombo alifanya mazungumzo na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mhe. Ali Bagheri ambapo walijadili na kukubaliana utekelezaji masuala mbalimbali muhimu katika kukuza ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mhe. Masoud Pezeshkian wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Tehran
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiagana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mhe. Masoud Pezeshkian mara baada ya hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa na Rais wa Iran kwa ajili ya wageni wake.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mhe. Masoud Pezeshkian walipokutana kwa mazungumzo katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Tehran, tarehe 30 Julai, 2024, alipokwenda kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Iran.

Thursday, August 1, 2024

NAIBU KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AFUNGUA MKUTANO KUJADILI ITIFAKI YA UMOJA WA AFRIKA KUHUSU UHURU WA WATU KUSAFIRI BILA VIKWAZO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ametoa wito kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika kuridhia Itifaki ya Uhuru wa Watu Kusafiri bila Vikwazo ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi hizo kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Balozi Mussa ametoa wito huo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo na uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na Umoja wa Ulaya uliofanyika leo Agosti 01, 2024 mjini Unguja, Zanzibar.

Amesema kuwa faida za Itifaki hiyo ni nyingi kwa watu wa Afrika ambapo mbali na kurahisisha usafiri wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine, lakini pia ni muhimu katika ukuzaji rasilimali watu na kutengeneza fursa kwa vijana kama vile biashara, utalii, kuimarisha utamaduni miongoni mwa watu na kwa kiasi kikubwa itakuza uchumi wa nchi za Afrika. Itifaki hiyo pia itawawezesha raia kutoka nchi za Afrika kuishi na kujenga uchumi kwa maendeleo endelevu ya Bara la Afrika.

Amesema  mafanikio ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) ambao umeanza kutekelezwa na nchi wanachama tangu mwaka 2021, yatafikiwa kikamilifu pale nchi zote wanachama zitakaporidhia Itifaki hii ili kwenda sambamba na Itifaki nyingine za Uhuru wa Kuingiza  Bidhaa na Uhuru wa Kutoa Huduma.

“Ninafurahi kwamba Nchi nyingi na Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi kama EAC, ECOWAS, IGAD na SADC zimefanyia kazi Itifaki hii kupitia kanda zao na lengo ni kuongeza zaidi uhuru wa watu wa Afrika kutembea kutoka nchi moja kwenda nyingine”, amesema Balozi Mussa.

Pia amewataka wajumbe wa mkutano huo kujadili changamoto mbalimbali zinazokwamisha kuridhiwa kwa Itifaki hiyo ambayo ilipitishwa na nchi za Afrika mwaka 2018. Hadi sasa ni nchi nne pekee zimeridhia itifaki hiyo inayohitaji nchi 15 kuiridhia ili kuanza utekelezaji wake.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Balozi na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shiyo  amesema kuwa Mkutano huo utajikita katika kuainisha changamoto na nini kifanyike ili kuwezesha kuridhiwa na kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Bara la Afrika hususan katika sekta ya ukuzaji biashara, utalii na uchumi kwa ujumla. Pia amesema wajumbe watajadili, kujifunza na kubadilishana uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na nchi ambazo tayari zimeridhia  Itifaki hiyo.

Naye Mkuu wa Idara ya masuala ya Kibinadamu na Harakati Huru kutoka AIJC, Mhe. Rita Amijkhobu amesema Itifaki hiyo ikianza kutumika itainganisha Afrika na kuwa kitu kimoja ambapo itawezesha watu kupita kwenye mipaka kwenda nchi nyingine bila vikwazo hatua itakayosaidia mzunguko wa biashara kukua kwa haraka.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akizungumza katika ufungua rasmi Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo na uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na Umoja wa Ulaya uliofanyika leo Agosti 01, 2024 mjini Unguja, Zanzibar. 


Mhe. Rita Amijkhobu, Mkuu wa Idara ya masuala ya Kibinadamu na Harakati Huru kutoka AIJC naye akizungumza kwenye Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo na uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na Umoja wa Ulaya uliofanyika leo

Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania Mhe. Emilio Rossetti akielezea jambo kwenye mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo. 

Balozi na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shiyo akizungumza na kuwakaribisha wageni waliokuja nchini kuhudhuria Mkutano wa majadiliano.

Juu na chini ni sehemu ya wajumbe walio hudhuria  Mkutano kwenye mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo. 




Sehemu ya wajumbe kutoka Zimbabwe na Uganda wakifuatalia kwa makini ufunguzi rasmi wa mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo. 

Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo ukiendelea. 


Saturday, July 27, 2024

WAZIRI KOMBO AANZA KAZI RASMI












Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameanza kazi rasmi katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kombo ameanza majukumu hayo muda mfupi baada ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri Mhe. January Makamba (Mb).

Makabidhiano hayo yalihudhuriwa pia na Naibu Mawaziri ambao waliteuliwa pamoja, Mhe. Cosato Chumi na Mhe. Dennis Londo

Mhe. Waziri katika siku yake ya kwanza amekutana na kufanya mazungumzo na Mgombea wa nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile.

Aidha, Mhe. Waziri amekutana na baadhi ya Wakurugenzi waliopo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutekeleza majukumu

mbalimbali ambapo amepoeka taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara.


Friday, July 26, 2024

BALOZI KOMBO NA MANAIBU WAKE WAPOKELEWA KATIKA OFİSİ NDOGO ZA WIZARA DSM

 


 

 





















 

 

 

 

 

 



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amewasili na kupokelewa katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam akitokea Ikulu ya Dar es Salaam baada ya kuapishwa kuwa Waziri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Katika mpokezi hayo, Mhe. Balozi Kombo aliiambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Lazaro Londo na kulakiwa kwa bashasha na viongozi na Watumishi wa Wizara waliokusanyika katika Ofisi ndogo, Dar Es Salaam.


Mhe. Balozi Kombo pamoja na Naibu Mawaziri, Mhe. Londo na Mhe. Chumi waliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa hizo katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika Julai 21, 2024

 

RAIS SAMIA AWAAPISHA MHE. BALOZI KOMBO NA MANAIBU WAZIRI IKULU DAR ES SALAAM

Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiapa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ikulu Dar es Salaam, Julai 26, 2024

Mhe. Dennis Lazaro Londo akiapa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Masharika, Ikulu Dar es Salaam, Julai 26, 2024


Mhe. Cosato Chumi akiapa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ikulu Dar es Salaam, Julai 26, 2024



Mawaziri na Manaibu Waziri Wakiapa kiapo cha Uadilifu baada ya kuapishwa na Mhe. Rais  kushika nyadhifa hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Julai, 2024.


Mawaziri na Manaibu Waziri wakisaini Hati ya kiapo cha Uadilifu baada ya kula kiapo hicho na kuapishwa na Mhe. Rais  kushika nyadhifa hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Julai, 2024.