TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
nchini
Rais wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Ayodeji Adesina atafanya ziara ya siku nne (4)
nchini kuanzia tarehe 25 hadi 28 Aprili, 2018 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Lengo la ziara ya Dkt. Adesina
nchini ni kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo ambayo imekuwa
ikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya miradi ya miundombinu nchini.
Akiwa nchini, Mhe. Dkt. Adesina
ataonana kwa mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Magufuli pamoja na kuzindua Barabara
kutoka Dodoma kwenda Babati hafla itakayofanyika katika eneo la Mradi wa
Barabara wa Mayamaya-Mela-Bonga Wilayani Kondoa.
Aidha, Dkt. Adesina atatembelea
Mtambo wa Kusafirisha Umeme wa Iringa kwenda Shinyanga pamoja na Kituo Kidogo
cha Umeme cha Zuzu cha Mkoani Dodoma.
Dkt. Adesina ambaye ameambatana
na Makamu wa Rais wa Benki hiyo anatarajiwa kushiriki Maadhimisho ya Miaka 54
ya Muungano wa Tanzania yatakayofanyika Mkoani Dodoma tarehe 26 Aprili, 2018.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za
Afrika zinazoongoza kwa kupokea misaada kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kupitia
Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF). Aidha, tangu kuanzishwa kwa Benki hiyo hapa
nchini mwaka 1971, Tanzania imenufaika kwa kiasi cha zaidi ya Dola za Marekani
bilioni 3.5 huku miradi ya maendeleo ya miundombinu ikipewa kipaumbele.
Aidha, hadi kufikia mwezi Novemba
2017 Benki ya Maendeleo ya Afrika imekuwa ikitekeleza miradi 25 yenye thamani
ya Dola za Marekani milioni 1.9. Kati ya miradi hiyo, 22 ni ya Sekta ya Umma yenye
thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.8 huku miradi mitatu (3) ikiwa chini ya
Sekta Binafsi kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 187.0.
Kati ya miradi yote, miradi ya
maendeleo ya miundombinu inachukua asilimia 73 ambapo kati yake miradi ya
Barabara ni asilimia 51, Maji na Usafi wa Mazingira asilimia 12 na Nishati
asilimia 10. Asilimia 27 zilizosalia zinasaidia miradi ya sekta binafsi hususan
katika kilimo na ustawi wa jamii.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 24 Aprili, 2018
-Mwisho-