Saturday, April 21, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA WAZIRI WA SHERIA WA ISRAEL NCHINI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Taarifa kuhusu ziara ya Waziri wa Sheria wa Israel nchini

Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Ayelet Shaked atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 22 hadi 24 Aprili, 2018. 

Akiwa nchini, Mhe. Waziri Shaked ambaye anaongoza ujumbe wa wafanyabiashara na wawakilishi wa makampuni kutoka Israel atashiriki Kongamano la Tano la Biashara kati ya Tanzania na Israel litakalofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam tarehe 23 na 24 Aprili, 2018.

Kongamano hilo ambalo linalenga kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Israel, litahusisha Sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambazo ni pamoja na Kilimo, Viwanda, Afya, Nishati na Utalii. Aidha, kupitia Kongamano hilo wafanyabiashara katika sekta hizo watabadilishana mawazo baina yao pamoja na watendaji wa Serikali ili kufikia malengo waliyopanga.

Kongamano hilo linaratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT).

Pamoja na kushiriki katika Kongamano hilo, Mhe. Waziri Shaked ameomba miadi ya kukutana na Viongozi mbalimbali Serikalini akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Aderladus Kilangi.

Kabla ya kuhitimisha ziara hiyo, Mhe. Shaked atakutana na vyombo vya habari tarehe 24 Aprili, 2018 kwa ajili kueleza mafanikio ya ziara yake nchini. Mhe. Shaked na ujumbe wake wataondoka nchini siku hiyohiyo kurejea Israel.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 21 Aprili, 2018
-Mwisho-

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.