Friday, April 6, 2018

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
FURSA ZA UFADHILI WA MAFUNZO KWA WATANZANIA
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea fursa za ufadhili wa masomo ya muda mfupi na muda mrefu katika kada mbalimbali kutoka Umoja wa Afrika, Serikali za China, Ujerumani na Jamhuri ya Korea.
Kuhusu ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu, Umoja wa Afrika kupitia Mwalimu Nyerere African Union Scholarship Scheme umetoa ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu (PhD) kwenye masuala ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM). Waombaji wa mafunzo haya ni wanawake pekee wenye umri wa miaka isiyozidi 35 kwa mafunzo ya ngazi ya Shahada ya Uzamili na miaka isiyozidi 40 kwa mafunzo ya ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD). Maelezo ya ziada kuhusu mafunzo haya yanapatikana kupitia tovuti ya http://www.au.int. au maombi yatumwe kwa OlgaA@african-union.org na nakala kwa mwalimunyerere@africa-union.org. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Aprili, 2018.  Mafunzo haya yanaratibiwa  na Wizara ya Elimu, Sayansi  na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Aidha, Baraza la Ufadhili wa Mafunzo la China limetoa nafasi za ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu. Maelezo kuhusu mafunzo haya yanapatikana kupitia http://www.esc.edu.cn. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Aprili, 2018. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Vilevile,  Serikali ya China imetoa fursa ya ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili katika masuala ya Utawala na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Nadharia ya Uchumi na Maendeleo ya Taifa. Maelezo ya ziada ya kozi hizi yanapatikana kupitia http://www.isscad.pku.edu.cn. Pia maombi yatumwe kupitia http://www.administration@isscad.pku.edu.cn. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Mei, 2018. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimentii ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Wakati huohuo, Serikali ya China imetoa fursa za ufadhili wa mafunzo kwa wataalam wa kilimo kutoka Tanzania. Mafunzo haya yatafanyika Beijing, China. Mratibu wa mafunzo haya ni Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kwa upande mwingine, Wizara imepokea nafasi za mafunzo ya muda mfupi kutoka Serikali ya Ujerumani katika Kozi ya Stashahada ya Juu ya Usimamizi wa Mazingira kwa Nchi Zinazoendelea (International Postgraduate Course on Environmental Management for Developing Countries). Mafunzo haya yatafanyika Ujerumani kuanzia tarehe 10 Januari, 2019 hadi tarehe 12 Julai, 2019. Mafunzo haya yanaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira) na Baraza la Mazingira (NEMC).
Pia, Jamhuri ya Korea kupitia Program ya Dkt. Lee Jong-Wook imetoa nafasi mbili za ufadhili wa masomo ya muda mfupi kwa wataalam wa tiba kwa kipindi cha kati ya miezi 2 hadi 12. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
06 Aprili, 2018

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.