Friday, April 27, 2018

Tanzania yajikita kutumia fursa za soko la Afrika Mashariki

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akiongea na wawakilishi kutoka kampuni ya Agricom Afrika Ltd walioshiriki maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya yanayoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta Jijini Nairobi, Kenya tarehe 27 Aprili 2018.

=======================================

Tanzania yajikita kutumia fursa za soko la Afrika Mashariki.

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesisitiza kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali za Tanzania na Kenya ili kuhakikisha bidhaa na mazao ya kilimo yanayozalishwa na wananchi yanapata soko la kuaminika katika ukanda wa Afrika Mashariki hususan Kenya.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda alipotembelea maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya, yaliyofunguliwa rasmi na Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Mhe. Mwangi Kiunjuri tarehe 25 April, 2018 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) Jijini Nairobi, Kenya.

Maonesho hayo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Tanzania nchini Kenya ambayo imeambatana na maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Kongamano la biashara kati ya Tanzania na Kenya ambapo lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wafanyabiashara wa mataifa hayo ili waweza kufanya makubaliano ya kibiashara, kupeana uzoefu na kuwezesha bidhaa za viwanda vya Tanzania kupenyeza katika soko la Kenya kama ambavyo bidhaa na huduma za wakenya zilivyoingia katika soko la Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Aidha, aliongeza ushirikiano huo utasaidia kukuza biashara na uwekezaji na hivyo kuongeza ajira, kuinua pato la taifa na kipato cha mtu mmoja mmoja kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla. ‘’ Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa yote na itaendelea kufata taratibu na kanuni za biashara zilizokubaliwa kimataifa” alisema Prof. Mkenda

Vilevile Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji alipata fursa ya kutembelea maonesho hayo ya bidhaa ambapo alisisitiza  umuhimu wa kuthamini bidhaa zetu na kwamba Serikali ya Tanzania na Kenya zitaendelea kuimarisha undugu na mshikamano uliopo kama ilivyokubaliwa na marais wa Tanzania na Kenya walipokutana Kampala, Uganda katika Mkutano wa 19 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo waliwataka viongozi katika nchi zao kumaliza vikwazo vya kibiashara.  “ Serikali itaendelea kuweka mazingira wezesha kwa wafanyabiashara hivyo natoa rai kwa wafanyabiashara wote kufuata taratibu na masharti katika kufanya biashara zao” alisema Prof. Ole Gabriel

Wiki ya Tanzania nchini Kenya imeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia ubalozi wake wa Nairobi, Kenya kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Bara), Wizara ya Viwanda na Biashara (Serikari ya Mapinduzi Zanzibar), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Taasisi ya Sekta Binafsi, Wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa Tanzania ambao walijitoa kwa hali mali katika kudhamini ili kufanikisha Wiki ya Tanzania nchini Kenya.

Prof. Adolf Mkenda pamoja na maafisa waandamizi wa Serikali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wakipata ufafanuzi wa biashara ya matunda na mboga mboga kutoka kampuni ya Agricom.



Prof. Mkenda akipata ufafanuzi wa ubora na matumizi ya mabomba yanayotengenezwa na kampuni ya kitanzania ya PLASCO LTD kutoka kwa Mhandisi Elisaria Aminiel.

Mmoja wa Mabalozi wanaowakilisha nchini Kenya akinunua mkanda kutoka banda la kampuni ya kitanzania inayozalisha bidhaa za ngozi WOISO Original Products, Pembeni ni mwakilishi kutoka kampuni hiyo, Bw. Justine Msigwa.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.