Sunday, April 2, 2017

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama yapitisha Bajeti ya Wizara

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba (wa kwanza kushoto) akiwa na Viongozi wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama meza kuu kabla ya kuanza  kikao. Kamati hiyo imeridhia na kupitisha bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ambayo baadae itawasilishwa mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikao cha Kamati kikiendelea

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhani Mwinyi akifuatilia jambo wakati wa kikao

Naibu Waziri Mhe.Susan Kolimba akizungumza wakati wa Kikao

Saturday, April 1, 2017

Waziri Mkuu wa Ethiopia amaliza ziara nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (kulia) akiagana na Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili nchini. Wakati wa ziara hiyo pamoja na mambo mengine alimaliza kwa kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na Mhe. Dessalegn ameahidi kuitumia Bandari hiyo kupitisha mizigo ya nchi yake pamoja na kufanya biashara na nchi za Afrika Mashariki.Ziara hiyo ilifanyika kuanzia tarehe 31 Machi hadi 01 Aprili, 2017.
Mhe. Dessalegn akiagana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb) akiagana na Mhe. Dessalegn.
Waziri Mkuu, Mhe. Dessalegn akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz mara baada ya kumaliza ziara yake hapa nchini
Waziri Mkuu, Mhe. Dessalegn akiagana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Innocent Shiyo mara baada ya kumaliza ziara yake hapa nchini
Waziri Mkuu Dessalegn akiagana na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Zulekha Tambwe.
 Mhe. Dessalegn akimpungia mkono wa kwaheri Rais Magufuli, viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi (hawapo pichani) waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumuaga  mara baada ya kumaliza rasmi ziara yake nchini.
Rais John Pombe Magufuli (wa kwanza kulia), Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda kwa pamoja wakimpunga mkono wa kwaheri kumuaga Mhe. Dessalegn (hayupo pichani). 

PRESS RELEASE



Friday, March 31, 2017

Tanzania na Ethiopia zakubaliana kukuza ushirikiano

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza wakati wa Mkutano wa Pamoja kati yake na Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia ya Jamhuri ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn (aliyeketi kulia) na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya ushirikiano kati yao.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Workneh Gebeyehu wakisaini Mkataba wa Ushirikiano na ule wa kuanzisha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
==================================================== 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameeleza kuwa ziara ya siku mbili ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn nchini Tanzania ni ya mafanikio makubwa kwa nchi zote mbili.
Rais Magufuli amesema kuwa amejadiliana mambo mengi yenye faida kubwa na mgeni wake huyo walipokuwa katika mazungumzo ya faragha na rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
“Tumezungumza na kukubaliana takriban masuala 13 ambayo yatakapotekelezwa yatakuwa na faida kubwa kwa pande zote mbili.” Rais Magufuli alisema.
Masuala hayo ni pamoja na ushirikiano katika masuala ya usafiri wa anga ambapo  Shirika la Ndege la Ethiopia litashirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika masuala mbalimbali ikiwemo mafunzo na matengenezo ya ndege.
Shirika hilo la Ethiopia ambalo kwa sasa lina ndege takriban 96 zinazofanya kazi na nyingine 42 zipo katika mchakato wa ununuzi limepanga pia kufungua kituo kikubwa kuliko vyote Barani Afrika cha kuhifadhi mizigo hapa nchini. Mizigo hiyo ambayo itapokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam na kusambazwa nchi husika kupitia Shirika la Ndege la Ethiopia.  
Masuala mengine yaliyoafikiwa ni pamoja na kushirikiana katika uwekezaji wa viwanda vya ngozi, nyama, na maziwa kwa kuwa Tanzania na Ethiopia ni moja ya nchi zenye mifugo mingi Barani Afrika.
Viongozi hao pia walizungumzia matumizi ya maji ya Mto Nile na kusisitiza kuwa matumizi ya maji hayo lazima yanufaishe nchi zote. Kwa kuzingatia hilo Tanzania imeipongeza Ethiopia kwa kujenga Bwawa la Gilgel Gibe la kuzalisha umeme wa MW 1870 pamoja na bwawa kubwa kabisa Barani Afrika la The Grand Ethiopian Renaissance ambalo litakuwa na uwezo wa kuzalisha MW 6400 litakapokamilika.
Ethiopia imeahidi kuiuizia Tanzania MW 400 kwa bei nafuu kabisa. Rais Magufuli alisema mpango huo utakapokamilika utatoa ushindani kwa TANESCO kwa kuwa bei za umeme wa shirika hilo zipo juu kidogo. Kwa sasa umeme unaozalishwa Tanzania hauzidi MW 1500.
Aidha, Mhe. Dessalegn ameahidi kutuma wataalamu wake nchini kuja kufanya utafiti wa maeneo ambayo Tanzania inaweza kujenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme kama huo.
Ili kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, Serikali ya Ethiopia imepanga kufungua Ubalozi hivi karibuni mjini Dodoma ambapo Rais Magufuli ameahidi kutoa eneo bure kwa ajili ya ujenzi. 
Sanjari na hayo, Mhe. Dessalegn ameahidi kukiendeleza Kiswahili ambapo atachagua chuo kikuu kimoja nchini Ethiopia kifundishe somo hilo. Kwa upande wake Rais Magufuli ameahidi kutoa walimu wa kufundisha somo la Kiswahili katika chuo kitakachochaguliwa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia alieleza kuwa Tanzania na Ethiopia zina uzoefu wa kutosha, hivyo zikishirikiana katika uzoefu huo zitaendelea kiuchumi bila ya kuzishirikisha nchi nyingine. 
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta zitakazotoa ajira kwa wingi kwa vijana ambao ni takriban asilimia 70 ya watu wote. Alitoa mfano wa sekta hizo kuwa ni pamoja na kilimo ambayo ikiendelezwa vizuri itapunguza umaskini kwa kiasi kikubwa kwa wananchi.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
31 Machi, 2017


Waziri Mkuu wa Ethiopia awasili nchini kuanza ziara ya siku mbili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (kushoto) akimpokea Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia ya Jamhuri ya Ethiopia nchini Mhe. Hailemariam Dessalegn mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Mhe. Dessalegn yupo nchini kwa ziara ya siku mbili ambapo atafanya mazungumzo yake na Rais Magufuli pamoja na kutembelea Bandarini.   
Rais Magufuli pamoja na Mhe. Dessalegn wakiwa kwenye jukwaa tayari kwa kupigiwa nyimbo za taifa.
Waziri Dessalgn akikagua gwaride maalumu lililoandaliwa wakati wa mapokezi yake
Waziri Mkuu Dessalegn akiwapungia mkono wananchi waliojitokeza kumpokea mara baada ya kuwasili.

WAZIRI MAHIGA AWASILISHA UJUMBE MAALUM WA MHE. RAIS MAGUFULI KWA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt. Augustine  Mahiga akiwakilisha Ujumbe Maalum wa Mhe. Rais Magufuli kwa Bi Maria Luiza Ribeiro - Mnadhimu Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani jana

Mhe. Mahiga akitoa maelezo kuhusu ujumbe aliouwasilisha  kutoka kwa Rais Magufuli.
(Kushoto kwa Mhe. Mahiga ni  Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, kulia ni Mhe. Balozi Modest Mero - Mwakilishi wa Kudumu  wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa  na mwisho ni Lt Col George Itang'are - Mwambata Jeshi.
Mhe Mahiga akisindikizwa na Bi  Ribeiro baada ya kumaliza mazungumzo.

Mhe. Mahiga akizungumza na Mabalozi wa nchi za SADC wanaochangia majeshi ya Ulinzi wa Amani - FIB - MONUSCO - DRC.

Mhe. Dkt Augustine Mahiga amewasilisha kwenye Umoja wa Mataifa ujumbe maalumu wa Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaoeleza msimamo wa Wakuu wa Nchi na Serikali ya Nchi za SADC kuhusu kuongezewa muda wa jukumu wa kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO – Force Intervention Brigade - FIB) nchini DRC kinachotarajiwa kumaliza muda wake wa jukumu ifikapo tarehe 31 Machi 2017.

Waziri Mahiga aliwasilisha ujumbe huo kwa Mhe. Maria Luiza Ribeiro, Mnadhimu Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (Chef de Cabinet) kwa niaba ya Mhe. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa safarini nje ya Marekani kikazi.

Akiwasilisha ujumbe huo, Mhe. Mahiga alieleza kuwa, moja ya maazimio ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 18 Machi 2017 nchini Swaziland ni pamoja na Jumuiya ya SADC kufikisha ujumbe kwenye Umoja wa Mataifa wakuunga mkono jitihada zinazofanywa na Umoja wa Mataifa (Baraza la Usalama) kukiongezea muda kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja wa Mataifa kinachotarajia kumaliza muda wake wa jukumu kwa mujibu wa Mkataba tarehe ifikapo 31 Machi 2017.

Mhe. Mahiga alimueleza Bibi Maria kuwa, Jumuiya ya SADC inaupongeza Umoja wa Mataifa kwa jitihada za kuleta amani nchini DRC na kwamba, Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC wana matumaini kuwa kuongezewa muda kwa kikosi hicho kutazingatia mahitaji ya changamoto za usalama zilizopo nchini DRC na hivyo kukiwezesha kikosi hicho kukabiliana na changamoto hizo.
Mhe.Mahiga alitumia nafasi hiyo kueleza hali iliyopo kwa sasa ya ulinzi na usalama katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, ambapo aligusia na kuomba Umoja wa Mataifa kuongeza jitihada za kupatia ufumbuzi wa matatizo yaliyopo nchini DRC na Burundi.

Waziri Mahiga alifanya mazungumzo na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mabalozi wa Nchi zinazochangia vikosi vya Ulinzi na Usalama MONUSCO – FIB nchini DRC, Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa ambaye ni Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa (Pen-holder) wa DRC na Mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa.
Mhe. Mahiga   alitarajiwa kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe30 Machi  2017.







Thursday, March 30, 2017

Waziri Mkuu wa Ethiopia kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba (katikati), akizungumza na waandishi wa habari  (hawapo pichani) juu ya ziara ya siku mbili ya kitaifa ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn nchini. Waziri Mkuu huyo atawasili nchini tarehe 31 Machi, 2017 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Akiwa nchini atakutana kwa mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli pamoja na  kutembelea Bandarini. Wengine katika picha ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Balozi Naimi Aziz (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Innocent Shiyo (kulia).
Sehemu ya Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini mazungumzo ya Dkt. Kolimba (hayupo pichani)
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Aziz naye akielezea jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 


Taarifa kuhusu ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia nchini



Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 31 Machi hadi tarehe 1 Aprili 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Ziara ya Mhe. Dessalegn inakuja kufuatia mkutano kati yake na Mhe. Dkt. Magufuli uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kawaida wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mapema mwaka huu.

 Mhe. Dessalegn anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 31 Machi, 2017 asubuhi na atapokelewa na Mhe. Rais Magufuli. 

Madhumuni ya  ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja ‎na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Dessalegn atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili. Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Jioni ya siku hiyo, Mhe. Dessalegn na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.

Tarehe 01 Aprili, 2017 Mhe. Dessalegn ataendelea na ziara yake kwa kutembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kujionea shughuli mbalimbali Bandarini hapo. Mhe. Dessalegn na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Ethiopia.
Mahusiano ya Tanzania‎ na Ethiopia

Mahusiano ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri. Ethiopia imeonesha nia ya kufungua Ubalozi wake hapa nchini hivi karibuni. Kwa sasa Ethiopia inawakilishwa nchini na Balozi wake aliyepo Nairobi, Kenya. 

Aidha, kumekuwa na ziara za viongozi wa ngazi mbalimbali wa nchi hizi mbili ili kukuza na kudumisha mahusiano. Ziara hizo ni pamoja na ile ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin Mkapa nchini Ethiopia mwaka 2005. Wakati wa ziara hii Mhe. Mkapa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia wakati huo, Hayati Meles Zenawi walisaini Mkataba wa Jumla wa Ushirikiano. 

Vile vile, mwaka 2015 Mhe. Dessalegn alitembelea Tanzania na kushiriki uzinduzi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wanaoeneza Malaria kilichojengwa Kibaha, Pwani kwa ufadhili wa Serikali ya Cuba. Pia, Mhe. Dessalegn alishiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Mhe. Rais Magufuli zilizofanyika mwezi Novemba, 2015 Jijini Dar es Salaam.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
30 Machi, 2017