Friday, March 31, 2017

WAZIRI MAHIGA AWASILISHA UJUMBE MAALUM WA MHE. RAIS MAGUFULI KWA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt. Augustine  Mahiga akiwakilisha Ujumbe Maalum wa Mhe. Rais Magufuli kwa Bi Maria Luiza Ribeiro - Mnadhimu Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani jana

Mhe. Mahiga akitoa maelezo kuhusu ujumbe aliouwasilisha  kutoka kwa Rais Magufuli.
(Kushoto kwa Mhe. Mahiga ni  Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, kulia ni Mhe. Balozi Modest Mero - Mwakilishi wa Kudumu  wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa  na mwisho ni Lt Col George Itang'are - Mwambata Jeshi.
Mhe Mahiga akisindikizwa na Bi  Ribeiro baada ya kumaliza mazungumzo.

Mhe. Mahiga akizungumza na Mabalozi wa nchi za SADC wanaochangia majeshi ya Ulinzi wa Amani - FIB - MONUSCO - DRC.

Mhe. Dkt Augustine Mahiga amewasilisha kwenye Umoja wa Mataifa ujumbe maalumu wa Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaoeleza msimamo wa Wakuu wa Nchi na Serikali ya Nchi za SADC kuhusu kuongezewa muda wa jukumu wa kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO – Force Intervention Brigade - FIB) nchini DRC kinachotarajiwa kumaliza muda wake wa jukumu ifikapo tarehe 31 Machi 2017.

Waziri Mahiga aliwasilisha ujumbe huo kwa Mhe. Maria Luiza Ribeiro, Mnadhimu Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (Chef de Cabinet) kwa niaba ya Mhe. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa safarini nje ya Marekani kikazi.

Akiwasilisha ujumbe huo, Mhe. Mahiga alieleza kuwa, moja ya maazimio ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 18 Machi 2017 nchini Swaziland ni pamoja na Jumuiya ya SADC kufikisha ujumbe kwenye Umoja wa Mataifa wakuunga mkono jitihada zinazofanywa na Umoja wa Mataifa (Baraza la Usalama) kukiongezea muda kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja wa Mataifa kinachotarajia kumaliza muda wake wa jukumu kwa mujibu wa Mkataba tarehe ifikapo 31 Machi 2017.

Mhe. Mahiga alimueleza Bibi Maria kuwa, Jumuiya ya SADC inaupongeza Umoja wa Mataifa kwa jitihada za kuleta amani nchini DRC na kwamba, Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC wana matumaini kuwa kuongezewa muda kwa kikosi hicho kutazingatia mahitaji ya changamoto za usalama zilizopo nchini DRC na hivyo kukiwezesha kikosi hicho kukabiliana na changamoto hizo.
Mhe.Mahiga alitumia nafasi hiyo kueleza hali iliyopo kwa sasa ya ulinzi na usalama katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, ambapo aligusia na kuomba Umoja wa Mataifa kuongeza jitihada za kupatia ufumbuzi wa matatizo yaliyopo nchini DRC na Burundi.

Waziri Mahiga alifanya mazungumzo na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mabalozi wa Nchi zinazochangia vikosi vya Ulinzi na Usalama MONUSCO – FIB nchini DRC, Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa ambaye ni Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa (Pen-holder) wa DRC na Mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa.
Mhe. Mahiga   alitarajiwa kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe30 Machi  2017.







No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.