TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameeleza kuwa ziara ya siku
mbili ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn nchini Tanzania ni
ya mafanikio makubwa kwa nchi zote mbili.
Rais Magufuli amesema kuwa
amejadiliana mambo mengi yenye faida kubwa na mgeni wake huyo walipokuwa katika
mazungumzo ya faragha na rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
“Tumezungumza na kukubaliana
takriban masuala 13 ambayo yatakapotekelezwa yatakuwa na faida kubwa kwa pande
zote mbili.” Rais Magufuli alisema.
Masuala hayo ni pamoja na
ushirikiano katika masuala ya usafiri wa anga ambapo Shirika la Ndege la Ethiopia litashirikiana na
Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika masuala mbalimbali ikiwemo mafunzo
na matengenezo ya ndege.
Shirika hilo la Ethiopia ambalo
kwa sasa lina ndege takriban 96 zinazofanya kazi na nyingine 42 zipo katika
mchakato wa ununuzi limepanga pia kufungua kituo kikubwa kuliko vyote Barani
Afrika cha kuhifadhi mizigo hapa nchini. Mizigo hiyo ambayo itapokelewa katika
Bandari ya Dar es Salaam na kusambazwa nchi husika kupitia Shirika la Ndege la
Ethiopia.
Masuala mengine yaliyoafikiwa ni
pamoja na kushirikiana katika uwekezaji wa viwanda vya ngozi, nyama, na maziwa
kwa kuwa Tanzania na Ethiopia ni moja ya nchi zenye mifugo mingi Barani Afrika.
Viongozi hao pia walizungumzia
matumizi ya maji ya Mto Nile na kusisitiza kuwa matumizi ya maji hayo lazima
yanufaishe nchi zote. Kwa kuzingatia hilo Tanzania imeipongeza Ethiopia kwa
kujenga Bwawa la Gilgel Gibe la kuzalisha umeme wa MW 1870 pamoja na bwawa
kubwa kabisa Barani Afrika la The Grand Ethiopian Renaissance ambalo litakuwa na uwezo wa kuzalisha MW
6400 litakapokamilika.
Ethiopia
imeahidi kuiuizia Tanzania MW 400 kwa bei nafuu kabisa. Rais Magufuli alisema
mpango huo utakapokamilika utatoa ushindani kwa TANESCO kwa kuwa bei za umeme
wa shirika hilo zipo juu kidogo. Kwa sasa umeme unaozalishwa Tanzania hauzidi
MW 1500.
Aidha,
Mhe. Dessalegn ameahidi kutuma wataalamu wake nchini kuja kufanya utafiti wa
maeneo ambayo Tanzania inaweza kujenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme kama huo.
Ili
kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, Serikali ya Ethiopia
imepanga kufungua Ubalozi hivi karibuni mjini Dodoma ambapo Rais Magufuli
ameahidi kutoa eneo bure kwa ajili ya ujenzi.
Sanjari na hayo, Mhe. Dessalegn
ameahidi kukiendeleza Kiswahili ambapo atachagua chuo kikuu kimoja nchini Ethiopia
kifundishe somo hilo. Kwa upande wake Rais Magufuli ameahidi kutoa walimu wa
kufundisha somo la Kiswahili katika chuo kitakachochaguliwa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa
Ethiopia alieleza kuwa Tanzania na Ethiopia zina uzoefu wa kutosha, hivyo zikishirikiana
katika uzoefu huo zitaendelea kiuchumi bila ya kuzishirikisha nchi nyingine.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa
kuendeleza sekta zitakazotoa ajira kwa wingi kwa vijana ambao ni takriban
asilimia 70 ya watu wote. Alitoa mfano wa sekta hizo kuwa ni pamoja na kilimo
ambayo ikiendelezwa vizuri itapunguza umaskini kwa kiasi kikubwa kwa wananchi.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
31 Machi, 2017
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.