Monday, March 6, 2017

Waziri Mahiga azungumza rasmi na Mabalozi kuhusu kuhamia Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akiongea na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yanayowakilisha hapa nchini (hawapo pichani) kwenye kikao kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Aziz P.Mlima. Katika kikao hicho Mhe. Mahiga aliwaeleza rasmi kuhusu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma na kuwaomba nao kuwa tayari kuutekeleza.

Sehemu ya Mabalozi wakifuatilia kikao
Sehemu nyingine ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakifuatilia kikao.
Kikao kikiendelea
Mkuu wa Mabalozi  ambaye pia ni Balozi wa Angola nchini, Mhe. Ambrosio Lukoki (kushoto) akizungumza katika kikao hicho. Pamoja na mambo mengine alieleza kuwa Jumuiya ya wanadiplomasia imelipokea agizo la Makao Makuu ya Nchi kuhamia Dodoma na kwamba wapo tayari kushiriki katika hatua zote za maandalizi ya kuhamia Dodoma ili kufanikisha zoezi la kuhama na kuisaidia Serikali katika huduma za ushauri na uzoefu wa namna nzuri ya kuhamisha miji mikuu.
Kulia ni Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Grace Martin na Balozi Mlima wakifuatilia kikao.
Sehemu ya Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kikao.
Balozi wa Malawi nchini Mhe. Hawa Ndilowe akichangia hoja katika kikao hicho.
Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida naye akichangia hoja katika kikao.
Kikao kikiendelea.





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Balozi Mahiga aongea na Mabalozi kuhusu kuhamia Dodoma

Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wa hapa nchini wametakiwa kuyahimiza makampuni ya nchi yao kutumia fursa za uwekezaji zinazotokana na zoezi la Serikali la kuhamia Dodoma. 
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) katika kikao maalum cha kuwafahamisha wanadiplomasia hao uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuhamia Dodoma.
“Uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali mjini Dodoma umetengeneza fursa nyingi za uwekezaji katika maeneo mbalimbali kama vile utengenezaji wa vifaa vya ujenzi; ujenzi wa majengo ya ofisi, biashara na makazi; huduma za kijamii kama hospitali, shule, miundombinu ya maji safi na maji taka; TEHAMA; bustani za mapunziko; shughuli za kilimo na utalii. Hivyo, nachukua fursa hii kuwaomba muwahimize wawekezaji kutoka nchi zenu kuchangamkia fursa hizo”, Balozi Mahiga aliwambia wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
Balozi Mahiga alieleza kuwa uamuzi wa kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka Dar Es Salaam kwenda Dodoma ulifanywa mwaka 1973 lakini tokea kipindi hicho haukuweza kutekelezwa kutokana na sababu mbalimbali hadi Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilipoingia madarakani.
Mhe. Waziri alieleza kuwa zoezi la Serikali kuhamia Dodoma limepangwa kutekelezwa kwa awamu nne ambapo awamu ya kwanza tayari imeshakamilika. Katika awamu hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imehamisha watumishi 47 kati ya 152 waliopo Makao Makuu akiwemo yeye mwenyewe, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. 
Waziri Mahiga aliendelea kueleza kuwa kufuatia kuanza utekelezwaji wa uamuzi huo ambao ulitangazwa rasmi na Mhe. Magufuli alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM tarehe 23 Julai 2016, hakuna budi kwa Ofisi za Balozi na Mashirika ya Kimataifa nazo zianze kujiandaa kwa ajili ya kuhamia mji huo Mkuu wa Serikali.  
Aliongeza kuwa, katika kipindi hiki cha mpito, baadhi ya Watumishi wa Wizara watakuwepo Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine watasaidia mawasiliano na ofisi hizo. Aidha, katika kipindi hicho, Wizara katika ofisi zake mpya zilizopo kwenye Jengo la LAPF mjini Dodoma itaimarisha mawasiliano kwa njia ya simu, mtandao wa internet na kufunga kifaa cha kufanyia mikutano kwa njia ya video ili kurahisisha mawasiliano na ofisi za Balozi.
Mhe. Mahiga aliwafahamisha Mabalozi hao kuwa Serikali itatenga eneo maalum ambalo litakuwepo kwenye mji wa Serikali utakaojengwa Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za balozi na mashirika ya kimataifa.  Alisema pindi Serikali itakapokamilisha zoezi la kupitia upya Mpango Mkuu wa Mji wa Dodoma, itawasiliana na Balozi hizo ili ziweze kuwasilisha maombi ya mahitaji ya ardhi wanayohitaji.
Balozi Mahiga alihitimisha kikao hicho kwa kuwashauri wanadiplomasia wanaomiliki majengo jijini Dar es Salaam kuingia makubaliano maalum na kampuni zinazohitaji ofisi hapa jijini ili kampuni hizo ziwajengee majengo ya ofisi mjini Dodoma. 
Kwa ujumla wanadiplomasia walipokea uamuzi huo na kuiomba Wizara iwasilishe taarifa hiyo kwa maandishi ili nao waiwasilishe kwenye Serikali zao kwa ajili ya utekelezaji.
                                                                                                                                                                         
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 06 Machi 2017.


                                                                                                                                                                         

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.