Thursday, March 30, 2017

Waziri Mkuu wa Ethiopia kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba (katikati), akizungumza na waandishi wa habari  (hawapo pichani) juu ya ziara ya siku mbili ya kitaifa ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn nchini. Waziri Mkuu huyo atawasili nchini tarehe 31 Machi, 2017 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Akiwa nchini atakutana kwa mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli pamoja na  kutembelea Bandarini. Wengine katika picha ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Balozi Naimi Aziz (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Innocent Shiyo (kulia).
Sehemu ya Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini mazungumzo ya Dkt. Kolimba (hayupo pichani)
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Aziz naye akielezea jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 


Taarifa kuhusu ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia nchini



Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 31 Machi hadi tarehe 1 Aprili 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Ziara ya Mhe. Dessalegn inakuja kufuatia mkutano kati yake na Mhe. Dkt. Magufuli uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kawaida wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mapema mwaka huu.

 Mhe. Dessalegn anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 31 Machi, 2017 asubuhi na atapokelewa na Mhe. Rais Magufuli. 

Madhumuni ya  ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja ‎na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Dessalegn atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili. Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Jioni ya siku hiyo, Mhe. Dessalegn na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.

Tarehe 01 Aprili, 2017 Mhe. Dessalegn ataendelea na ziara yake kwa kutembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kujionea shughuli mbalimbali Bandarini hapo. Mhe. Dessalegn na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Ethiopia.
Mahusiano ya Tanzania‎ na Ethiopia

Mahusiano ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri. Ethiopia imeonesha nia ya kufungua Ubalozi wake hapa nchini hivi karibuni. Kwa sasa Ethiopia inawakilishwa nchini na Balozi wake aliyepo Nairobi, Kenya. 

Aidha, kumekuwa na ziara za viongozi wa ngazi mbalimbali wa nchi hizi mbili ili kukuza na kudumisha mahusiano. Ziara hizo ni pamoja na ile ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin Mkapa nchini Ethiopia mwaka 2005. Wakati wa ziara hii Mhe. Mkapa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia wakati huo, Hayati Meles Zenawi walisaini Mkataba wa Jumla wa Ushirikiano. 

Vile vile, mwaka 2015 Mhe. Dessalegn alitembelea Tanzania na kushiriki uzinduzi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wanaoeneza Malaria kilichojengwa Kibaha, Pwani kwa ufadhili wa Serikali ya Cuba. Pia, Mhe. Dessalegn alishiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Mhe. Rais Magufuli zilizofanyika mwezi Novemba, 2015 Jijini Dar es Salaam.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
30 Machi, 2017


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.