Wednesday, August 9, 2017

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kutembelea Tanzania

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari, kuhusu ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Patricia Scotland anayewasili nchini tarehe 10 - 12 Agosti, 2017
Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Deusidedit Kaganda.Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Habari na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Mindi Kasiga
Juu na chini ni sehemu ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Taarifa kuhusu ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola nchini

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mheshimiwa Patricia Scotland anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 10 hadi 12 Agosti, 2017. 

Lengo la ziara hiyo ni kueleza Viongozi wa Ngazi za Juu wa Taifa kuhusu  mageuzi yanayofanywa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na vipaumbele vya Jumuiya hiyo kwa sasa; Hatua zinazochukuliwa ili kuimarisha kazi za Jumuiya hiyo na kutoa taarifa kuhusu Mkutano wa Wakuu Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kufanyika London, Uingereza mwezi Aprili, 2018.

Mageuzi hayo yanajumuisha kuondoa vyeo vya Naibu Makatibu Wakuu watatu na kupunguza idadi ya Wakurugenzi kutoka 12 hadi 6. Mageuzi haya yataiwezesha Jumuiya kuokoa kiasi cha Pauni milioni 3 kwa mwaka. Mageuzi mengine ni ya kuanzisha nafasi tano za Maafisa Waandamizi kutoka maeneo ya kijiografia ya Jumuiya ya Madola kwa maana ya Afrika, Ulaya na Amerika, Karibeani, Asia na Pacific Kusini. Nafasi hizi zitaziba zile za Naibu Makatibu Wakuu.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Scotland atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo tarehe 11 Agosti, 2017, Ikulu, Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Scotland ataonana na Mawaziri mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. January Makamba, Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mhe. Scotland na ujumbe wake wataondoka nchini tarehe 12 Agosti, 2017 kuelekea Msumbiji.

Historia fupi kuhusu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Patricia Scotland alichaguliwa kwenye nafasi hiyo mwezi Novemba, 2015 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (CHOGM) uliofanyika nchini Malta. Kabla ya kuchaguliwa kwake Jumuiya hiyo iliongozwa na Bw. Kamalesh Sharma ambaye alishikilia nafasi hiyo kuanzia mwaka 2008 hadi 2016.

Jumuiya ya Madola

Jumuiya ya Madola ni Umoja ulioanzishwa mwanzoni mwa karne ya 20. Jumuiya hiyo inajumuisha Uingereza pamoja na nchi ambazo zilikuwa koloni la Uingereza. Uanachama wa Jumuiya hiyo kwa sasa hauzingatii kigezo cha koloni hivyo nchi yoyyote inaweza kujiunga na Jumuiya ya Madola kama itapenda. Malkia ndiye Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Madola.

Jukumu kubwa la Jumuiya ya Madola ni kuhakikisha nchi wanachama zinajikwamua kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kutumia jukwaa la majadiliano, makubaliano na utekelezaji.

Ushiriki wa Tanzania katika Jumuiya ya Madola


Jumuiya ya Madola inajumuisha nchi 52 Tanzania ikiwa ni mwanachama wa Jumuiya hiyo tangu mwaka 1961. Tangu kujiunga kwake, Tanzania imewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Jumuiya hiyo. Miongoni mwa nafasi hizo ni ile ya Uenyekiti wa Kundi la Mawaziri la Utekelezaji la Jumuiya ya Madola (Commonwealth Ministrial Action Group (CMAG). Kundi hili lilijumuisha Mawaziri tisa ambao walipewa jukumu la kusimamia misingi mikuu ya Jumuiya ya Madola. Tanzania ilishikilia nafasi hii kuanzia mwaka 2013 hadi 2015.

Pia Tanzania ni mjumbe kwenye Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA). Kutokana na mchango mkubwa wa Tanzania kwenye Jumuiya ya Madola, kuanzia mwaka 2007 hadi 2014 Marehemu Dkt. William F. Shija aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Bunge hilo. Aidha, mwaka 2009 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 55 wa Bunge la Jumuiya ya Madola uliofanyika Jijini Arusha.

Aidha, miongoni mwa faida ambazo Tanzania imepata kutokana na kujiunga na Jumuiya hii ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji na nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola zikiwemo Uingereza, India, Kenya na Afrika Kusini. Nchi hizi ni miongoni mwa  nchi  zilizowekeza zaidi kwa biashara nchini Tanzania.

Tanzania imenufaika kwenye masuala ya  Teknolojia kupitia Taasisi ya Commonwealth of Learning (COL) ambayo inahamasisha mafunzo ya wazi na ya mbali miongoni mwa nchi wanachama. Pia Jumuiya ya Madola ina  mchango mkubwa kwenye mageuzi katika  Sekta ya Umma na utoaji mafunzo, kozi na misaada mbalimbali ya kiufundi kupitia Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na Mfuko wa ushirikiano wa Kiufundi wa  Jumuiya ya Madola (CFTC).

Tanzania imekuwa mshiriki mzuri wa michezo maarufu ya Jumuiya ya Madola ambayo inalenga kuhamasisha ushirikiano na urafiki miongoni mwa nchi wanachama. Itakumbukwa kuwa mwaka 1974 Bw. Filbert Bayi alivunja rekodi  kwa kukimbia mita 1,500 mashindano yaliyofanyika huko Christchurch, New Zealand. 

Michezo ya Madola hufanyika kila baada ya miaka minne. Tanzania inajiandaa kushiriki kwenye michezo  ya Madola itakayofanyika mwezi Aprili, 2018 huko Gold Coast, Australia.

-Mwisho-

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam

09 Agosti, 2017

Monday, August 7, 2017

Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameitaja tarehe ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania kuwa ni siku ya maendeleo ya kweli kwa Tanzania na Uganda na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.

Uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo litakalokuwa na urefu wa kilomita 1445 litakalogharimu takribani Shilingi trilioni 8 za Tanzania ulifanywa na Rais Magufuli na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga siku ya Jumamosi tarehe 05 Agosti 2017 na kushuhudiwa na umati mkubwa wa watu wakiwemo viongozi wakuu wa Serikali na vyama vya siasa kutoka pande zote mbili.

Rais Magufuli alieleza kuwa hadi kufikia hatua ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa bomba hilo, vikwazo vingi vilijitokeza, hivyo anamshukuru Rais Museveni kwa kuipa kipaumbele Tanzania kwa kuwa bomba hilo lingeweza kupita mahali pengine ambako umbali ungekuwa mfupi kwa zaidi ya kilomita 500.

Aliendelea kueleza kuwa licha ya Tanzania kutoa vivutio vingi kwa Uganda ikwemo kusamehe baadhi ya kodi kama za ongezeko la thamani lakini ujenzi wa bomba hilo utakuwa na manufaa makubwa kwaTanzania katika kipindi cha ujenzi unaotarajiwa kuanza mwezi Januari 2018 na kukamilika mwaka 2020 na baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.

"Tutapata mamilioni ya Dola yatakayotokana na ada ya usafirishaji ambayo ni Dola 12.5 kwa pipa moja na inakadiriwa kwa siku yatasafirishwa mapipa 216,000". Rais Magufuli alisema.

Manufaa mengine ni pamoja na ajira ambapo inakadiriwa watu kati ya elf 10 hadi 15 watapata ajira za kudumu bomba litakapokamilika na ajira za muda mfupi za watu zaidi ya elf 30 katika kipindi cha ujenzi.

Aidha, bomba litakuza biashara ya bidhaa mbalimbali ikiwemo saruji na vifaa vingine vitakavyotumika katika ujenzi wa bomba,  ujenzi wa nyumba za kupangisha na kuchochea ujenzi wa viwanda ambavyo malighafi zake zinatokana na mabaki yanayotokana na usafishaji wa mafuta kama vile viwanda vya mbolea. 

Vile vile, bomba linatarajiwa kupunguza gharama za uendeshaji katika sekta ya anga kutokana na unafuu wa mafuta na linakuja wakati mwafaka kwa kuwa Tanzania imeshaanza kulifufua shirika lake la ndege na Uganda ipo mbioni pia kulifufua shirika lake. Imeelezwa kuwa moja ya sababu ya Mashirika ya ndege ya nchi za Mashariki ya Kati kufanya vizuri kibiashara inatokana na unafuu wa mafuta ya ndege.

Mhe. Rais alitoa wito kwa wakandarasi watakaojenga bomba hilo kuharakisha  ujenzi ili uweze kukamilika kabla ya muda uliopangwa wa miaka mitatu.

"Kuna sababu gani ya kutumia muda wote huo wakati fedha zipo na wakandarasi wote mnatoka nchi kubwa zilizopiga hatua ya maendeleo, Tuoeni zabuni kwa wakandarasi wengini (sub contractors) ili ujenzi ukamilike kwa muda mfupi". Rais Magufuli alishauri. 

Wakandarasi watatu, wawili kutoka Ufaransa, Total na Cnooc na mwingine kutoka Uingereza, Tullow Oil kwa pamoja watajenga bomba hilo.

Mhe. Magufuli alibainisha kuwa Tanzania na Uganda zipo katika mazungumzo ili wataalamu wa Kiganda waliogundua mafuta hayo mwaka 2006 waje Tanzania kufanya utafiti kwenye maziwa ya Tanganyika na Eyasi ambayo yana viashiria vya kuwepo kwa mafuta.

Rais Magufuli alihitimisha hotuba yake kwa kumuhakikishia Mhe. Museveni kuwa Tanzania ni nchi iliyokamilika kiulinzi, hivyo Waganda wasiwe na wasi wasi kuhusu usalama wa bomba hilo ambalo litapita katika mikoa 8 ya Tanzania , wilaya 24 na vijiji 124.

Kwa upande wake, Rais Museveni aliishukuru Tanzania kwa kutoa vivutio vingi ili ujenzi wa bomba hilo uendelee kwani bila ya hivyo mafuta hayo hayatakuwa na faida ukizingatia bei ya mafuta katika soko la dunia imeshuka.

Alisema sababu kubwa ya bara la Afrika kuwa masikini hadi leo ni kutumia bidhaa isiyozalisha na kuzalisha bidhaa isiyotumia. 

Kwa mujibu ya takwimu alizotoa, nchi za Afrika Mashariki zinaagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 33 na inauza bidhaa zenye thamani ya Dola milioni 13.8 tu kwa mwaka. Fedha hizo zinafaidisha nchi zilioendelea kuimarisha uchumi wao na kuziacha nchi za Afrika kubaki masikini.

Kutokana na hali hiyo, Rais Museveni alizisihi nchi za Afrika zibadilishe mfumo wa uchumi kwa kujenga viwanda na kuuziana bidhaa. Hivyo, ana matumaini makubwa  kuwa ujenzi wa bomba hilo litaongeza kipato kitakachotumika kuchochea mabadiliko ya kiuchumi ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Martine Shigella aliwahakikishia Marais wawili kuwa mkoa umejipanga kutoa huduma stahiki kwa wageni wote watakaoingia mkoani humo kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo.

"Tumejipanga kuzalisha chakula cha kutosha na tumetenga maeneo ya kujenga nyumba za makazi, hivyo wawekezaji jitokezeni kuchukua maeneo hayo". Mkuu wa Mkoa alihimiza. Aliwasihi watu wa Tanga wasomeshe watoto wao ili waweze kuwa na vigezo vya kupata ajira zitakazotokana na ujenzi wa bomba hilo.

Alihitimisha kwa kumuomba Rais Magufuli asaidie kuimarisha bandari ya Tanga angalau iwe na kina cha mita 12 ili iweze kuhudumia meli zote zitakazotumika kubeba shehena za vifaa vya kujengea bomba la mafuta.


 -Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Tanga, 05 Agosti, 2017.

Viongozi Wakuu wa Serikali wakiwa katika mstari kwa ajili ya kuwapokea Waheshimiwa Marais wa Tanzania na Uganda kwenye viwanja vilivyofanyika hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania. Mwenye ushungi ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Madam Balozi Grace Martin, Mkuu wa Itifaki

Rais wa Jamhuri ya Muungno wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) akiwa kwenye Meza Kuu na Mgeni wake, Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni (katikati) na Makamu wa Rais, Mama Samia Hassan Suluhu.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Martine Shigella akitoa neno la ukaribisho kwa Marais wa Uganda na Tanzania na wageni waalikwa waliohudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta iliyofanyika katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga tarehe 05 Agosti 2015.

Bw. Guy Mourice, Rais wa Kampuni ya Total na Msimamizi  wa ujenzi wa bomba hilo akitoa maelezo mafupi kuhusu ujenzi wa bomba hilo utaskavyotekelezwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Mhe. Abdulrahman Kinana akiwasalimia viongozi na wananchi waliofurika viwanjani hapo kushuhudia hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta.

AWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi.

Makamu wa Rais, Mhe. Samia Hassan Suluhu akiwasalimia wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Uganda akisoma hotuba yake kwenye hafla ya uwekasji wa jiwe las msingi la ujenzi wa bomba ls mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisoma hotuba katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa bomba lamfuta kutoka Uganda hadi Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mhe. Paul Makonda akipeana Mkono na Bw. Ruge Mutahaba wa Cloud FM. Wawili hao walitakiwa  na Mhe. Rais Magufuli kumaliza tofauti zao.

Viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wabunge walioshiriki hafla hiyo.

Sehemu ya umati wa wananchi waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi.

Burdani ndani ya viwanja vya Chongoleani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakiweka jiwe la Msingi kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Waheshimiwa Marasi wakishikana mikono baada ya kuweka jiwe la msingi.

Thursday, August 3, 2017

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kifaru

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba akizungumza na Dkt. Viktor Korcek, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kifaru ambaye pia ana nia ya kuwa Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech.
Mazungumzo yakiendelea
Dkt. Korcek nae akimweleza jambo Dkt. Kolimba.
Picha ya pamoja


Monday, July 31, 2017

Waziri Mahiga akutana na Mchungaji Ongere

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akisalimiana na Mchungaji John Oscar Ongere ambaye alifika ofisini kwa Mhe. Waziri kujadili maandalizi ya Kongamano kubwa la uwekezaji linalotarajiwa kufanyika nchini mwezi Novemba 2017..Kongamano hilo litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam litajumuiya wafanyabiashara wakubwa kutoka kote duniani na wa hapa nchini kujadiliana namna bora ya kutumia fursa lukuki za uwekezaji zilizopo hapa nchini.

Mchungaji Ongere akifanya maombi kwa ajili ya kuiombea nchi amani na utulivu ili iweze kukua kiuchumi
Picha ya pamoja
 Balozi wa Iran
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mhe. Mousa Farhang ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo.  Mazungumzo yao pamoja na mambo mengine walijadili maandalizi ya sherehe za kumuapisha Rais Mteule wa Iran, Mhe. Hassan Rouhani zitakazofanyika Tehran tarehe 05 August 2017.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo hayo, Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Bi. Zainab Angovi-Mrutu, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Bw Ayoub Mndeme na Katibu wa Waziri, Bw. Gerald Mbwafu.

Ujumbe aliofuatana nao Balozi wa Iran ukifuatilia mazungumzo.

Saturday, July 29, 2017

Balozi Mahiga apokea Nakala za Hati za Utambulisho za Balozi mteule wa Uganda

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Richard Tumusiime Kabonero katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera, leo tarehe 29/07/2017. Waziri Mahiga yupo Mkoani Kagera kwaajili ya kuhudhuria Mkutano wa Ujirani mwema Kati ya Tanzania na Uganda. 
Waziri Mahiga akizungumza na Balozi Mteule Kabonero
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mej.Gen. Salum M. Kijuu ( wa pili kutoka kulia), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga ( wa kwanza kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Grace Mgavano (wa pili kutoka kushoto) na Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, nao walikuwepo kushuhudia tukio hilo
Balozi Mgavano akisalimiana na Balozi Mteule Kabonero
Waziri Mahiga akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kupokea nakala za utambulisho za Balozi Mteule Mhe. Kabonero.

Friday, July 28, 2017

KIKAO CHA MAKATIBU WAKUU CHA UJIRANI MWEMA BAINA YA TANZANIA NA UGANDA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Aziz Mlima akizungumza wakati akifungua mkutano wa ujirani mwema kati ya Tanzania na Uganda, ngazi ya Makatibu Wakuu. Mkutano huo unao jadili pia masuala ya mpaka umefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa ELCT Mjini Bukoba, Mkoani Kagera.
Ujumbe kutoka nchi ya Uganda wakifuatilia kwa makini hotuba ya Dkt. Mlima (hayupo pichani),  alipokuwa akizungumza wakati wa ufunguzi.
Ujumbe wa upande wa Tanzania nao wakimsikiliza kwa makini Dkt. Mlima (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, wa kwanza kutoka kulia ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Gerson Mdemu (wa kwanza kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome, na wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi Dr. Florens Turuka
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda  Balozi Patrick Mugoya naye akizungumza kwenye ufunguzi  wa Mkutano huo kati ya Tanzania na Uganda kwa ngazi ya Makatibu wa Kuu.
Dkt. Mlima (katikati) akitoa miongozo ya kikao hicho, wa kwanza kulia ni Bw. Suleiman Salehe (kulia), Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wa kwanza kushoto ni  Balozi Mugoya.
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania ukisikiliza  kwa makini miongozo iliyokuwa inatolewa na Dkt. Mlima (hayupo pichani).
Sehemu ya Makatibu wa Kuu upande wa Uganda, nao wakisikiliza kwa makini miongozo iliyokuwa ikiendelea kutolewa na Dkt. Mlima (hayupo pichani), wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Uganda, na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Mazingira Uganda.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera Naibu Kamishina Jeremiah M. Nkondo (wa kwanza kulia) pamoja na Naibu Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera Bw. Butenge  Christopher.


Tanzania kuimarisha mipaka yake na nchi jirani

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi (Mb.), katikati, anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye ziara ya kutembelea na kujifunza juu ya mipaka iliyopo kati ya Tanzania na Uganda. Watatu kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Isaack Kamwele, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Suzan Kolimba (wa tatu kutoka kulia), Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima (wa pili kutoka kulia), Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe Gerson John Mdemu (wa kwanza kulia) na wa kwanza kushoto ni Bw. Deogratias Nholope, wakitizama Mto Kagera ulipopita.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Suzan Kolimba akisalimiana na wanakijiji wanaoishi mpakani mwa Tanzania na Uganda, mara baada ya kuwasili kwenye eneo hilo na kujionea alama za mipaka.
Mhe. Lukuvi pamoja na ujumbe wa Manaibu Waziri wakisalimiana na wanakijiji wa pande zote mbili, ambapo wananchi hao walionekana kufurahishwa na ziara hiyo.
Mhe. Lukuvi pamoja na ujumbe alioambatana nao, wakiwemo wataalamu kutoka sekta mbalimbali nchini Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja.
Mhe. Lukuvi akijadiliana jambo na Manaibu Waziri alioambatana nao kwenye ziara ya kujifunza na kujionea mipaka iliyopo kati ya Tanzania na Uganda. Wa pili kutoka kulia ni Mhe. Dkt. Susan Kolimba Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mhandisi Isaack Kamwelwe Naibu Waziri wa Maji (wa pili kutoka kulia), na Naibu Waziri wa TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Jafo Selemani Said (wa kwanza kulia).
Ziara ikiendelea ambapo Ujumbe ulioongozwa na Mhe. Lukuvi alipata fursa ya kutembelea majengo yanayotumika kwenye kukagua mizigo na kukusanya ushuru wa forodha kati ya Tanzania na Uganda yanayopatikana eneo la Mtukula.
Picha ya pamoja ya ujumbe wa viongozi na wataalam wa Tanzania ulioongozwa na Waziri Lukuvi wakiwa kwenye moja ya alama iliyopo mpakani mwa Tanzania na Uganda.