Monday, March 26, 2018

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU RAIA WA TANZANIA NCHINI OMAN


Kuna kipande cha video kinasambaa mitandaoni kikiwa na maelezo kuwa raia wa Tanzania wanaoishi nchini Oman wamekusanyika ofisi ya Ubalozi kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso na adhabu kali wanazopata kutoka kwa mabosi wao.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kutazama kipande hicho cha video iliwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Oman kwa madhumuni ya kujua usahihi wa jambo hilo.

Ubalozi ulitoa ufafanuzi kuwa uliandaa mkutano wa Watanzania wote wanaoishi Oman na ulipangwa kufanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Muscat tarehe 23 Machi 2018. Matangazo ya mkutano huo yalitaka Watanzania watakaopenda kushiriki wajisajili kabla ya siku ya mkutano. Watanzania takriban 200 walijisajili na ubalozi ulifanya maandalizi ya ukumbi, vyakula na vinywaji kwa ajili ya watu 300 kwenye hoteli ya Golden Tulip.

Siku ya mkutano ilipowadia, Watanzania zaidi ya elfu moja walijitokeza na kusababisha ugumu wa kuendelea na mkutano kutokana na maandalizi yaliyofanywa yalilenga watu 300.

Kamati ya maandalizi ilipoona ukumbi umejaa na watu walio nje ni weng mara mbili zaidi ya watu waliokuwemo ndani ya ukumbi iliamua kufunga milango na kuwaomba waliochelewa warejee nyumbani.

Uamuzi huo haukuwafurahisha watu waliochelewa, hivyo walishinikiza waingizwe kwenye ukumbi wa mkutano, kitendo ambacho kiliashiria uwezekano wa kutokea vurugu kubwa.

Kutokana na uhalisia huo, Kamati ya maandalizi ambayo ilijumuisha pia viongozi wa Watanzania wanaoishi nchini humo ilishauriana na kuamua kuwa mkutano huo uahirishwe na maandalizi yaanze upya kwa madhumuni ya kupata ukumbi na huduma nyingine zitakazokidhi idadi kubwa ya watu.

Kutokana na ufafanuzi huo, Wizara inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa kipande hicho cha video kimechukuliwa wakati Watanzania wanashinikiza kuingia kwenye ukumbi wa mkutano na sio kwamba wamekusanyika kwenye ofisi ya ubalozi wa Tanzania kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso wanayoyapata.


-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 26 Machi, 2018

Thursday, March 22, 2018

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israeli


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israeli

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Taifa la Israeli Mhe. Avigdor Liberman. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa kupokelea wageni maalum(VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere,Jijini Dar es Salaam, tarehe 22 Machi,2018.

Mazungumzo haya yalijikita zaidi katika kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Israeli. Akiongea katika mazungumzo hayo Waziri Mahiga alisema ziara hii ina maana kubwa sana kwa Tanzania na itazidi kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizi mbili. Kama inavyofahamika nchi ya Israeli ina Utaalam wa hali ya juu  katika maeneo mbalimbali hasa katika masuala ya Ulinzi na Usalama, Kilimo cha Umwagiliaji, mbinu za kisasa za kupambana na Ugaidi, Uhalifu wa Kimtandao na Teknolojia ya tiba na vifaa tiba.

"Tunatarajia Tanzania kunufaika zaidi  na Utaalam huu hasa katika maeneo ya mbinu za Kilimo bora cha umwagiliaji, Teknolojia ya tiba na vifaa tiba, mbinu za kupambana na Ugaidi, Ulinzi wa Mipaka na Uharamia, Biashara na Ushirikiano wa Teknologia na mafunzo mbalimbali ya kujenga uwezo wa Wataalam wa Tanzania hasa katika Sekta ya Viwanda, Afya na Kilimo" alisema Waziri Mahiga.

Naye Mhe. Liberman amesema Israeli inaishukuru Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kulinda Amani ya Dunia hasa kwa kushiriki katika Ulinzi wa amani nchini Lebanon na nchi nyingine za afrika zenye migogoro, na ameahidi nchi yake  itaendelea kuongeza maeneo ya Mashirikiano zaidi na Tanzania. 

Katika Ziara hii Mhe. Liberman alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mhe. Liberman ameondoka tarehe 22 Machi, 2018, kurejea nchini Israeli baada ya Ziara ya siku tatu(3) hapa nchini.




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akifafanua jambo kwa Waziri wa Ulinzi wa Taifa la Israeli ambaye pia ni Naibu Waziri wa Taifa hilo Mhe. Avigdor Liberman walipokutana kwa mazungumzo tarehe 22 Machi,2018, mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa kupokelea wageni Maalum(VIP) Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.



Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati Bw. Ayoub Mdeme na Bi. KisaDoris Mwaseba wakifuatilia mazungumzo hayo
Balozi wa Israeli nchini, ambaye Makazi yake yapo Jijini Nairobi Mhe. Balozi Noah Gal Gendler na Msaidizi wa Viongozi wakiwa katika mazungumzo hayo.
Waziri Mahiga akiagana na Mhe. Liberman baada ya kumaliza mazungumzo, 

Wednesday, March 21, 2018

Waziri wa Ulinzi wa Israeli afanya Ziara Nchini.


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi(Kulia) na Waziri wa Ulinzi wa Taifa la Israeli Mhe. Avigdor Liberman (kushoto) wakizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), baada ya Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Makao Mkuu ya Jeshi (Ngome), Dar es Salaam, tarehe 21 Machi,2018. 


Lengo la mazungumzo hayo ni kuboresha mashirikiano hasa katika eneo la Ulinzi na Usalama, Israeli imekuwa na Ushirikiano na Tanzania wa muda mrefu na imekuwa ikisaidia katika eneo la Ulinzi na Usalama kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa Wanajeshi wa Tanzania kama vile kupambana na ugaidi, Uharamia na Ulinzi wa Mipaka. Pia, kama itakavyokumbukwa katika Miaka ya 60 Israeli ilishiriki kikamilifu katika uanzishwaji wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Katika kuendelea kuboresha Mahusiano kati ya nchi hizi mbili, Tanzania  Mwaka 2017 ilifungua Ubalozi wake katika Mji wa Tel Aviv

Mhe. Avigdor Liberman yuko nchini kwa ziara ya Siku tatu(3), ambapo aliwasili tarehe 20 Machi,2018 na anatarajiwa kuondoka   tarehe 22 Machi,2018 


                  Mkutano ukiendelea
Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi,Mhe. Avigdor Liberman, Balozi wa Israeli nchini mwenye Makazi yake Jijini Nairobi Mhe. Noah Gal Gendler wakiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania pamoja na Ujumbe wa Israeli.

Thursday, March 15, 2018

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje atembelea Ofisi za Kamisheni ya Kiswahili ya EAC Zanzibar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (katikati upande wa kulia), akizungumza na Prof. Kenneth Simala (kushoto), Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.  Pamoja na mambo mengine Prof. Simala alimkabidhi Prof. Mkenda Mpango Mkakati wa Kamisheni hiyo wa mwaka 2017/2022. Kamisheni hiyo ina lengo la kukuza na kutangaza Lugha ya Kiswahili kwa nchi za Afrika Mashariki. Prof. Mkenda alitembelea Ofisi za Kamisheni hiyo zilizopo Zanzibar wakati wa ziara yake ya kujitambulisha kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ni Wizara ya Muungano. Wakati wa ziara


Prof. Mkenda (katikati) akiwa ameshikilia  Mpango Mkakati wa Kamisheni hiyo huku akisikiliza maelezo kutoka kwa Prof. Simala (kulia). Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Mohammed Hamza
Prof. Mkenda (kushoto) akiwa ameongozana na Prof. Simala (wa pili kushoto), Balozi Hamza (mwenye suti) na Maafisa wengine mara baada ya kutembelea Ofisi za Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

Wednesday, March 14, 2018

Prof. Mkenda afanya ziara ya kujitambulisha Zanzibar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kulia) akiagana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ofisini kwa Dkt. Mzee, Zanzibar.  Prof. Mkenda alifanya ziara Zanzibar kwa lengo la  kujitambulisha kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ni Wizara ya Muungano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Amina Salum Ali wakati wa ziara ya Prof. Mkenda ya kujitambulisha.
Balozi Amina Salum Ali akimkabidhi Prof. Mkenda bidhaa za viungo mbalimbali vya chakula vinavyozalishwa Zanzibar
Bidhaa za viungo vya chakula zinazozalishwa Zanzibar.
Katibu Mkuu wa WIzara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na  Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Salum Maulid Salum alipo kwenda kujitambulisha Ofisini kwake Zanzibar hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (wanne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Idara ya  Mambo ya Nje Zanzibar alipofika kuwatembelea wakati wa ziara yake ya kujitambulisha aliyoifanya Visiwani humo hivi karibuni.



Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa akutana na Katibu Mkuu wa WTO


Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Samwel Shelukindo akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Bw. Zurab Pololikashvili. Balozi Shelukindo alikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Pololikashvili ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzia uwezekano wa Shirika hilo kusaidia miradi mbalimbali hapa nchini.
Balozi Shelukindo na wajumbe wengine


Friday, March 9, 2018

Katibu Mkuu akutana na Mabalozi wa Afrika waliopo nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akihutubia kwenye hafla iliyoandaliwa na Umoja wa Mabalozi wa nchi za Afrika nchini Tanzania. Katika hotuba yake Prof. Mkenda aliwashukuru Mabalozi hao kwa kumwalika kwenye hafla hiyo na kuwaahidi kushirikiana nao kwenye shughuli zao za uwakilishi wa mataifa yao hapa nchini.
Balozi wa Misri nchini Mhe. Yasser Ahmed Al Eldin Elshawaf
Balozi wa Algeria nchini, Mhe. Saad Belabeb (kushoto), pamoja na Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica Patricio Clemente wakisikiliza hotuba ya Prof. Mkenda.

Mkurugenzi wa Idara ya Itifaki, Balozi Grace Martin pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hapa nchini, Mhe. Jean Mutamba wakimsikiliza kwa makini Prof. Mkenda hayupo pichani.
Sehemu nyingine ya wageni waalikwa wakifuatilia kwa makini hotuba.

Prof. Mkenda akiendelea kuhutubia kwenye hafla hiyo.
Balozi wa Afrika Kusini akizungumza kama mshereheshaji katika hafla iliyoandaliwa na Umoja wa Mabalozi hao wa Afrika.
Sehemu ya Maafisa kutoka Ofisi mbalimbali za Balozi za Afrika zilizopo nchini.

 


Thursday, March 8, 2018

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan afanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Mh. Li Yong, ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu. 
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb.)na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb.). Mazungumzo hayo yamefanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam, tarehe 08 Machi,2018.
Mhe. Samia Suluhu akimsikiliza Mhe. Yong wakati wa mazungumzo hayo.
Mazungumzo yakiendelea kati ya Mhe. Suluhu na Mhe. Yong, wa kwanza kulia ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mwijage akifuatilia mazungumzo hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (wa kwanza kushoto), Waziri wa Fedha  na Mipango, Mhe. Philip Mpango (katikati) na  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekaji, Bw. Ludovick J. Nduhiye nao wakifuatilia mazungumzo 
Mwakilishi wa UNIDO nchini  Bw. Stephen Kargbo akifuatilia mazungumzo hayo.
Sehemu ya watumishi wa Serikali wakifuatilia mazungumzo hayo.
Mhe. Samia Suluhu akishuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya Mpango shirikishi baina ya nchi, UNIDO na  Washirika wengine wa Maendeleo, wanaosaini Mpango huo kushoto ni Mhe. Waziri  Mwijage na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Bw. Li Young. Mpango huo umesainiwa katika ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, tarehe 08 Machi,2018.
Mhe. Waziri Mwijage na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Bw. Li Yong wakibadilishana Makubaliano hayo baada ya kusainiwa.
Mhe. Samia Suluhu na Mhe. Li Yong katika picha ya pamoja na Viongozi kutoka Serikalini pamoja na uongozi kutoka UNIDO.