Wednesday, December 1, 2021

KIKAO CHA FOCAC DAKAR KIMEKUWA CHA MAFANIKIO - BALOZI MULAMULA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza baada ya kumalzika kwa mkutano wa nane wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)

 


Na Mwandishi wetu, Dakar

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umefanyika kwa mafanikio makubwa.

Balozi Mulamula ametoa kauli hiyo jijini Dakr nchini Senegal baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika Novemba 29 na 30 2021 nchini humo.

Amesema kikao hicho kimekuwa cha mafanikio kwani kimepitisha maazimio makubwa na mpango kazi ambao umejikita katika kutekeleza maeneo ya kimkakati ambayo yakisimamiwa kikamilifu yatazinufaisha nchi za Afrika .

Balozi Mulamula amesema kauli ya China ya kuzihakikishia nchi za Afrika kuwa itasaidia kuanzisha viwanda vya kuzalisha chanjo za COVID 19 pamoja na dawa nyingine ni ya kujivunia na ya kupongezwa.

"Tanzania imefurahishwa na ahadi hiyo kwani jambo hilo litazifanya nchi za Afrika kuwa na uwezo wa kuzalisha chanjo na dawa nyingine kwa ajili ya kuwalinda watu wake na kuacha kutegemea msaada., kauli ya Rais Jinping ni ya kujivunia na ya lupongezwa,"amesema Balozi Mulamula.

Amesema kikao kimekuwa na mafanikio zaidi kwani mbali na kuangalia maeneo ya siku zote ya kuendeleza miundombinu na viwanda, kwa mara ya kwanza umeangalia jinsi ya kusaidia na kuendeleza wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Amesema uamuzi wa China kwa kutoa kipaumbele katika eneo la kujenga viwanda vya kuzalisha dawa na chanjo na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ni wa kupongezwa mno kwani mambo hayo ndiyo ambayo Tanzania ilitilia mkazo katika taarifa yake na kuongeza kuwa wamefarijika kwamba Rais Jinping ameahidi kusaidia katika eneo hilo.

“Jambo hili ni zuri na kubwa sana, ni miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania iliyasemea, eneo hilo ndiko watu wengi walikopata ajira hasa akina mama na vijana tunaishukuru na kuipongeza China  kwa kutoa kipaumbeele katika eneo hilo”, alisema Mhe. Waziri.

Amesema kikao hicho pia kimeangalia maeneo ya kujengea uwezo wananchi wa Afrika katika eneo la ufadhili wa masomo ambalo kwa wakati huu limekwama kutokana na mlipuko wa virusi vya Covid 19 lakini wameahidi kuendelea nalo pale hali itakapotengemaa.

Ameongeza kuwa kikao pia kimeangalia suala la kuendeleza kilimo ili kuwa na kilimo cha kisasa na kuendeleza miundombinu ya kidijitali hasa nyakati hizi ambazo ni lazima kujiunganisha kidigitali ili kujikwamua  kiuchumi.

Amesema China imesisitiza na kuweka mkazo katika eneo la kundeleza kilimo ili kuziwezesha nchi za Afrika kujikwamua na umasikini na wameahidi kutoa fedha na kuleta wataalamu kwa ajili ya kuendeleza kilimo.

Mkutano huo wa siku mbili ulijumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China uliangalia jinsi China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu cha 2018-2021 kwenye  maeneo ya miradi ya kimkakati na ukuzaji wa wigo  wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.


 

 

 

TANZANIA YASISITIZA KUUNGA MKONO, KUENDELEZA UHUSIANO NA CHINA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa kwenye Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza mshiriki wakati wa Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021.


Washiriki wa Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021 wakipitia nyaraka mbalimbali za mkutano huo.

Washiriki wa Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021 wakifuatilia mkutano huo.


Tanzania imesisitiza kuunga mkono, kuendeleza ushirikiano, uhusiano na mshikamano ambao China umekuwa ukiuonesha  kwa nchi za Afrika.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula alipozungumza katika Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30, 2021.

Amesema kwa kuangalia yaliyotokea katika kipindi hiki kigumu ambacho dunia inakipitia, China imekuwa ikishirikiana na Afrika kwa kutoa misaada mikubwa  ya fedha, wataalamu na vifaa kwa nchi za Afrika katika nyanja mbalimbali na kuwa na ushirikiano ambao umenufaisha pande zote.

Amesema kwa upande wa Tanzania China imekuwa ikisaidia katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati  ambayo imekuwa ikifanyika kwa kushirikiana na makampuni yao makubwa yanayowekeza chini .

Aidha Tanzania imeiomba China kuweka msisitizo mkubwa  katika sekta ya afya hasa katika kupambana na janga la ugonjwa wa korona unaosababishwa na virusi vya COVID 19 kwa kujengewa viwanda na kupatiwa uwezo wa kuzalisha chanjo hizo na dawa nyingine wenyewe. 

Waziri Mulamula amepongeza kauli ya Rais wa China Mhe. Xi Jinping ya kuwa nchi hiyo itatoa dozi billioni moja zaidi kwa nchi za Afrika ili kuziwezesha nchi  za Afrika kufikia lengo la kutoa chanjo kwa angalau asilimia 60 kwa watu wake ifikapo mwaka  2022.

“Tanzania imepokea taarifa hizo kwa mikono miwili na tunaishukuru serikali ya China kwani iliipatia Tanzania chanjo laki tano na tunategemea kupata  chanjo nyingine, na sasa kwa tangazo hilo China wametuhakikishia kwamba tutapata chanjo kwa kiasi kile tunachohitaji”, amesema Balozi Mulamula.

Mkutano huo ulijumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China na kuangalia ambavyo China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu cha 2018-2021 kwenye  maeneo ya ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda barani Afrika, ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji, habari na mawasiliano, kukuza wigo  wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.

Maeneo mengine ni kampeni ya mapinduzi ya kijani, mpango maalum wa mafunzo ya ufundi, kuboreha sekta ya Afya, ulinzi na usalama na ushirikiano katika masuala ya habari, utamaduni sanaa na michezo.

Tuesday, November 30, 2021

Balozi Togolani Mavura awasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Naibu Waziri na Mkuu wa Itifaki wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Korea, Mhe. Togolani Edriss Mavura, leo tarehe 30 Novemba 2021 amewasilisha Nakala za Hati za  Utambulisho kwa Naibu Waziri na Mkuu wa Itifaki Balozi Jeongyun RYU wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea jijini Seoul.


Akiongea baada ya kupokea Nakala hizo, Balozi Ryu amempongeza Balozi Mavura kwa imani kubwa aliyopewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kumuwakilisha nchini humo. 

Pia ametumia nafasi hiyo kumhakikishia utayari wa Wizara ya Mambo ya Nje na Serikali ya Korea kwa ujumla kumpatia ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuimarisha ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Korea.

Naye Balozi Mavura alimshukuru Balozi Ryu kwa mapokezi mazuri aliyopata kutoka Serikali ya Korea tangia alipowasili nchini Korea tarehe Novemba 10, 2021, na kutenga muda wake kupokea Nakala za Utambulisho.

 Aidha, Balozi Mavura alielezea kufurahishwa kwa hali ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Korea unaoelekea kutimiza miaka 30 mwezi Aprili 2022. 

Vilevile, Alimfahamisha mwenyeji wake juu ya azma yake ya kuuona ushirikiano huu unazidi kuimarika siku za usoni kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Korea.


Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Korea, Mhe. Togolani Edriss Mavura, leo tarehe 30 Novemba 2021 amewasilisha Nakala za Hati za  Utambulisho kwa Naibu Waziri na Mkuu wa Itifaki, Balozi Jeongyun RYU wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea jijini Seoul.

Makabidhiano yakiendelea, wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Utawala na Fedha wa Ubalozi wa Tanzania katika jamhuri ya Korea, Bw. Deogratius Mwanyasi akishuhudia makabidhiano hayo.
 

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CHINA

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi walipokutana kwa mazungumzo jijini Dakar nchini Senegal wanakohudhuria Mkutano wa Nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula wakisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi walipokutana kwa mazungumzo jijini Dakar nchini Senegal wakati wa Mkutano wa Nane wa wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi na ujumbe wake (kulia) walipokutana kwa mazungumzo jijini Dakar nchini Senegal.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi akizungumza wakati wa mazungumzo  na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula hayupo pchani jijini Dakar nchini Senegal.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi na ujumbe wake hawako pichani  jijini Dakar nchini Senegal.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi baada ya kumaliza mazungumzo yao walipokutana jijini Dakar nchini Senegal.

 

 Na mwandishi wetu,  Dakar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi jijini Dakar nchini Senegal.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wameelezea kuridhishwa kwao na ushirikiano na uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na China na kuahidi kuendeleza uhusiano huo kwa faida ya pande zote mbili.

Waziri Mulamula amemuhakikishia Waziri Yi utayari wa Serikali  kuendelea kushirikiana na China katika kuhakikisha Tanzania inafikia maendeleo ya kweli kwa ufanisi mkubwa.

Amemshukuru Waziri huyo kutokana na ahadi iliyotolewa awali na Rais Xi Jinping wa China wakati wa ufunguzi wa mkutano wa FOCAC ya kutoa dozi bilioni moja zaidi za chanjo ya virusi vya Covid 19 kwa bara la Afrika kwani kitendo hicho kitazisaidia nchi za Afrika kutoa chanjo ya ugonjwa huo kwa watu wengi zaidi.

Pia ameishukuru China kwa kuwa soko la bidhaa za Tanzania na amemuhakikishia Waziri huyo kuwa Tanzania iko tayari kutumia fursa ya soko la China la kuuza mazao yake ya mbogamboga na matunda ili kuongeza ujazo wa biashara na hivyo kukuza uchumi.

Pia ameelezea ambavyo Tanzania inafarijika na utayari wa China katika kuisaidia kwenye miradi mbalimbali kama ile ya  ya ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme utokanao na maji kama ya Ruhuji, mradi wa uendelezaji wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji , upanuzi wa Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete  na ujenzi wa barabara kuu katika Visiwa vya  Zanzibar miradi ambayo amesema itasaidia kuinua na kukuza uchumi wa nchi.

Naye Waziri Yi kwa upande wake ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono China na kuahidi kuendelea na harakati za kusaidia nchi zinazoendelea na kuongeza kuwa China itaendelea kuisadia Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati na kuielezea Reli ya TAZARA kama moja ya kielelezo cha ushirikiano huo.

Amesema China itaendelea kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kujikwamua kiuchumi na itatoa mamilioni ya fedha ili  kukamilisha miradi ya ujenzi, uanzishwaji wa kituo cha mfano kwa ajili ya kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo na kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo wadogo nchini.

Mawaziri hao wako Senegal kuhudhuria  Mkutano wa Nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika nchini Senegal ulioanza tarehe 29  hadi 30 Novemba  2021.