Friday, March 18, 2022
WFP YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUBORESHA SEKTA YA KILIMO NCHINI
Na Mwandishi wetu, Dar
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeahidi kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha kilimo nchini na kukifanya kuwa cha kisasa zaidi.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Haile amesema WFP inajivunia uhusiano mzuri na Tanzania na itaendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano huo kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Leo tumejadili na kuona ni namna gani tunaweza kuwaunga mkono wakulima wa Tanzania ili waweze kupata faida zaidi kupitia kilimo ambapo faida hiyo itawasaidia kuyaboresha zaidi maisha yao,” amesema Dkt. Haile
“………… kwa kuwa kilimo ndiyo sekta pekee inayotoa fursa ya ajira kwa wingi duniani, tuna mkakati wa kuwawezesha vijana kujikita zaidi kwenye kilimo ili kupunguza tatizo la ajira,” amesema Dkt. Haile na kuongeza kuwa WFP itahakikisha Tanzania inakuwa kituo cha uzalishaji katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa kuwa ina rasilimali za kutosha kuwekeza katika sekta ya Kilimo.
Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amemuahidi Mkurugenzi huyo wa WFP kuwa Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inaboreshwa zaidi.
“Nimewahakikishia WFP kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano katika kuhakikisha maboresho katika sekta ya kilimo yanafanyika na kuboresha maisha ya wakulima na kuwafanya vijana kujikita zaidi kwenye sekta hiyo muhimu,” amesema Balozi Mulamula.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na WFP katika kuboresha zaidi sekta ya kilimo.
Thursday, March 17, 2022
KAMATI YA KITAIFA YA KUZUIA MAUAJI YA KIMBARI YAJADILI MFUMO WA KUZUIA MIGOGORO NCHINI
Mjwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari bibi Felistas Mushi akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Kamati hiyo kinachofanyika jijini Dar es Salaam |
Wednesday, March 16, 2022
WAZIRI MULAMULA APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO ZA BALOZI WA MALAWI
Na Waandishi wetu, Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amepokea nakala ya Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Malawi nchini Mhe. Andrew Kumwenda leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Baada ya kupokea nakala ya hati hizo Balozi Mulamula amemuahidi Balozi mteule ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibalozi wakati wote atakaokuwepo nchini.
“Leo nimepokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Malawi na tumefarijika kwa Mhe. Rais Chakwera kumteua Balozi huyu mara baada ya Balozi wa awali kumaliza muda wake wa uwakilishi, hii ni ishara ya uhusiano wa karibu, undugu na urafiki uliopo baina ya Tanzania na Malawi,” amesema Balozi Mulamula
Kwa upande wake Balozi Mteule wa Malawi Mhe. Andrew Kumwenda amesema kuwa Malawi na Tanzania siku zote zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na jukumu langu hapa kama Balozi ni kuhakikisha uhusiano huu unazidi kuku ana kuimarika.
“Tanzania inatekeleza Diplomasia ya Uchumi na vivyo hivyo Malawi………kwa hiyo sisi wote tuna lengo moja, na nitahakikisha Tanzania na Malawi zinashirikiana kufanya biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande mbili,” Amesema Balozi Kumwenda.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi Mteule wa Malawi nchini Mhe. Andrew Kumwenda |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Balozi Mteule wa Malawi nchini Mhe. Andrew Kumwenda katika picha ya pamoja na maafisa walioambatana nao |
Tuesday, March 15, 2022
KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA KUSAIDIA KUWAREJESHA WANAFUNZI WALIOKUWA NCHINI UKRAINE
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea Chuo Cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam |
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Stella Ikupa akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea Chuo Cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam |
BALOZI MULAMULA ATAJA MAFANIKIO WIZARA YA MAMBO YA NJE
Na Waandishi Wetu, Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametaja maeneo 11 ambayo Wizara inajivunia katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita madarakani chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akiongea na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Balozi Mulamula amesema Wizara ya Mambo ya Nje katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita Wizara imetekeleza majukumu yake kwa mafanikio.
Balozi Mulamula ameyataja mafanikio hayo kuwa ni kusainiwa kwa makubaliano na mikataba ya ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa kufuatia ziara mbalimbali zilizofanywa na viongozi wa Kitaifa nje ya nchi na Wakuu wa nchi na Mashirika ya Kimataifa kutembelea nchini.
“Ziara hizo pia zimewezesha upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu ambapo fedha kiasi cha Shilingi Trilioni 1.77 na Euro milioni 425 kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya zilipatikana, wakati huohuo Tanzania ilichaguliwa na nchi 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwa Makamu wa Rais wa Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo katika uchaguzi huo, Tanzania ilipita bila kupingwa, mara ya mwisho Tanzania kupata nafasi hiyo ilikuwa mwaka 1991,” amesema Balozi Mulamula.
Mafanikio mengine ni kufunguliwa kwa Balozi mpya mbili katika nchi za Austria na Indonesia na Konseli Kuu tatu katika miji ya Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Shanghai na Guangzhou nchini China, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa majengo katika balozi za Tanzania.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa wawekezaji kutoka nje ambapo wengi wameonesha dhamira ya kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.
Balozi Mulamula amesema Lugha ya Kiswahili kwa mara ya kwanza kiswahili kimetambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kuwekewa siku maalum ya kuadhimishwa duniani ambayo ni tarehe 7 Julai kila mwaka. Niwakumbushe kuwa, Kiswahili ni lugha ya kwanza ya kiafrika kupewa hadhi hiyo na UNESCO," Amesisitiza Balozi Mulamula.
Mafaniko mengine yaliyoainishwa na Mhe. Waziri wakati wa mkutano huo ni pamoja na kuondolewa kwa vikwazo 56 kati ya 64 vya kibiashara kufuatia maagizo ya Marais wa Kenya na Tanzania. Aidha, vikwazo vingine vinane viliondolewa na Mawaziri wa Biashara wa nchi hizi mbili walipokutana Zanzibar tarehe 13 Machi 2022.
Kadhalika, Waziri Mulamula amesema Wizara yake itaendelea kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje hususan kwenye masuala ya kukuza uchumi wa nchi kwa kuhamasisha uwekezaji kutoka nje, biashara na utalii.
Balozi Mulamula amehitimisha na Suala la Watanzania waliokuwa wamekwama nchini Ukraine ambapo amesema serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha raia wake wanakuwa salama pamoja na changamoto hizo.
“Napenda kuwafahamisha kuwa, zoezi la kuwaondoa Watanzania wote waliokuwepo nchini humo wakiwemo Wanafunzi limekamilika ambapo hadi sasa takribani Watanzania 300 wamefanikiwa kuondoka na kuelekea nchi jirani na baadhi yao wamerejea hapa nchini”, amesema Balozi Mulamula.
Monday, March 14, 2022
BALOZI WA MAREKANI APONGEZA UENDESHAJI MICHAKATO YA KISIASA NCHINI
Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Donald Wright akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimueleza jambo Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Donald Wright |
Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Donald Wright kikiendelea |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Norway nchini Mhe. Elisabeth Jacobsen katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
BALOZI SOKOINE AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA KIKAO CHA MAKATIBU WAKUU WA SADC MJINI LILONGWE, MALAWI
Kikao cha Makatibu Wakuu kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kikiendelea katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Bingu wa Mutharika Lilongwe, Malawi |
Friday, March 11, 2022
WAZIRI MULAMULA AKUTANA NA WATANZANIA WANAOISHI SAUDI ARABIA
Bi Amina akiwasilisha nakala ya risala aliyoisoma kwa Mhe. Waziri Mulamula alipokutana na Watanzania wanaoishi nchini Saudi Arabia nyumbani kwa Balozi wa Tanzania jijini Riyadh |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi nchini Saudi Arabia na kuwataka kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania nchini humo.
Balozi Mulamula amekutana na Watanzania hao jijini Riyadh katika kikao kilichofanyika nyumbani kwa Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Mwadini.
Akizungumza na Watanzania hao Balozi Mulamula amesisitiza juu ya umuhimu wa Watanzania hao kuishi kwa kufuata sheria na kanuni za nchi hiyo kwani kufanya hivyo kutaendelea kulinda taswira nzuri ya nchi yao.
Balozi Mulamula pia amewahahakishia watanzania hao juu ya nia ya Serikali ya kufanyia kazi mawazo na maoni yao ili kuwa kuwa na amani.
‘’Niwahakikishieni ndugu zetu mlioko huku, serikali yenu ni sikivu inathamini na kujali maoni mnayoyatoa na inayafanyia kazi, na muda si mrefu mtaona tulipofikia,” alisema Balozi Mulamula.
Awali katika risala yao kwa mhe. Waziri Watanzania hao walielezea changamoto na mafanikio yaliyopatikana kupitia umoja wao na kuiomba serikali kufanyia kazi changamoto wanazozipata hasa wakati wa kuondoka nyumbani.
Waziri Mulamula yuko nchini Saudi Arabia kwa ziara ya kikazi kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwana Mfalme, Mtukufu Faisal bin Farhan Al Saud, alioutoa mwezi Machi 2021 alipotembelea Tanzania.