Friday, October 16, 2020

BALOZI IBUGE AKUTANA, KUMUAGA BALOZI WA NIGERIA

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amekutana na kumuaga Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada ambaye amemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini.  

Mazungumzo hayo yamefanyika leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Ibuge amemtakia maisha mema na kumsihi kuwa balozi mwema kwa Tanzania nchini Nigeria na kwingineko duniani.

Balozi Ibuge amesema kuwa Nigeria imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Tanzania hasa katika kuunga mkono jitihada za kuimarisha sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta za usafirishaji, utalii, biashara na uwekezaji na usafirishaji

“Leo nimekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Gada ambae amemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini na anarudi Nigeria, na kwa hakika mazungumzo marefu na yamelenga urafiki baina ya nchi zetu mbili na watu wetu pamoja na ushirikiano uliopo wa kibiashara, kibenki lakini pia tumezungumzia namna ambavyo Nigeria inapiga hatua kama Tanzania inavyopiga hatua, na mfano mzuri ni kuwa Nigeria ilipojenga mji wake mkuu mpya (Abuja) walikuja Tanzania kuja kujifunza na kupata ramani ya Dodoma ambayo wamemaliza kuijenga na sisi sasa tunaendelea kuijenga Dodoma tangu tulipotangaza rasmi kuhamia Dodoma mwaka 1973" Amesema Balozi, Brigedia Jenerali Ibuge  

Balozi Brigedia Jenerali Ibuge amemhakikishia Balozi Gada, kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Nigeria utaendelea kuimarika ikiwa ni ishara ya kuwaenzi waasisi wa mataifa ya Tanzania Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Rais wa kwanza wa Nigeria Nnamdi Azikiwe ambapo viongozi hawa walikuwa ni sehemu ya juhudi za kukomboa bara la Afrika na hata kusimi mwa Afrika. 

Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesisitiza kuwa Tanzania na Nigeria zitaendelea kushirikiana katika sekta ya uwekezaji na biashara kwa maslahi mapana ya mataifa yote mawili ambapo pia ametoa wito kwa wafanyabiashara kutoka nchini Nigeria kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za benki na utalii. 

Kwa upande wake, Balozi Sherlock ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano iliyompatia wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake nchini na kuahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa Nigeria na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri na imara tangu miaka ya 1962.

”Nimekuja kumuaga Katibu Mkuu kama ishara ya ushirikiano wetu kati ya Nigeria na Tanzania kwa kweli nashukuru sana kwa ushirikiano nilioupata wakati wa utumishi wangu hapa nchini, nikiwa hapa nimeona uchumi wa Tanzania ukikua kila wakati jambo ambalo ni zuri hapa kwetu Afrika, pia namshukuru Katibu Mkuu, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kwa kuuendeleza ushirikiano wetu kwa kweli naiona Tanzania kama nyumbani kwangu pia,"Amesema Balozi Gada.  

Nigeria itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuhakikisha kuwa inasonga mbele kimaendeleo,” amesema Balozi Gada.

Tanzania na Nigeria zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia tangu Serikali ya Nigeria ilipofungua ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 1962.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkaribisha Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada alipokenda kumuaga leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati alipokwenda kumuaga leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimuelezea jambo Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada wakati alipokwenda kumuaga   


Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada  

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa kutoka Wizarani na Ubalozi wa Nigeria hapa nchini 








No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.