Sunday, April 3, 2022

MKUTANO WA DHARURA WA KAMATI YA MAWAZIRI WA SADC KUFANYIKA PRETORIA, AFRIKA KUSINI

Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Extra-Ordinary Ministerial Committee of the Organ) ambao utahusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) utafanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022.

Mkutano huo ambao umetanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu (Senior Officials meeting), unalenga pamoja na mambo mengine Kupokea na Kujadili Ripoti ya Maendeleo ya Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) pamoja na Mapendekezo mbalimbali kutoka kwa Makatibu Wakuu.

Itakumbukwa kuwa, wakati wa Mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulichofanyika jijini Maputo, Msumbiji mwezi Juni 2021, uliridhia kupelekwa kwa Misheni ya SAMIM (SADC Mission in Mozambique) nchini Msumbiji kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo kupamabana na ugaidi na vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto vilivyokuwa vinaendelea kwenye baadhi ya Wilaya zilizopo kwenye Jimbo la Cabo Delgado.

Misheni hiyo ambayo ilianza kazi rasmi mwezi Julai 2021, inajumuisha Nchi Wanachama kumi (10) za SADC ambazo ni Tanzania, Angola, Malawi, Lesotho, Namibia, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Botswana, Zimbabwe na Zambia.

Lengo kuu la misheni hiyo ni kukomesha matishio ya ugaidi,  kuimarisha hali ya ulinzi na  usalama, kurejesha utawala wa sheria kwenye maeneo yaliyoathirika kwenye Jimbo la Cabo Delgado na kuisadia Msumbiji kwa kushirikiana na Mashirika yanayotoa misaada ya kibinadamu ili kuyawezesha kutoa misaada kwenye maeneo yaliyoathirika na vitendo vya kigaidi ikiwemo kuwasaidia watu walioyakimbia makazi yao.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo utaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe. Viongozi wengine kutoka Tanzania watakaoshiriki Mkutano huo ni pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo akitoa taarifa fupi kwa Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Ministerial Committee of the Organ-MCO) ambao utahusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) unaofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022.

Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakati wa kikao kati yao na kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa SADC unaofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.

Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania, Dkt. Mnyepe (wa tatu kulia walioketi) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Gaudence Milanzi (wa pili kulia walioketi) na wajumbe wengine wakimsikiliza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo wakati akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao utahusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) unaofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022. 

Wajumbe wengine wa Tanzania wanaoshiriki Mkutano.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.