Thursday, February 20, 2014

Naibu Katibu Mkuu ashiriki maadhimisho ya mwaka mpya wa China

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha akizungumza kwenye halfa ya kuadhimisha mwaka mpya wa China, iliyoandaliwa na Benki ya Standard Chartered na kufanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, Dar es Salaam. Wakati wa hafla hiyo Balozi Gamaha aliupongeza Ubalozi wa China katika kusaidia na kuchangia maendeleo ya Tanzania. Pia Balozi Gamaha aliipongeza Benki ya Standard Chartered kwa kushirikiana na Ubalozi wa China nchini katika kurahisisha  biashara kati ya Tanzania na China. 
Balozi wa  Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. Lv Youqing akitoa neno la shukrani kwa Benki ya Standard Chartered kwa kuandaa hafla hiyo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered nchini, Bi. Lizzy Lloyd akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Wageni waalikwa walioshiriki hafla hiyo.
Balozi Gamaha (kulia) akimsikiliza Bw. Nathaniel Kaaya,  Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati wa hafla hiyo. Wengine wanaosikiliza  kutoka kushoto ni Bw. Iman Njalikai na Bw. Emmanuel Luangisa, Maafisa Mambo ya Nje.
Balozi Gamaha akizungumza na Waandishi wa Habari.




Picha na Reginald Kisaka

Wednesday, February 19, 2014

Makatibu Wakuu Zanzibar wapigwa msasa kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Balozi Celestine Mushy (wa kwanza kushoto kwa waliokaa), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa katika picha ya Pamoja na Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Serikali ya Zanzibar baada ya kikao cha IMTC. Balozi Mushy alitumia kikao hicho kuwasilisha mada kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo yatachukuwa nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia


Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mushy (kulia) na Balozi Silima Haji, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar mara baada ya kukamilika kikao cha IMTC.


Monday, February 10, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kukanusha taarifa za uvumi zinaosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na vyombo vya habari kuwa kuna Watanzania wapatao 160 wamenyongwa nchini China kwa kosa la kusafirisha madawa ya kulevya.

Wizara inapenda kuujulisha Umma kuwa hakuna Mtanzania yeyote aliyenyongwa kama inavyodaiwa kwenye mitandao na vyombo vya habari.

Aidha, taarifa hiyo ya uvumi imedai kuwa ndugu wa mmoja wa Watanzania hao ambaye kwa jina anajulikana kama Bw. Rajab Mohamed Ismail Mapusa wamekaa matanga kuomboleza kifo chake.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Serikali ya China, Bw. Mapusa yupo hai gerezani akitumikia kifungo cha maisha kwa kosa la kuingiza madawa ya kulevya nchini humo, na hivi karibuni alishiriki kuandaa maonyesho ya utamaduni wa Kiafrika wakati wa kuadhimisha sherehe za Mwaka Mpya wa China.

Wizara inapenda kuwakumbusha Wanahabari kuandika taarifa ambazo ni sahihi zisizopotosha Umma kwa kuzingatia weledi, maadili na ukweli kutoka mamlaka zote husika.

 

Imetolewa na: Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam

10 Februari, 2014

Friday, February 7, 2014

Wizara kutengeneza Database ya Diaspora kwa kushirikiana na IOM

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Rosemary Jairo akizungumza wakati wa kikao kuhusu uundwaji wa Database na Tovuti kuhusu masuala ya Diaspora. Kikao hicho kiliwashirikisha Wajumbe kutoka Ofisi ya Rais Zanzibar, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uhamiaji na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji hapa nchini (IOM).
Wajumbe kutoka IOM, Ofisi ya Rais Zanzibar na Uhamiaji wakimsikiliza Bibi Jairo (hayupo pichani) wakati wa kikao hicho
Mwakilishi kutoka IOM, Bi. Mia Immelback akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
Bibi Jairo (wa pili kulia) akiwa na Wajumbe wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Mwakilishi wa IOM (hayupo pichani). Kutoka kushoto ni Bw. Mkumbwa Ally, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasialiano katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Kalumuna, Mkuu wa Kitengo cha ICT, Wizara ya Mambo ya Nje na Bi. Susan kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Bw. Kalumuna akichangia jambo wakati wa kikao hicho.

Picha na Reginald Kisaka.


Mkataba kuhusu Ujenzi wa Taasisi ya kuweka kumbukumbu za kazi za iliyokuwa Mahakama ya ICTR wasainiwa.

        Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha (kulia) pamoja na Katibu Mkuu Msaidizi wa masuala ya Sheria katika Umoja wa Mataifa, Bw. Stephen Mathias (kushoto) wakisaini Mkataba kuhusu  "Suplementary Agreement to the Agreement between the United Republic of Tanzania and the United Nations concerning the Headquarters of the International Residual Mechanism for Tribunals". Taasisi hii ya Kimataifa itajengwa Jijini Arusha eneo la Lakilaki kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ya kazi za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR).

     Balozi Gamaha akibadilishana Mkataba huo na Bw. Mathias mara baada ya kuusaini

Balozi Gmaha akizungumza mara baada ya kusaini mkataba. Kulia ni Mhe. Tuvako Manongi, Balozi wa Tanzania kwenye Uwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa, New York, Marekani

Bw. Mathias kutoka Umoja wa Mataifa naye akizungumza mara baada ya kusaini Mkataba

Wajumbe waliokuwepo wakati wa kusainiwa Mkataba huo


Picha na Reginald Kisaka

Thursday, February 6, 2014

Mhe. Rais Kikwete alipokutana na Waziri wa Maendeleo wa Canada

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Mhe. Christian Paradis mara baada ya Waziri huyo kuwasili Ikulu. Mhe. Paradis alitembelea Tanzania hivi karibuni kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya nchini hizi mbili.
Mhe. Rais Kikwete akisalimiana na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Alexandre Leveque.
Mhe. Rais Kikwete katika mazungumzo na Mhe. Paradis.
Mhe. Rais Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Paradis pamoja na Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) (wa kwanza kulia), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb.), (wa pili kulia), Waziri wa Fedha, Balozi wa Canada hapa nchini, Mhe. Leveque (wa kwanza kushoto) na Wajumbe wengine.

Picha na Reginald Kisaka.

Mhe. Membe akutana kwa mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiaano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akisalimiana na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Mhe. Christian Paradis walipokutana kwa mazungumzo rasmi katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia ni Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb.). Mhe. Paradis alifanya ziara hapa nchi hivi karibuni kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Tanazania na Canada.
Mhe. Membe katika mazungumzo na Mhe. Paradis.


Mhe. Membe na Mhe. Mkuya na wajumbe wengine wakati wa mazungumzo na Mhe. Paradis (hayupo pichani) . Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dora Msechu.

Mhe. Paradis na Ujumbe wake akiwemo Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Alexandre Leveque (wa nne kutoka kushoto) wakimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani)

Mhe. Mkuya akiagana na Mhe. Paradis mara baada ya mazungumzo huku Mhe. Membe akishuhudia.

Picha na Reginald Kisaka

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada atembelea Tanzania


 Waziri wa  Maendeleo  ya Kimataifa wa Canada, Mhe. Christian Paradis' (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya  Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dora Msechu mara baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya siku mbili kuanzia tarehe  3-4 Februari, 2014. Akiwa nchini Mhe. Paradis atashiriki Kongamano kuhusu Afya ya Mama na Mtoto.
Mhe. Waziri   Paradis' (kulia) akisalimiana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Benno Ndulu mara baada ya kuwasili nchini.
Balozi Msechu akibadilishana mawazo na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Alexandre Leveque
Balozi Msechu skizungumza na Mhe. Paradis mara baada ya kumokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Picha na Reginald Kisaka



Friday, January 31, 2014

Mhe. Membe akutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mhe. Ahmed Davutoglu walipokutana Mjini Addis Ababa kwa mazungumzo kuhusu kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki. Mhe. Membe yupo Addis Ababa akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika kuanzia tarehe 30 hadi 31 Januari, 2014.
Mhe. Membe (katikati) akiwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Tuvako Manongi (kushoto) pamoja na Bw. Togolani Mavura, Msaidizi wa Waziri wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki (hayupo pichani)
Mhe. Membe (kushoto) akimsikiliza Mhe. Davutoglu (wa pili kulia) wakati wa mazungumzo yao.
Mhe. Membe akifurahia jambo na Mhe. Davotoglu huku akiondoka baada ya mazungumzo yao.

Mhe. Membe ahutubia Mkutano kuhusu Amani DRC na Nchi za Maziwa Makuu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwa katika moja ya Mikutano ya Umoja wa Afrika inayoendelea mjini Addis Ababa, Ethiopia. Mhe. Membe alihutubia Mkutano wa Tatu wa Ngazi ya Juu kuhusu Utaratibu wa Usimamizi wa masuala ya Amani, Usalama na Ushirikiano  katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 31 Januari, 2014 pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea mjini hapa.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Tanzania wakiwa kwenye Mkutano kuhusu Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) mjini Addis Ababa. Mwenye tai nyekundu ni Bw. Robert Kahendaguza, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda na Balozi David Kapya.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliason akizungumza wakati wa Mkutano kuhusu DRC na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika Addis Ababa.
Mjumbe wa Sudan akisaini Mkataba wa Kujiunga na Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano ulio chini ya ICGLR
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bibi Mary Robinson naye pia alikuwepo katika mkutano huo.
Wajumbe wengine kutoka nchi wanachama wa ICGLR wakifuatilia mkutano.
===============================




Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ametoa rai kwa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) kuweka nia mpya ili kutimiza lengo la kupatikana kwa amani ya kudumu katika Nchi za Ukanda huo. 

Mhe. Membe aliyasema hayo wakati akihutubia Mkutano wa Tatu wa Ngazi ya Juu kuhusu Utaratibu wa Usimamizi wa masuala ya Amani, Usalama na Ushirikiano  katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea mjini hapa.

Waziri Membe alisema kuwa kumekuwa na hatua nzuri zilizofikiwa katika kutafuta amani ya kudumu DRC na katika Kanda kwa ujumla. Hatua hizo ni pamoja na kusambaratishwa kwa kikundi cha Waasi cha M23 huko Mashariki mwa DRC. Hata hivyo alisema bado kunahitajika jitihada na nia madhubuti ili kuhakikisha migogoro isiyoisha inamalizwa kabisa. 

“Tunayashukuru Majeshi ya Ulinzi ya DRC kwa msaada wa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa (MUNOSCO) na kile cha FIB ambapo tumeshuhudia kusambaratishwa kwa Kikundi cha M23, tunapongeza pia jitihada za Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni ambaye pia ni msuluhishi wa mgogoro huo kufuatia kusainiwa kwa Azimio la Amani kati ya Serikali ya DRC na M23 hapo tarehe 12 Desemba, 2013”, alisema Mhe. Membe.

Mhe. Membe aliongeza kuwa umefika wakati sasa kwa watu na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu  kusema inatosha kwa migogoro isiyoisha ili kuwawezesha kuwekeza nguvu na vipaji vyao katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, kwa namna ya pekee, Waziri Membe alimpongeza Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, Mhe. Bibi Mary Robinson na Kamati yake ya Ufundi (TSC) kwa kazi nzuri waliyoifanya mwaka 2013. Kamati hiyo ya Ufundi imefanikiwa kutoa Mpango Kazi kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Kanda.

 “Nimeridhishwa na kazi inayofanywa na Kamati hiyo ya Ufundi  kwa kutoa Mpango Kazi ambao unajitosheleza kwa ajili ya kuutekeleza  Mpango wa Amani. Hivyo, tumekutana hapa kuridhia mpango huo ili kila mmoja wetu aweke nia mpya ya kutekeleza yale yote tuliyowahi kukubaliana chini ya Mpango wa Amani” alisisitiza Waziri Membe.

Aidha, wakati wa Mkutano huo nchi za Kenya na Sudan zilisaini rasmi Mkataba wa kujiunga na Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Kanda ya Maziwa Makuu  ( Peace, Security and Cooperation Framework).

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson.

-Mwisho-


Tanzania na Colombia zajidili namna ya kuboresha ushirikiano wa kiuchumi.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Balozi Rajabu Gamaha (kulia) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Asia, Afrika na Oceania kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Colombia, Bibi Sandra Salamanca. katika kikao hicho, viongozi hao walijadili namna Tanzania na Colombia zitakavyoweza kushirikiana ili kutumia fursa zinazopatikana katika nchi hizo kwa madhumuni ya kuinua kipato cha wananchi wao.


Bibi Salamanca (kulia) akisisitiza jambo huku Balozi wa Colombia nchini Tanzania mwenye makao yake Nairobi, Kenya Mhe. Maria Lugenia Correa akisikiliza kwa makini.

Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dora Msechu akifafanua jambo katika kikao hicho huku Bw. Graison Ishengoma, Afisa Mambo ya Nje akinukuu masuala muhimu ya mazungumzo. 



Picha ya pamoja, wa tatu kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu ambapo kulia kwake ni Mratibu wa Masuala ya Afrika, Mashariki ya Kati na Asia ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Colombia, Balozi Betty Escorcia.



Picha na Reginald Philip Kisaka.

Ubalozi wa China watoa msaada kwa waathirika wa mafuriko


Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youping akikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Leteni Jenerali Sylivester Rioba. Msaada huo ambao unathamani ya Shilingi milioni 32 umetolewa kwa ajili ya watu walioathirika na mafuriko mkoani Morogoro.

Balozi wa China (katikati) akishikana mikono na Luteni Generali Rioba na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Athony Mtaka wakati wa hafla ya kukabidhi msaada iliyofanyika katika Ubalozi wa China. nyuma yao lori aina ya fuso likiwa limejazwa baadhi ya bidhaa za msaada huo.


Balozi wa China akikabidhi stakabadhi za vifaa vya msaada kwa Leteni Jenerali Rioba huku Mkuu wa Wilaya ya Mvomero akishuhudia.

Wanahabari nao hawakuwa mbali kushuhudia hafla ya makabidhiano.

Balozi wa China, Mhe. Lu Youping akitoa hotuba fupi.

Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu akitoa hotuba ya kushukuru msaada uliotolewa na Balozi wa China.


Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mberwa Kairuki akisalimiana na Luteni Jenerali Rioba mara baada ya hafla ya kukabidhi msaada kukamilika.



Picha na Reginald Philip Kisaka