Friday, January 31, 2014

Mhe. Membe ahutubia Mkutano kuhusu Amani DRC na Nchi za Maziwa Makuu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwa katika moja ya Mikutano ya Umoja wa Afrika inayoendelea mjini Addis Ababa, Ethiopia. Mhe. Membe alihutubia Mkutano wa Tatu wa Ngazi ya Juu kuhusu Utaratibu wa Usimamizi wa masuala ya Amani, Usalama na Ushirikiano  katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 31 Januari, 2014 pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea mjini hapa.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Tanzania wakiwa kwenye Mkutano kuhusu Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) mjini Addis Ababa. Mwenye tai nyekundu ni Bw. Robert Kahendaguza, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda na Balozi David Kapya.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliason akizungumza wakati wa Mkutano kuhusu DRC na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika Addis Ababa.
Mjumbe wa Sudan akisaini Mkataba wa Kujiunga na Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano ulio chini ya ICGLR
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bibi Mary Robinson naye pia alikuwepo katika mkutano huo.
Wajumbe wengine kutoka nchi wanachama wa ICGLR wakifuatilia mkutano.
===============================




Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ametoa rai kwa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) kuweka nia mpya ili kutimiza lengo la kupatikana kwa amani ya kudumu katika Nchi za Ukanda huo. 

Mhe. Membe aliyasema hayo wakati akihutubia Mkutano wa Tatu wa Ngazi ya Juu kuhusu Utaratibu wa Usimamizi wa masuala ya Amani, Usalama na Ushirikiano  katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea mjini hapa.

Waziri Membe alisema kuwa kumekuwa na hatua nzuri zilizofikiwa katika kutafuta amani ya kudumu DRC na katika Kanda kwa ujumla. Hatua hizo ni pamoja na kusambaratishwa kwa kikundi cha Waasi cha M23 huko Mashariki mwa DRC. Hata hivyo alisema bado kunahitajika jitihada na nia madhubuti ili kuhakikisha migogoro isiyoisha inamalizwa kabisa. 

“Tunayashukuru Majeshi ya Ulinzi ya DRC kwa msaada wa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa (MUNOSCO) na kile cha FIB ambapo tumeshuhudia kusambaratishwa kwa Kikundi cha M23, tunapongeza pia jitihada za Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni ambaye pia ni msuluhishi wa mgogoro huo kufuatia kusainiwa kwa Azimio la Amani kati ya Serikali ya DRC na M23 hapo tarehe 12 Desemba, 2013”, alisema Mhe. Membe.

Mhe. Membe aliongeza kuwa umefika wakati sasa kwa watu na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu  kusema inatosha kwa migogoro isiyoisha ili kuwawezesha kuwekeza nguvu na vipaji vyao katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, kwa namna ya pekee, Waziri Membe alimpongeza Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, Mhe. Bibi Mary Robinson na Kamati yake ya Ufundi (TSC) kwa kazi nzuri waliyoifanya mwaka 2013. Kamati hiyo ya Ufundi imefanikiwa kutoa Mpango Kazi kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Kanda.

 “Nimeridhishwa na kazi inayofanywa na Kamati hiyo ya Ufundi  kwa kutoa Mpango Kazi ambao unajitosheleza kwa ajili ya kuutekeleza  Mpango wa Amani. Hivyo, tumekutana hapa kuridhia mpango huo ili kila mmoja wetu aweke nia mpya ya kutekeleza yale yote tuliyowahi kukubaliana chini ya Mpango wa Amani” alisisitiza Waziri Membe.

Aidha, wakati wa Mkutano huo nchi za Kenya na Sudan zilisaini rasmi Mkataba wa kujiunga na Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Kanda ya Maziwa Makuu  ( Peace, Security and Cooperation Framework).

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson.

-Mwisho-


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.