Friday, January 24, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Mhe. Membe kumwakilisha Rais Madagascar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye sherehe za kumwapisha Rais Mteule wa Madagascar, Mhe. Henry Rajaonarimampianina zitakazofanyika nchini humo tarehe 25 Januari, 2014.

Mhe. Membe ataondoka kwenda Madagascar tarehe 24 Januari, 2014. Mahakama Maalum ya Uchaguzi nchini Madagascar ilimtangaza Mhe. Rajaonarimampianina kuwa mshindi wa uchaguzi wa Urais tarehe 17 Januari, 2014.
Duru ya kwanza ya uchaguzi huo ilifanyika tarehe 31 Julai, 2013, ambapo hakupatikana mshindi. Katika duru ya pili iliyofanyika tarehe 20 Desemba, 2013, Mahakama Maalum ya Uchaguzi ilitangaza kuwa Mhe. Rajaonarimampianina alipata asilimia 53.49 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake Bw. Jean Louis Robinson akipata asilimia 46.51.

Kwa kushirikiana na wanachama wengine wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Tanzania,  ambayo ilikuwa mwenyekiti wa  Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa mwaka mmoja ulioishia Agosti, 2013, ilitoa mchango mkubwa kuhakikisha Madagascar inaendesha uchaguzi wake katika hali ya amani na utulivu na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, ili kumaliza mgogoro wa kisiasa ulioibuka mwaka 2008 baada ya Bw. Andry Rajoelina kuingia madarakani kwa kusaidiwa na Jeshi.

IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,

DAR ES SALAAM23 JANUARI, 2014, Januari 23, 2014

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.