Tuesday, January 28, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI






 Waziri Mkuu wa Finland kuzuru Tanzania

Waziri Mkuu wa Findland, Mhe. Jyrki Katainen atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania tarehe 29 na 30 Januari, 2014.Mhe.Katainen anategemewa kuwasili usiku wa tarehe 28 januari akitokea Addis Ababa, Ethiopia, na atafanyiwa mapokezi rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, kesho yake asubuhi.

Mhe. Katainen atafuatana na Waziri wake wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Pekka Haavisto, na wafanyabiashara 25 wa Finland.

Baada ya mapokezi rasmi, Mhe. Waziri Mkuu wa Finland atafanya mazungumzo na Mwenyeji wake, Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam, na baadaye atashiriki majadiliano kuhusu ushirikiano kati ya Ulaya na Afrika, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi  kwenye hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro.

Wakati wa ziara hiyo, Tanzania na Finland zitatiliana saini Mkataba wa Msaada wa Bajeti (General Budget Support) na Makubaliano ya Ushirikiano (Memorandum of Understanding) kwenye Nyanja za madini na misitu.

Mhe.Rais Kikwete atamwandalia mgeni wake chakula rasmi cha jioni, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 29 Januari, Mhe. Katainen anatarajiwa kuzuru Unguja  na kukutana na Rais  wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein. Kadhalika, atafanya mazungumzo na Wafanybiashara, wachumi na maafisa wa mashirika ya kimataifa jijini Dar es Salaam, pamoja na kutembelea bandari, kabla ya kuondoka nchini Januari 30 usiku.

 

IMETOLEWA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

 

DAR ES SALAAM, JANUARI 27, 2014

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.