Wednesday, January 22, 2014

Mhe. Waziri afungua Kongamano kuhusu masuala ya Diaspora

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano kuhusu masuala ya Uhamiaji na Watanzania waishio nje (Diaspora). Ufunguzi huo ulifanyika katika Hoteli ya JB Belmont Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Januari, 2014. Mwingine katika picha ni Bw. Jo Rispoli, Mtaalam wa masuala ya Uhamiaji katika Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria ufunguzi wa kongamano hilo wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe (hayupo pichani)


Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) hapa nchini Bw. Damien Thuriaux naye akizungumza huku Mhe. Membe na Bw.Rispoli wakimsikiliza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Rosemary Jairo akifuatilia kwa makini ufunguzi wa kongamano kuhusu masuala ya Diaspora.

Wajumbe wakifuatilia hotuba ya ufunguzi. Kutoka kulia ni Bw. Seif Kamtunda, Afisa Mambo ya Nje, Bi. Linda Helgesson, Mtaalam wa masuala ya Maendeleo ya Wahamiaji, Bi. Sudah Lulandala, Afisa Mipango na Bi. Tunsume Mwangolombe, Afisa Mambo ya Nje.

Picha ya pamoja.


Mhe. Membe akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ufunguzi wa kongamano hilo.



Na Reginald Philip Kisaka

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuridhia uraia wa nchi mbili ili Watanzania wanaoishi ughaibuni waweze kufaidika na fursa za kiuchumi na kijamii zinazotolewa kwa raia katika nchi wanazoishi.

Mhe. Waziri alitoa kauli hiyo katika ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na kufanyika katika Hoteli ya JB Belmont jijini Dar es Salaam tarehe 22 Januari, 2014. Kongamano hilo ambalo linawakutanisha wawakilishi kutoka Serikalini, wanazuoni, asasi za kiraia na watafiti mashuhuri lina lengo la kujadili njia mbalimbali ambazo wanadiaspora wanaweza kuzitumia kuchangia maendeleo ya nchi yao kwa mazingira ya Tanzania.

Mhe. Waziri aliwambia wajumbe wa kongamano hilo kuwa hoja ya uraia wa nchi mbili itawasilishwa na kutetewa katika Kikao Maalum cha Bunge la Katiba ambacho kinatarajiwa kufanyika katika siku za karibuni. “Endapo uraia wa nchi mbili utaridhiwa, Watanzania wanaoishi ughaibuni wataweza kupata kazi nzuri na kukopa benki  katika nchi wanazoishi, hivyo kipato chao kitaongezeka ambacho watakitumia pia kuwekeza nyumbani. Mhe. Waziri alisikika akisema.

Mhe. Membe alitolea mfano wa nchi zilizoweka mazingira mazuri ya wanadiaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi zao kuwa ni pamoja na Nigeria, Ghana na Kenya.


Awali, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji hapa nchini Bw. Damien Thuriaux alisema kuwa, kongamano hilo ambalo litafanyika kuanzia tarehe 22 hadi 29 Januari 2014 lina lenga kuhamasisha uratibu wa masuala ya Uhamiaji na Diapora kwa kuzishirikisha Wizara na Taasisi mbalimbali. Aidha katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania, Bw. Damien alisema kuwa Shirika lake litasaidia uundwaji wa Tovuti maalum kwa ajili ya watu waishio Nje (Diaspora) na masuala mengine yanayohusu uhamiaji.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.