Tuesday, January 28, 2014

TANZANIA YACHAGULIWA TENA MJUMBE BARAZA LA AMANI NA USALAMA LA AU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ambaye pia anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU), mjini Addis Ababa akisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Baraza hilo. Wengine katika picha ni Mhe. Naimi Aziz, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Mhe. Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa na Bw. Samwel Shelukindo, Afisa Mwandamizi kwenye Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa.
---------------------------------------------------------------------

Na Mwandishi wetu, Addis Ababa


Tanzania imechaguliwa kwa mara nyingine tena kuwa Mjumbe wa Baraza la  Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC)  kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo tarehe 28 Januari, 2014 wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika, Tanzania na Ethiopia zimechaguliwa kuiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki katika Baraza hilo muhimu linaloshughulikia masuala ya amani na usalama Barani Afrika.

Tanzania ilichaguliwa kwa mara ya kwanza katika Baraza hilo mwaka 2012. Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa aliongoza ujumbe wa Tanzania katika uchaguzi huo.

Matokeo ya uchaguzi huo yanaonyesha kuwa Tanzania na Ethiopia zilipata kura 40 kati ya kura 50 zilizopigwa ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya kura zinazotakiwa huku Eritrea ikipata kura 13.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lina Wajumbe 15 wanaochaguliwa na Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika. Wajumbe hao wanaowakilisha Kanda tano ambazo ni Afrika ya Kati, Afrika Mashariki, Afrika Kaskazini, Afrika ya Kusini na Afrika Magharibi.

Malengo ya Baraza hili ni pamoja na kulinda amani na usalama Barani Afrika; kuzuia migogoro; kulinda amani na kujenga amani katika maeneo yenye migogoro; kusimamia demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu.

-Mwisho-



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.