Wednesday, December 16, 2015

Wafanyabiashara wa Qatar wahimizwa kuwekeza Tanzania


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji, hivyo alitoa wito kwa wafanyabiashara kutoka Qatar kutumia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini. 


Balozi Mulamula aliyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Qatar iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regence, Kilimanjaro jijini Dar es Salaam jana.


“Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, madini, uchukuzi, elimu, afya, nishati, wanyamapori, mafuta na gesi, hivyo natoa wito kwa ndugu zetu wa Qatar watumie fursa ya uhusiano mzuri tulionao kuja kuwekeza nchini”, Balozi Mulamula alisema.  


Balozi Mulamula aliendelea kusema kuwa Serikali inaelekea katika uchumi wa gesi na ina matumani makubwa ya kufaidika na uzoefu wa mshirika wake Qatar ambayo ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa gesi duniani. 


Suala lingine ambalo Katibu Mkuu aliligusia ni umuhimu wa Tanzania na Qatar kuunganisha nguvu ili kutumia rasilimali fedha na ardhi zilizopo kuimarisha sekta ya kilimo kwa madhumuni ya kuodoa changamoto za usalama wa chakula kati ya nchi hizi mbili.


Kwa upande wake, Balozi wa Qatar nchini, Mhe. Abdulla Jassim Al Maadadi pamoja na mambo mengine, aliongelea suala la Qatar kuwa mwenyeji wa mashindano ya mpira wa miguu wa Kombe la Dunia kwa mwaka 2022. Alisema miradi mingi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2020.  Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara, mtandao wa reli, viwanja vya mpira, viwanja vya ndege na nyumba za makazi.


Alisema miradi hiyo ni mikubwa hivyo inahitaji wafanyakazi wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani na aliahidi kuwa watu watakaokwenda kufanya kazi nchini humo, haki zao zitalindwa.



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Liberata Mulamula akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha ya Siku ya Taifa la Qatar kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Augustine Mahiga. Katika maadhimisho hayo, Balozi Mulamula alisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar hususan katika sekta za kiuchumi na biashara.
Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakimsikiliza Balozi Mulamula (hayupo pichani)
Balozi Mulamula akiendelea kuzungumza
Balozi wa Qatar nchini, Mhe. Abdallah Jassim Al-Maadadi naye akizungumza katika maadhimisho hayo.
Sehemu nyingine ya Mabalozi waliohdhuria hafla hiyo.
Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. Hangi Mgaka (wa kwanza kulia), na Bw. Batholomeo Jungu (wa pili kutoka kulia) nao wakimsikiliza Balozi Al-Maadadi (hayupo), katika maadhimisho hayo.
Balozi Mulamula (wa pili kutoka kulia), Balozi wa Qatar nchini (wa tatu kutoka kulia), Balozi wa Demokrasia ya Kongo, Mhe. Juma Mpango (wa nne kutoka kushoto), Balozi wa Oman nchini, Mhe. Soud Ali Bin Mohamed Al Rugaishi (wa kwanza kushoto), Balozi wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Mhe. Abdulla Ibrahim Ghanim Al suwaidi (wa pili kutoka kushoto) wakishiriki tendo la kukata Keki ya maadhimisho ya Siku ya Taifa la Qatar.
Balozi Mulamula akizungumza na Balozi Al - Maadadi.
Balozi Mulamula akimtangaza mshindi wa bahati nasibu iliyochezeshwa hapo jana, mshindi huyo (hayupo pichani) alijishindia tiketi ya Ndege ya kuelekea Doha.
Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Al-Maadadi
Katibu Mkuu Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi waliohudhuria maadhimisho hayo.


Picha na Reginald Philip

Tuesday, December 15, 2015

Waziri wa Mambo ya Nje akutana na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) (kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Seiji Kihara yaliyofanyika katika Ofisi ya Wizara hiyo leo.

Walioshuhudia mazungumzo hayo kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Mbelwa Kairuki, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi, Mindi Kasiga na Katibu wa Waziri, Bw. Thobias Makoba.
Katikati ni Balozi wa Japani Mhe. Masahau Yoshinda nchini akiwa na Maofisa kutoka Serikali ya Japan.
Mazungumzo yanaendelea.
Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akikabidhi zawadi ya picha kwa Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan.
Balozi Mahiga akiagana na Mgeni wake Mhe. Kihara.


TAARIFA FUPI YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA KUHUSU UHUSIANO KATI YA JAPAN NA TANZANIA TAREHE 15 DESEMBA 2015


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amefanya mazungumzo leo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Seiji Kihara ambaye aliwasili nchini jana kama Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Japan Mhe.  Shinzo Abe ambapo kesho tarehe 16 Desemba 2015 anatarajiwa kuwasilisha Ujumbe wa Waziri Mkuu wa Japan kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.   Dk. John Pombe Joseph Magufuli.

Pamoja  na kuwasilisha ujumbe kwa Mheshimiwa Rais, mgeni huyo anatarajiwa kuhudhuria hafla ya utiaji saini wa mkataba wa mkopo wa dola za kimarekani milioni 96 utakaotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme wa Kenya na Tanzania wenye urefu wa kilometa 441.5 kutoka Singida na Manyara kupitia Babati na Arusha mpaka Namanga.


          MAHUSIANO KATI YA TANZANIA NA JAPAN
Tanzania na Japan zimekuwa katika uhusiano na ushirikiano wa karibu mara tu baada ya Tanzania kupata uhuru wake. Mahusiano hayo yamekuwa yakikua na kuimarika miaka hadi miaka katika nyanja mbalimbali ikiwemo miundombinu, afya, nishati, Kilimo, biashara, viwanda, usafirishaji na uwekezaji.  Kufanyika kwa ziara hii ya Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan ni muendelezo wa kukuza ushirikiano baina ya nchi zetu mbili.


            MIRADI MIPYA ITAKAYOFADHILIWA NA SERIKALI YA JAPAN



Serikali imeingia makubaliano na Serikali ya Japan kutekeleza miradi mitatu ya ujenzi wa barabara yenye lengo la kupunguza tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam linaloathiri uchumi wa nchi yetu. Miradi hiyo ni pamoja na:



    Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Juu katika eneo la TAZARA (TAZARA flyover):

Mkataba wa ujenzi wa Barabara hiyo tayari ulikwishasainiwa tangu tarehe 15 Oktoba 2015 na ujenzi unategemewa kuanza mapema mwakani.



              Mradi ya Ujenzi wa Barabara ya Morocco – Mwenge

Serikali ya Japan itafadhili upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco ili kuweza kupunguza msongamano wa magari.  Upanuzi wa barabara hii nao unatarajiwa kuanza mwakani.  Tayari Serikali imekwishaanza hatua za mwanzo za ujenzi wa barabara hiyo kufuatia uamuzi wa Mhe. Rais kuelekeza fedha zilizokuwa zigharamie sherehe za uhuru zitumike kuanza kazi ya upanuzi wa barabara hiyo.


            Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Gerezani mpaka bendera tatu

Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kwa fedha za msaada kutoka Serikali ya Japan. Ujenzi wa barabara hii nao unatarajiwa kuanza mwakani.



Mbali na miradi ya ujenzi wa barabara, Serikali ya Japan imeingia makubaliano na Serikali ya Tanzania kutekeleza miradi ya umeme kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme wa kutosha kwa matumizi ya wananchi na viwandani kama ilivyoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM.    Miradi itakayotekelezwa kwa ufadhili kutoka Japan ni pamoja na:



 Mradi ya Ujenzi wa Njia ya Kusafirishia Umeme Kenya – Tanzania Power Interconnection Project


Mradi huu una lengo la kuimarisha usambazaji kwa kuuza na  kununua umeme katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa Kenya. Ni ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme wenye KV400 na urefu wa kilomita 414.5 kutoka Singida na Namanga kupitia Babati na Arusha.

Mkataba wa mradi huu unatarajiwa kutiwa saini baadaye leo Wizara ya Fedha na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi wa  Mambo ya Nje wa Japan.



    Ujenzi wa mradi wa Mtambo wa kuzalisha umeme katika eneo la Kinyerezi (Kinyerezi II power plant project).



Mkataba wa ujenzi wa Mitambo ya kuzalisha umeme wa MW 300 huko Kinyerezi ulisainiwa  tarehe 27 Machi 2015 kati ya Serikali na Benki ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Kimaendeleo ya Japan (Japan Bank for International Cooperation – JBIC).  Utekelezaji wa Mradi huu unatarajiwa kuanza mapema mwakani.




Balozi Mulamula afungua Mkutano wa Asasi za Kiraia wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano wa siku mbili wa Asasi za Kiraia kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliwashirikisha wenyeviti wa asasi za kiraia kutoka nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu.
Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia ufunguzi wakati Katibu Mkuu, Balozi Mulamula akizungumza (hayupo pichani)
Sehemu nyingine ya wajumbe wakifuatilia ufunguzi
Wajumbe wengine wa mkutano
Mwenyekiti wa Asasi za Kiraia eneo la Maziwa  Makuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku akizungumza wakati wa mkutano huo.  

Wajumbe wakifuatilia wakati Mzee Butiku akizungumza
Balozi Mulamula akiagana na Mzee Butiku mara baada y akufungua mkutano
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Samwel Shelukindo (kushoto) akizungumza na mmoja wa washiriki wa mkutano mara baada ya ufunguzi

Balozi Mulamula akizungumza na Wandishi wa Habari kuhusu umuhimu wa Asasi za Kiraia katika eneo la Maziwa Makuu.
Picha ya Pamoja kati ya mgeni rasmi Balozi Mulamula na Wajumbe wa Mkutano

=================================

BALOZI MULAMULA: ASASI ZA KIRAIA ZINA MCHANGO MKUBWA KATIKA AMANI UKANDA WA MAZIWA MAKUU

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula  amesema kuwa Asasi za Kiraia zina nafasi kubwa katika utatuzi wa migogoro na kuleta amani hususan katika eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika kwa ujumla.

Balozi Mulamula aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa Wenyeviti wa Asasi za Kiraia kutoka Nchi za Maziwa Makuu unaofanyika kwa siku mbili katika Hoteli ya Golden Tulip, Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Kwanza wa Sekretarieti ya Maziwa Makuu alisema kuwa kwa uzoefu wake utatuzi wa migogoro, kulinda amani na katika kuhakikisha demokrasia na utawala wa sheria vinafuatwa kila chombo kina nafasi na umuhimu wake  na kwamba Asasi za Kiraia zina nafasi kubwa zaidi kwani zinawakilisha maoni ya wananchi.

“Asasi za Kiraia ni chombo muhimu sana katika kuhakikisha amani inakuwepo hususan katika Ukanda wa Maziwa Makuu kwani zinawawakilisha wananchi moja kwa moja hivyo ni vizuri kutambua nafasi yenu”, alisema Balozi Mulamula.

Aidha, aliipongeza Asasi hiyo ya ambayo kwa kiasi kikubwa imefanikiwa tangu ilipoanzishwa mwaka 2011 na kusisitiza ijikite zaidi katika kutekeleza  majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha misingi ya demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria katika nchi za Ukanda wa Maziwa makuu vinafuatwa na kutekelezwa kikamilifu.

“Najua mnazijua hadidu za rejea na wajibu wenu kama Asasi  za Kiraia, ni kuhakikisha nchi wanachama zinafuata misingi ya sheria, utawala bora na ule wa sheria ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara katika eneo letu la Maziwa Makuu”, alisisitiza Balozi Mulamula.

Awali akimkaribisha Balozi Mulamula kuzungumza, Mwneyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku alisema kwamba mkutano huo wa Wenyeviti wa Asasi kutoka nchi wanachama wa Maziwa Makuu ni muhimu sana hususan katika kipindi hiki ambapo pamoja na mambo mengine utaandaa na kupitisha agenda za Asasi hiyo zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari, 2016.

Aidha, aliongeza kuwa wakati umefika kwa Nchi Wanachama wa Maziwa Makuu kutambua mchango wa asasi za kiraia  na kuzishirikisha ipasavyo katika msuala muhimu hususan yale ya utatuzi wa migogoro ili kuleta tija kwenye eneo hili la Maziwa Makuu ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa na migogoro ya kisiasa na kikabila.

Mkutano huo wa siku mbili uliwashirikisha Wenyeviti wa Asasi kutoka nchi zote 12 wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Jamhuri ya Congo, Angola, Sudan na Zambia.

(Mwisho)

Katibu Mkuu, Balozi Mulamula akutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la IDLO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,  Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Sheria (IDLO) nchini Kenya, Bi. Enid Muthoni. Mkurugenzi huyo alikuja kwa lengo la kulitambulisha shirika hilo ambalo linajishughulisha na kuzijengea uwezo nchi katika masuala ya Utawala wa Sheria. Shirika hilo ambalo  lilianzishwa mwaka 1988  lina Makao Makuu  Mjini Roma, Italia.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Baraka Luvanda. Kulia ni Bw. Abdallah Mtibora, Afisa Mambo ya Nje.
Bi. Muthoni akifafanua jambo kwa Balozi Mulamula kuhusu shirika hilo la IDLO.
Mwakilishi wa IDLO hapa nchini, Prof. Gaston Kennedy kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nae akitoa maelezo ya nyongeza kuhusu shirika hilo.
Picha ya pamoja