Mhe. Waziri Mahiga akijibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa Wizara. Kushoto ni Mhe. Dkt. Kolimba, Naibu Waziri, Balozi Mlima (wa pili kulia), Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kulia) ==================================================
Waziri wa Mambo ya
Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine
Mahiga (Mb.), amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia
nidhamu, uadilifu na kuweka mbele maslahi ya Watanzania wote ili kuliletea
Taifa maendeleo.
Mhe. Dkt. Mahiga aliyasema
hayo hivi karibuni wakati wa mkutano wake wa kwanza na Watumishi wote wa Wizara
hiyo wakiwemo wa iliyokuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki
uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini
Dar es Salaam.
Mhe. Mahiga ambaye
kwenye mkutano huo aliongozana na Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb.),
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Aziz Ponary Mlima na Naibu Katibu Mkuu,
Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi alisema kuwa lengo la kukutana na Watumishi
wote ni kuwatakia heri ya mwaka mpya, kufahamiana, pamoja na kuwapa mwelekeo wa
utendaji wa Wizara kufuatia kuunganishwa kwa Wizara mbili.
Dkt. Mahiga alieleza
kuwa kuunganishwa kwa Wizara hizi mbili kuna lengo la kuboresha utendaji na
kuimarisha ushirikiano hususan katika masuala ya Kikanda na hivyo kuwataka
Watumishi wote kufanyakazi zao kwa ushirikiano wa hali ya juu huku wakizingatia
nidhamu, uadilifu, kuheshimiana, kujali utu, kutunza mali ya umma na kuwa
wabunifu.
“Watumishi wenzangu
kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu ambayo imeasisiwa na Rais wetu ina tafsiri pana sana.
Moja ya tafsiri hiyo ni kufanya kazi kwa malengo na weledi wa hali ya juu huku
tukizingatia nidhamu, uadilifu na kuepukana na ubadhirifu na matumizi mabaya ya
mali ya umma” alisema Waziri Mahiga.
Waziri Mahiga
aliongeza kusema kwamba, katika
kutekeleza kaulimbiu hiyo Watumishi wa Umma wanatakiwa kuzingatia kanuni,
taratibu na miongozo mbalimbali iliyowekwa ili kuepukana na vitendo viovu na
kutanguliza maslahi ya taifa mbele katika kuwatumikia wananchi. Aidha, Mhe.
Mahiga alisisitiza umuhimu wa kufanyakazi kwa uwazi na ubunifu huku akihimiza
Watumishi kujiendeleza kimasomo ili kujiongezea ujuzi.
Vile vile Dkt. Mahiga
alitumia fursa hiyo kuwaondoa hofu Watumishi wa iliyokuwa Wizara ya Afrika
Mashariki kwamba kuunganishwa kwa Wizara hizi hakutaathiri maslahi wala ajira
zao kwa namna yoyote ile na kuwataka kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano
wakati taratibu za kimuundo, kisheria na kiutumishi zikiendelea kukamilishwa.
“Nawaomba Watumishi
wote mfanyekazi zenu kwa ushirikiano na kwa wenzetu kutoka iliyokuwa Wizara ya
Ushirikiano wa Afrika Mashariki msijisikie unyonge kwani ajira zenu zitabaki
zilivyo na maslahi yenu hayataathirika kwa kuungana huku. Zaidi napenda
kwasisitiza muwe na mawazo endelevu na utayari wa kupokea mabadiliko”
alisisitiza Dkt. Mahiga.
Akichangia neno
wakati wa Mkutano huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba alisisitiza Watumishi
wa Wizara kufanyakazi kwa bidii huku wakiweka maslahi ya nchi mbele hususan
wanapotekeleza jukumu la msingi la Wizara la kuiwakilisha nchi nje ya mipaka
yake.
“Naomba niwapongeze
Watumishi wote kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuiwakilisha nchi kimataifa.
Lakini napenda kuwahimiza kuongeza nguvu zaidi katika kutekeleza majukumu yenu
ili kuendelea kutetea maslahi ya nchi yetu vizuri na kuiletea maendeleo”
alisema Dkt. Kolimba.
Awali akimkaribisha
Mhe. Waziri kuzungumza, Katibu Mkuu, Balozi Aziz Ponary Mlima alisema kuwa
Wizara imejiwekea utaratibu wa Watumishi wote kukutana na Waziri katika kila
robo ya mwaka yaani mara nne kwa mwaka ili kuweka mikakati ya pamoja na kuwa na
utendaji wenye tija.
-Mwisho-
|