Tuesday, January 12, 2016

Waziri Mahiga awataka Watumishi wa Wizara kufanya kazi kwa kuzingatia maadili

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akizungumza kwa mara ya kwanza na Watumishi wote wa Wizara kwa ajili ya kuwatakia heri ya mwaka mpya, kufahamiana nao na kuwapatia mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Mkutano huo umefanyika  hivi karibuni katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb.) naye akitoa salamu zake wakti wa mkutano huo wa kwanza na Watumishi wote wa Wizara.
Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wakimsikiliza Naibu Waziri (hayupo pichani)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, Balozi Aziz Ponary Mlima akizungumza machache wakati wa mkutano na Watumishi wa Wizara 
Sehemu nyingine ya Watumishi wa Wizara wakimsikiliza Katibu Mkuu (hayupo pichani)
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga akitoa ratiba ya mkutano huo wa Waziri na Watumishi wote.
Baadhi ya Wakurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Masahriki, Kikanda na Kimataifa nao wakifuatilia matukio wakati wa mkutano kati ya Waziri na Watumishi wa Wizara.
Sehemu nyingine ya Wakurugenzi wa Wizara nao wakifuatilia matukio
Bw. Abdallah Mtibora, Afisa Mambo ya Nje akiuliza swali kwa Mhe. Waziri wakati wa mkutano huo.
Bw. Octavian Kivyiro, Afisa kutoka Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji nae akiomba ufafanuzi wa baadhi ya mambo wakati wa mkutano huo
Mhe. Waziri Mahiga akijibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa Wizara. Kushoto ni Mhe. Dkt. Kolimba, Naibu Waziri, Balozi Mlima (wa pili kulia), Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kulia)
==================================================


Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia nidhamu, uadilifu na kuweka mbele maslahi ya Watanzania wote ili kuliletea Taifa maendeleo.

Mhe. Dkt. Mahiga aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa mkutano wake wa kwanza na Watumishi wote wa Wizara hiyo wakiwemo wa iliyokuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mahiga ambaye kwenye mkutano huo aliongozana na Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb.), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Aziz Ponary Mlima na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi alisema kuwa lengo la kukutana na Watumishi wote ni kuwatakia heri ya mwaka mpya, kufahamiana, pamoja na kuwapa mwelekeo wa utendaji wa Wizara kufuatia kuunganishwa kwa Wizara mbili.

Dkt. Mahiga alieleza kuwa kuunganishwa kwa Wizara hizi mbili kuna lengo la kuboresha utendaji na kuimarisha ushirikiano hususan katika masuala ya Kikanda na hivyo kuwataka Watumishi wote kufanyakazi zao kwa ushirikiano wa hali ya juu huku wakizingatia nidhamu, uadilifu, kuheshimiana, kujali utu, kutunza mali ya umma na kuwa wabunifu.

“Watumishi wenzangu kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu ambayo imeasisiwa na Rais wetu ina tafsiri pana sana. Moja ya tafsiri hiyo ni kufanya kazi kwa malengo na weledi wa hali ya juu huku tukizingatia nidhamu, uadilifu na kuepukana na ubadhirifu na matumizi mabaya ya mali ya umma” alisema Waziri Mahiga.

Waziri Mahiga aliongeza kusema  kwamba, katika kutekeleza kaulimbiu hiyo Watumishi wa Umma wanatakiwa kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali iliyowekwa ili kuepukana na vitendo viovu na kutanguliza maslahi ya taifa mbele katika kuwatumikia wananchi. Aidha, Mhe. Mahiga alisisitiza umuhimu wa kufanyakazi kwa uwazi na ubunifu huku akihimiza Watumishi kujiendeleza kimasomo ili kujiongezea ujuzi.

Vile vile Dkt. Mahiga alitumia fursa hiyo kuwaondoa hofu Watumishi wa iliyokuwa Wizara ya Afrika Mashariki kwamba kuunganishwa kwa Wizara hizi hakutaathiri maslahi wala ajira zao kwa namna yoyote ile na kuwataka kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano wakati taratibu za kimuundo, kisheria na kiutumishi zikiendelea kukamilishwa.

“Nawaomba Watumishi wote mfanyekazi zenu kwa ushirikiano na kwa wenzetu kutoka iliyokuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki msijisikie unyonge kwani ajira zenu zitabaki zilivyo na maslahi yenu hayataathirika kwa kuungana huku. Zaidi napenda kwasisitiza muwe na mawazo endelevu na utayari wa kupokea mabadiliko” alisisitiza Dkt. Mahiga.

Akichangia neno wakati wa Mkutano huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba alisisitiza Watumishi wa Wizara kufanyakazi kwa bidii huku wakiweka maslahi ya nchi mbele hususan wanapotekeleza jukumu la msingi la Wizara la kuiwakilisha nchi nje ya mipaka yake.

“Naomba niwapongeze Watumishi wote kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuiwakilisha nchi kimataifa. Lakini napenda kuwahimiza kuongeza nguvu zaidi katika kutekeleza majukumu yenu ili kuendelea kutetea maslahi ya nchi yetu vizuri na kuiletea maendeleo” alisema Dkt. Kolimba.

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri kuzungumza, Katibu Mkuu, Balozi Aziz Ponary Mlima alisema kuwa Wizara imejiwekea utaratibu wa Watumishi wote kukutana na Waziri katika kila robo ya mwaka yaani mara nne kwa mwaka ili kuweka mikakati ya pamoja na kuwa na utendaji wenye tija.


-Mwisho-







No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.