Wednesday, January 6, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mashauriano kuhusu mgogoro wa Burundi baina ya Tanzania, Angola, Uganda na Jumuiya ya Afrika Mashariki

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ameihakikishia dunia leo kuwa mazungumzo ya kuleta amani nchini Burundi bado yanaendelea vizuri licha ya taarifa zilizosambaa kuwa mazungumzo hayo yamegonga mwamba.
Dkt. Mahiga ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mashauriano baina yake na Mhe. George Pinto Chicoti, Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR); Mhe. Dkt. Crispus Kiyonga, Waziri wa Ulinzi wa Uganda ambaye ni mwakilishi wa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi Rais Yoweri Kaguta Museveni, pamoja na Dkt. Richard Sezibera, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha tarehe 6 Januari 2016.
Akielezea madhumuni ya mashauriano hayo Dkt. Mahiga alisema kuwa wadau hawa wanaunga mkono na kusifu jitihada zinazofanyika ndani na nje ya Burundi zenye lengo la kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa kisiasa na kiusalama nchini humo kwa njia ya majadiliano.
Aidha Waziri Mahiga alisema mazungumzo hayo pia yanalenga kubadilishana ushauri, mawazo na kuandaa taarifa ya pamoja kabla ya mikutano mikubwa ya kikanda; yaani ule wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR Summit), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Summit) na Umoja wa Afrika (AU Summit) inayotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwaka huu.
Dkt. Mahiga alisema mazungumzo yao yaliyojumuisha nchi za Tanzania, Angola na Uganda ambazo zimekasimiwa majukumu ya uenyekiti na usuluhishi na jumuiya zao, yatatoa uelewa wa pamoja wa jinsi ya kuendesha mashauriano ya kuleta amani ya kudumu kabla ya mikutano tarajiwa ambayo pamoja na mambo mengine, itajadili pia suala la amani na usalama nchini Burundi.
“Naomba nirudie tena mbele yenu waandishi wa habari kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli; kama wenyekiti wa jumuiya hii, bado tuna nia ya dhati kabisa ya kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunapata suluhu ya mgogoro huu, ambayo ni muhimu sana kwa usalama na maendeleo ya eneo letu na bara la Afrika kwa ujumla” alisisitiza Dkt. Mahiga kabla ya kuanza mazungumzo ya faragha na viongozi wenzake.
Waziri Dkt. Mahiga alipongeza jitihada za wadau wengine na jumuiya ya kimataifa zinazoendelea ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini humo.
           
MWISHO.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa.
06 Januari 2016


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.