Sehemu ya washiriki wa hafla ya siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa hafla hiyo ilifanyika jana Mei 19. |
=============================================
Na Mwandishi Maalum, New York
Umoja wa Mataifa, jana
Mei 19 umefanya hafla maalumu ya
siku ya Kimataifa ya Walinzi wa
Amani wanaohudumu katika Misheni mbalimbali za Kulinda Amani chini ya kofia ya
Umoja wa Mataifa.
Katika hafla hiyo
jumla ya walinzi 129 wanajeshi
na polisi waliopoteza maisha mwaka jana kwa kushambuliwa na makundi ya wapiganaji wenye silaha, matukio
ya kigaidi, ajali na kuumwa walikumbukwa
na kuenziwa kwa mchango wao.
Miongoni mwa Mashujaa
hao 129 kutoka nchi 50, wapo mashujaa watatu kutoka Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Mashujaa hao ni Sgt. Musa Abdrahamani Yusuf, Cpl. John Leornad
Mkude na Pte. Juma Ally Khamis.
Hafla hiyo maalum ya kutambua mchango wa walinzi
hao wa Amani na ambao wamejitolea
maisha yao kwaajili ya kuwalinda na kuokoka maisha ya wananchi
wasiokuwa na hatia katika
nchi zinazokabiliwa na vita na
migogoro ya wenyewenye kwa
wenyewewe iliongozwa na Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, ndiye aliyepokea medali maalum za mashuja hao
watatu kwa niaba ya familia zao. Medali waliyotunukiwa mashujaa hao na wengine inatambuliwa kama medali
ya Dag Hammarskjold.
Hafla ya mwaka huu, pamoja na
kutambua mchango wa mashujaa hao 129 ,
pia ilitambua kwa namna ya pekee na kwa
mara ya kwanza, mchango na kujitolea wa hali ya juu ulikofanywa na Kapteni
Mbaye Diagne raia ya Senegal,
aliyepoteza maisha mwaka 1994 wakati
akiokoa maisha ya wanyarwada
wakati wa mauaji ya kimbali.
Kapteni Mbaye Diagne ameeziwa
rasmi katika maadhimisho ya mwaka huu
kwa kupewa medali maalum iliyopewa jina la
Medali ya Mbaye Diagne, medali
ambayo alikabidhiwa mjane wa Mbaye Bibi
Yacine Mar Diop huku akishuhudiwa na
watoto wake wawili.
Kapten Mbaye Diagne alikuwa
mwangalizi wa Amani nchini Rwanda, kwa ushujaa mkubwa na bila ya kujali hatari iliyokuwa ikimkabili alitumia lori kuwaficha na kuwapeleka mahali
salama mamia ya wanyarwada wakati wa mauaji ya kimbali ya Rwanda.
Kwa kutambua ushujaa na
uthubutu wake huo, Baraza la Usalama lilibuni
mwaka 2014 medali ya Kapten Mbaye
Diagne ambayo watakuwa wanatunukiwa wanajeshi, polisi na raia ambao wameonyesha uthubutu na
ushupavu wa hali ya juu kiasi cha kupoteza maisha yao wakati wakitekeleza
majukumu yao.
Akizungumza wakati wa
halfa hiyo ambayo ilibeba majonzi ya aina yake,
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alieleza kwamba, hadi kufikia mwezi wa nne
mwaka huu, jumla ya walinzi wa Amani
3,400 wakiwamo wanajeshi, polisi
na raia walikuwa wamepoteza maisha tangu
kuanzishwa wa shughuli za ulinzi wa
Amani kwa kofia ya Umoja wa Mataifa
miaka 70 iliyopita.
“Wakati leo tunawaenzi
na kuwakumbuka mashujaa hawa 129 kutoka
mataifa 50 waliopoteza maisha yao mwaka
jana wakati wakitekeleza jukumu la kuwalinda wananchi wengine, jana ( Mei 18) walinzi wengine watano
wanaohudumu huko Mali wamepoteza maisha baada ya kushambuliwa”.
Akasema Ban Ki Moon kwa huzuni.