Wednesday, May 11, 2016

Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro washiriki uangalizi wa uchaguzi Kisiwani Anjouan

Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro, Bw. Mudrick Soragha akiwa katika picha ya pamoja na Meya wa Mji wa Mrigou, Bw. Abdul  Latif wakati Bw. Soragha alipoongoza ujumbe wa Ubalozi kwenye Uchaguzi kwenye Kisiwa cha Anjouan.
Mmoja wa Wagombea kwenye uchaguzi huo Bw. Azali Othman (katikati) akiwa na timu yake kwenye Kampeni
Bw. Soragha (kulia) na Bw. Thabit Khamis wakiwa kwenye moja ya maeneo ya kampeni
Bw. Soragha na Wajumbe wengine kutoka Ubalozini wakiwa katika picha ya pamoja na Meya wa Mji wa Sima, Bw. Abdallah Abdou (wa pili kulia)
=====================================================


Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro umeshiriki katika zoezi la uangalizi wa uchaguzi wa marejeo katika Kisiwa Anjouan. Uchaguzi huo unafanyika kufuatia Mahakama ya Katiba Visiwani Comoro kutoa amri ya kurejewa kwa uchaguzi wa majimbo 15 ambayo uchaguzi wake ulikumbwa na sintofahamu tarehe 10 Aprili 2016 ambapo zaidi ya wananchi 6305 kutoka Kisiwa hicho walishindwa kutekeleza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wao.

Maeneo yanayorejea uchaguzi huo ni Mramani, Niamboimro, Mrijou, Bambini, Mjimandra na Bougoueni. 

Kwa kutambua umuhimu wa chaguzi hizi, Ubalozi wa Tanzania kama moja wapo ya nchi inayowakilisha jumuiya ya kimataifa iliyopo Comoro imetuma ujumbe unaoongozwa na Bw. Mudrick Soragha,  Mkuu wa Utawala na Fedha kwa lengo la kujiridhisha na kujionea hali halisi ya namna mchakato huo utakavyokuwa. Ikumbukwe kwamba Tanzania ina mahusiano ya muda mrefu na Muungano wa Visiwa vya Comoro.

Mahusiano hayo yalipata nguvu zaidi baada ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mstari wa mbele katika Operesheni ya Kukikomboa Kisiwa cha Anjoun kutoka kwenye mikono ya mvamizi Kanali. Mohammed Bacar mwaka 2008 na kufanikiwa kukirejesha kisiwa hicho katika Umoja wa Visiwa vya Comoro.

Wakati ukiwa katika Kisiwa hicho, Ujumbe huo ulipata fursa ya kukutana na wadau  mbalimbali wa Siasa hasa viongozi wa Tume ya Uchaguzi wa Kisiwa ijulikanayo kama CEII, Meya wa Miji pamoja na viongozi wa Vyombo Vya Ulinzi na Usalama wa Kisiwa cha Anjoun. Katika mazungumzo na viongozi hao wote walionyesha kutaka uchaguzi huo ufanyike katika mazingira ya amani na utulivu ili wananchi wa miji hiyo wapate fursa ya kutekeleza haki yao ya msingi ya Kidemokrasia.

Ni matarajio ya Ubalozi kuwa uchaguzi huo utapita salama kama zilivyopita chaguzi nyingine. Licha ya ujumbe wa Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro pia Umoja wa Afrika na Jumuiya nyingine za kimataifa na kitaifa zipo Kisiwani Anjoun kungalia uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.