Thursday, May 5, 2016

Wizara ya Mambo ya Nje yafanya Mkutano na Vyombo vya Habari

 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Bi. Mindi Kasiga, akiongea na waandishi wa habari kwenye Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, ambapo alizungumzia Mkutano wa Tume ya pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda uliofanyika nchini Rwanda pamoja tarehe 28 hadi 1 Mei, 2016 na Kikao cha Serikali ya Tanzania na Zambia kilichojadili utatuzi wa changamoto za mipaka  kilichofanyika tarehe 27 Aprili, 2016.
Mkurugenzi wa Masomo katika Chuo cha Diplomasia, Dkt. Watengele Kitojo (kushoto) akiwa na Maafisa Habari wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na Taasisi zake wakati wa  Mkutano kati ya Wizara na Waandishi wa Habari. 
 Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia taarifa iliyokuwa ikitolewa na Msemaji wa Wizara.
Wakati Mkutano ukiendelea.
================================================



Kikao cha Kumi na Nne cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda, 29 Aprili – 1 Mei, 2016


Kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kilifanyika kuanzia tarehe 29 Aprili hadi Aprili, 2016, Mjini Gisenyi, Rwanda, ambapo wataalam wa sekta mbalimbali waliazimia kuharakisha maeneo ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Kikao hicho cha 14 cha ushirikiano kimefanyika kufuatia maagizo ya Marais wa Tanzania na Rwanda wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nchini Rwanda mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.

Wakati wa ziara hiyo, wakuu hao walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano na kuibua maeneo mapya yanayolenga kuinua shughuli za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho cha wataalamu kiongozi wa ujumbe wa Tanzania Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania aliwakumbusha wajumbe wa pande zote mbili kuendesha mazungumzo na mjadala kwa kuzingatia maagizo ya viongozi hao na vilevile kuchangamkia fursa za ushirikiano wa shughuli za kiuchumi za wananchi wa pande zote mbili baada ya mindombinu ya kikanda kuimarika.

Kwa upande wake, Balozi Jeanine Kambanda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda na mwenyeji wa kikao hicho, alihimiza wajumbe kujiwekea malengo yanayotekelezeka na tarehe za ukomo kwenye maeneo yote watakayokubaliana ili kusukuma utekelezaji na kupata matokeo ya haraka.

Pamoja na mambo mengine, pande zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu kama vile miundombinu ya ushoroba wa kati (central corridor), kuharakisha ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kimataifa (standard gauge), kukuza ushirikiano katika sekta ya anga hususan baina ya mashirika ya ndege ya Rwandair na ATCL, kuimarisha ushirikiano katika sekta za sayansi na teknolojia, afya, kilimo na ufugaji, utalii, elimu, mawasiliano n.k.

Mkutano huo pia umekubaliana kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Utekelezaji (Joint Implementation Committee) kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu maeneo yote ya ushirikiano yaliyokubaliwa katika Kikao hicho cha 14. Kamati hiyo itakayoongozwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizo mbili, itakutana kila robo mwaka.

Aidha, Serikali ya Rwanda imeonesha utayari wake wa kuleta nchini Maafisa na Watumishi wa Serikali kwa lengo la kupata uzoefu na mafunzo katika vyuo vya kitaalamu nchini kama vile Chuo cha Diplomasia  (CFR), Chuo cha Taifa cha Utalii na Wanyamapori  (Mweka) na Chuo cha Usafirishaji (NIT).

Kwa upande wa Tanzania, Serikali imedhamiria kuwakutanisha wataalamu wa mitaala ya elimu kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Rwanda kwenye upande wa kuandaa mitaala ya elimu ya tehama kwenye shule za awali, msingi na sekondari.

Mkutano ujao wa kumi na tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda utafanyika mwaka 2018, nchini Tanzania.

WAKATI HUO HUO, Kikao cha pamoja cha Makatibu Wakuu kati ya Tanzania na Zambia kwa ajili ya kujadili utatuzi wa changamoto za mpaka wa Nakonde Tunduma kilifanyika Lusaka Zambia 25 hadi 27 Aprili, 2016.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano  huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Dkt. Servacius Likwelile na kwa upande wa Zambia uliongozwa na Bw. Bright Nundwe, Katibu Mkuu wa Jimbo la Muchinga.

Miongoni mwa changamoto zilizojadiliwa na ufumbuzi wake wakati wa mkutano huo ni pamoja na:- Msongamano wa magari ambapo kwa  upande wa Zambia huduma kwa  magari ya mizigo zinafanyika hadi saa nne usiku na kwa magari ya abiria huduma inatolewa kwa masaa 24. Ili kupunguza msongamano, Tanzania imeiomba Zambia kutoa huduma kwa magari ya aina zote kama Tanzania inavyotoa huduma ya masaa 24; na Kuimarisha usalama mpakani ili kukabiliana na biashara haramu za kubadilisha fedha, biashara za magendo na biashara haramu za binadamu.

Mwisho, pande zote mbili zilikubaliana suala hilo lishughulikiwe kwa kufanya ukaguzi na ulinzi wa pamoja na kubadilishana taarifa za kiusalama.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,

 05 Mei, 2016




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.