Friday, May 20, 2016

UN YAWAENZI WALINZI WAKE WA AMANI WALIOPOTEZA MAISHA

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa  Balozi Tuvako Manongi akiwa ameshika medali  ya  Dag Hammarskjold waliyotunukiwa  mashujaa watatu watanzania ambao wamepoteza maisha mwaka jana wakati wakihudumu katika Misheni za kulinda Amani  za Umoja wa Mataifa. kushoto kwa Balozi ni Luteni Kanal  George Ita'ngare, mshauri wa  masuala ya kijeshi  katika Uwakilishi wa Kudumu na  kulia ni  Bw,Herve Ladsous,  Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya  Operesheni za Ulinsi wa Amani  za Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, akimvisha Bibi Yacine Mar Diop medal maalum ya   Kapteni Mbaye Diagne ambaye alikuwa ni  mume wa Bibi Yacine, Kapteni Diagne aliuawa mwaka 1994 wakati wa mauaji ya kimbali ya Rwanda. medali hiyo  maalum imebuniwa na  Baraza  la Usalama kwa kutambua ushujaa na uthubutu wake na kujituma kwake kwa hali ya juu hadi  kupelekea kupoteza maisha.  Kapteni  Diagne anakumbukwa  kwa namna alivyookoa maisha ya mamia ya wanyarwanda kwa kuwaficha kwenye lori na kuwapeleka  mahali salama kabla ya  yenye mwenyewe kuuawa.
Balozi Tuvako Manongi  akiandika katika kitabu cha  kuwaeni walinzi wa amani wa  Umoja wa Mataifa waliopotea maisha mwaka jana. miongoni mwa mashujaa 129 waliokumbukwa  wapo watanzania watatu ambao ni Sgt. Musa Abdrahamani Yusuf, Cpl John Leornad Mkude na Pte. Juma Ally Khamis 
Sehemu ya  washiriki wa hafla ya siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa hafla hiyo ilifanyika  jana Mei 19.

=============================================



Na Mwandishi Maalum, New York

Umoja wa Mataifa,  jana   Mei 19 umefanya  hafla  maalumu ya  siku ya Kimataifa ya  Walinzi wa Amani  wanaohudumu  katika Misheni mbalimbali za Kulinda Amani chini  ya kofia ya  Umoja wa Mataifa.

Katika   hafla hiyo  jumla ya walinzi 129  wanajeshi na  polisi waliopoteza maisha  mwaka  jana  kwa kushambuliwa na  makundi ya wapiganaji wenye silaha, matukio ya kigaidi, ajali na kuumwa    walikumbukwa  na kuenziwa kwa mchango wao.

Miongoni mwa Mashujaa hao  129   kutoka  nchi   50, wapo mashujaa watatu kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mashujaa hao ni  Sgt. Musa Abdrahamani Yusuf, Cpl. John Leornad Mkude na Pte. Juma Ally Khamis. 

Hafla  hiyo maalum ya kutambua mchango wa  walinzi  hao  wa Amani na ambao wamejitolea maisha  yao kwaajili ya  kuwalinda na kuokoka maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia   katika  nchi zinazokabiliwa na vita na  migogoro ya wenyewenye  kwa wenyewewe iliongozwa na Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa,  Ban Ki  Moon.

Mwakilishi wa Kudumu wa  Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi,  ndiye aliyepokea medali maalum za mashuja hao watatu kwa niaba ya familia zao.  Medali    waliyotunukiwa  mashujaa hao na  wengine inatambuliwa kama  medali   ya  Dag Hammarskjold.

Hafla ya mwaka huu,   pamoja na  kutambua mchango wa mashujaa hao 129 ,  pia  ilitambua kwa namna ya pekee  na kwa  mara ya kwanza,  mchango  na kujitolea wa hali ya juu  ulikofanywa   na Kapteni  Mbaye Diagne raia ya  Senegal, aliyepoteza maisha mwaka 1994 wakati  akiokoa maisha ya  wanyarwada wakati wa  mauaji ya kimbali.

Kapteni Mbaye Diagne ameeziwa rasmi katika maadhimisho ya mwaka  huu kwa kupewa medali maalum iliyopewa  jina  la  Medali ya  Mbaye Diagne, medali ambayo alikabidhiwa mjane wa Mbaye  Bibi Yacine Mar Diop  huku akishuhudiwa na watoto  wake wawili.

Kapten Mbaye Diagne alikuwa mwangalizi wa Amani nchini Rwanda, kwa ushujaa mkubwa na bila ya kujali  hatari iliyokuwa ikimkabili  alitumia lori kuwaficha na kuwapeleka  mahali  salama mamia ya wanyarwada wakati wa mauaji ya kimbali ya Rwanda.

Kwa kutambua ushujaa na uthubutu wake huo, Baraza la Usalama lilibuni   mwaka 2014 medali ya  Kapten Mbaye Diagne ambayo  watakuwa  wanatunukiwa wanajeshi,  polisi na raia ambao wameonyesha uthubutu na ushupavu wa hali ya juu kiasi cha kupoteza maisha yao wakati wakitekeleza majukumu yao.

Akizungumza wakati wa halfa  hiyo ambayo  ilibeba majonzi ya  aina yake,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,  alieleza kwamba,  hadi kufikia mwezi   wa nne mwaka huu, jumla ya walinzi wa Amani  3,400 wakiwamo  wanajeshi, polisi na raia walikuwa wamepoteza maisha  tangu kuanzishwa wa  shughuli za ulinzi wa Amani kwa  kofia ya Umoja wa Mataifa miaka 70 iliyopita.

“Wakati leo tunawaenzi na  kuwakumbuka mashujaa hawa 129 kutoka mataifa 50 waliopoteza maisha  yao mwaka jana  wakati wakitekeleza  jukumu la kuwalinda  wananchi wengine,  jana ( Mei 18) walinzi wengine watano wanaohudumu huko   Mali  wamepoteza maisha baada ya kushambuliwa”. Akasema Ban  Ki Moon kwa huzuni.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.