Wednesday, September 7, 2016

Waziri Mahiga azungumza na Vyombo vya Habari kuhusu Mkutano wa dharura wa EAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt Augustine Mahiga (Mb) akiongea katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam tarehe 7 Septemba, 2016.
Katika Mkutano huo Mhe. Mahiga aliwaarifu waandishi kuhusu Mkutano wa 17 wa Dharura wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika tarehe 08 Septemba , 2016, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na nchi wanachama wote wa Jumuiya hiyo.
Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano.
Sehemu nyingine ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano.






TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyika Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitisha Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Septemba, 2016.

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na vikao vya maandalizi vya Makatibu Wakuu na Mawaziri vilivyofanyika Jijini Arusha utajadili agenda kuu nne ambazo ni:- Mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara (EPA).

Agenda zingine ni Kupokea Taarifa ya Mwezeshaji wa mazungumzo ya Amani nchini Burundi, Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania; Kupata taarifa ya hatua za kukamilisha uanachama wa Sudan Kusini kwenye EAC; na
Kuapishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Rwanda.

Akizungumzia mkutano huo kwa Waandishi wa Habari, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa mkutano huu umeitishwa kwa dharura ili kuzungumzia agenda hizo muhimu hususan ile ya nchi wanachama kukubaliana kwa pamoja kusaini au kutosaini Mkataba wa EPA ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016.

Kuhusu Mkataba wa EPA, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza mazungumzo na Jumuiya ya Ulaya ya kushirikiana kibiashara kupitia EPA miaka 14 iliyopita na kuingia makubaliano ya awali mwaka 2014. Alieleza kuwa kwa mujibu wa makubaliano hayo ya awali EU na EAC zilikubaliana Mkataba huo usainiwe kwa pamoja na nchi zote za Jumuiyamwezi Julai 2016 kabla ya kuanza utekelezaji wake. 

Hata hivyo Tanzania ilitangaza kutosaini makubaliano hayo kwa sababu mkataba huo unaweza kukwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania nchi ya Viwanda na Uchumi wa kati ifikapo 2025.
Aidha, Tanzania inahitaji kujadiliana zaidi na nchi wanachama ili kujiridhisha kuwa mkataba huo hautoathiri Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki hususan hatua ya mwanzo ya mkataba ambayo ni Umoja wa Forodha. 

Kuhusu nchi nyingine wanachama Mhe. Mahiga alieleza kwamba, tayari Kenya na Rwanda zimesaini mkataba huo huku Uganda ikisubiri majadiliano ya nchi wanachama kabla ya kusaini na Burundi ikijitoa kusaini mkataba huo kwa vile tayari nchi za Ulaya zimeiwekea vikwazo vya kiuchumi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 07 Septemba 2016.

Tuesday, September 6, 2016

Kamati ya Sheria na Kinga ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki yakusanya Maoni ya Wadau, Dar es Salaam

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Sheria na Kinga ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe mara baada ya mkutano wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu  Mswada wa Sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa Binadamu.
Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mjumbe wa Kamati ya Kinga na Sheria, Mhe. Maryam Ussi (katikati) akizungumza na wadau (hawapo pichani), kushoto ni Mhe. Twaha Taslima,  Mbunge na Mjumbe wa Kamati hiyo na Kulia ni Bw. Ashery Wimile Karani Mwandamizi EALA
Mkurugenzi Msaidizi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Amani Mwatonoka (Wa kwanza kulia) akichangia hoja kwenye mjadala uliokuwa ukiendelea. 
Mdau akichangia jambo

Monday, September 5, 2016

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati akutana kwa mazungumzo na Kaimu Balozi wa S. Arabia nchini

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima (kulia) akisalimiana na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bw. Bandau Abdullah Al hazani. Kaimu Balozi huyo alikuja Wizarani kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia.
Balozi Kilima akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania.
Mazungumzo yakiendelea

Saturday, September 3, 2016

Waziri Mahiga aongoza Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya SADC

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
Coat of Arms
Simu: 255-22-2114615, 211906-12 
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

               

                20 KIVUKONI FRONT,
                           P.O. BOX 9000,
                  11466 DAR ES SALAAM,  
                                    Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri Mahiga aongoza Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya SADC -Uchaguzi wa Jamhuri ya Shelisheli

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb.), jana tarehe 2 Septemba, amezindua Misheni ya Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC kwenye uchaguzi wa Jamhuri ya Shelisheli kwa niaba ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa  Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika -SADC Organ.
Misheni hiyo ya waangalizi wa uchaguzi  itakayojumuisha waangalizi kutoka nchi za SADC, itashiriki kwenye uangalizi katika vituo vyote 25 vya upigaji kura nchini Shelisheli. Pamoja na kuongoza misheni hiyo, Tanzania kama Mwenyekiti wa SADC Organ itaongoza timu za uandishi wa taarifa ya SADC pamoja na ufuatiliaji wa taarifa za vyombo vya habari kuhusu mwenendo mzima wa uchaguzi nchini humo unaotarajiwa kufanyika tarehe 8-10 Septemba, 2016.
Tanzania ilikabidhiwa nafasi ya uenyekiti wa kuongoza asasi hii muhimu ya Jumuiya, wakati wa Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika huko Mbabane, Swaziland tarehe 29 – 31 Agosti, 2016. Mara baada ya kukamilika kwa Mkutano huo, Mhe.  Dkt. Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alielekea Jamhuri ya Shelisheli kumwakilisha Mhe. Dkt. Magufuli, katika kuongoza ujumbe wa Waangalizi wa SADC.
Wajibu wa Tanzania kuongoza Misheni hya Waangalizi wa Uchaguzi imetokana na misingi na muongozo wa Jumuiya ya SADC ya kuwa na chaguzi za kidemokrasia katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.
Waziri Mahiga anatarajiwa kutoa taarifa ya awali ya Misheni hiyo ya waangalizi  wa SADC Septemba 12, 2016.
Mwisho



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akifungua Misheni ya timu ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Wabunge tarehe 2 Septemba, 2016 Mahe-Shelisheli. Mheshimiwa Waziri anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika picha ya pamoja na Misheni ya timu ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Wabunge tarehe 2 Septemba, 2016 huko Mahe-Shelisheli.

Wednesday, August 31, 2016

Mkurugenzi wa Idara ya Asia akutana na Mwakilishi masuala ya Uchumi Ubalozi wa China

Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbelwa Kairuki (kulia) akizungumza na  mwakilishi wa masuala ya Uchumi na Biashara wa Jamhuri ya Watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw.Li Zhiyong ambaye alimtembelea katika Ofisi za Wizara tarehe 31 Agosti, 2016.
 Mazungumzo yao yalijikita katika kujadili maandalizi ya mkutano wa 5 wa Kamati ya Pamoja ya Uchumi, Biashara, Uwekezaji na Ushirikiano wa masuala ya Teknolojia  kati ya Tanzania na China unaotarajiwa kufanyika nchini   tarehe 13 Oktoba, 2016.
Maafisa wa Ubalozi wa China wakifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Mbelwa na Bw. Zhiyong (hawapo pichani)
Mazungumzo yakiendelea

Monday, August 29, 2016

Waziri Mkuu atembelea Banda la Tanzania na nchi zingine maonesho ya TICAD VI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisikiliza maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade, Bw. Edwin Rutageruka kuhusu Michoro maarufu ya Tanzania ijulikanayoo kama Tingatinga alipotembelea Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan yaliyofanyika Jijini Nairobi wakati wa Mkutano wa TICAD VI. Wengine wanaoshuhudia ni Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Chirau Ali Mwakere (wa kwanza kushto),  Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki ya Kenya, Bi. Betty Maina na Kaimu Balozi wa Tanzania, Kenya, Bi. Talha Waziri.
Bw. Rutageruka akisisitiza jambo kuhusu michoro hiyo kuwa asili yake ni Tanzania na si sehemu nyingine yoyote
Mhe. Waziri Mkuu akifurahia jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Cliford Tandari (kushoto) alipowasili kwenye Banda la maonesho la TIC.
Mhe. Waziri Mkuu akisaini kitabu cha wageni kwenye Banda la TIC huku Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho Bw. Tandari na Maafisa kutoka TIC wakishuhudia.
Mhe. Wazir Mkuu akimsikiliza Meneja wa Uwekezaji wa EPZA, Bw. Lameck Borega alipotembelea Banda lao la Maonesho.
Mhe. Waziri Mkuu akisalimiana na Bi. Alistidia Karaze, Afisa Utafiti Mkuu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) alipotembelea Banda la Maonesho la TTB.
Bi. Karaze akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu kuhusu mikakati ya kutangaza Utalii inayofanywa na TTB.
Mhe. Waziri Mkuu nae akitoa maelekezo kuhusu namna bora ya kujipanga katika kutangaza utalii. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Sayansi, Prof. Makame Mbarawa ambaye naye alikuwa Jijini Nairobi kuhudhuria Mkutano wa TICAD VI
Mhe. Waziri Mkuu akipata maelezo kuhusu soko la Batiki kutoka kwa mmoja wa akina mama wa Kitanzania wanaoshiriki maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan Jijini Nairobi alipotembelea Banda lao. Kushoto ni Bw. Francis Mosongo, Afisa Mwandamizi wa Dawati la Japan katika Ubalozi wa Tanzania, Japan.
Mhe. Waziri Mkuu akimsikiliza mshiriki mwingine kutoka Tanzania ambaye anajishughulisha na biashara ya bidhaa kutoka Tanzania kama vitege, khanga, na batiki

Mhe. Waziri Mkuu akiwa ametembelea Banda la Maonesho la Rwanda

Mhe. Waziri Mkuu akipata maelezo alipotembelea Banda la Maonesho la Kenya

Mhe. Waziri Mkuu akikaribishwa alipotembelea Banda la Maonesho la Uganda
Mhe. Waziri Mkuu akinsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Sumitomo ya Japan alipotembelea Bandani hapo. Kampuni ya Sumitomo ndiyo inajenga mitambo ya uzalishaji wa Umeme wa gesi asilia wa Megawati 240 iliyopo Kinyerezi Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo wa Sumitomo akimwonesha Waziri Mkuu picha za Mitambo ya Umeme iliyopo Kinyerezi
Mhe. Waziri Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya waliofika Uwanja wa Ndege wa Jommo Kenya kwa ajili ya kumsindikiza kabla ya kuondoka kurejea nchini mara baada ya kuhudhuria Mkutano wa TICAD VI. Katika Picha ni Bi. Talha Waziri, Kaimu Balozi wa Tanzania, Kenya; Bw. Mkumbwa Ally (wa pili kushoto), Bw. Amos Mwakasege (kushoto) na Bw. Loshilaari Ole Kambainei (Kulia), Maafisa Waandamizi Ubalozini hapo.


Sunday, August 28, 2016

Tanzania kushirikiana na Japan katika mafunzo kwa Wahandisi wa Gesi


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa kwenye Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan lililofanyika Nairobi, Kenya wakati wa Mkutano wa TICAD VI. Kongamano hilo pia lilifuatiwa na hafla ya baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kuingia makubaliano na Makampuni na Mashirika ya Japan katika kuimarisha biashara na uwekezaji. Mhe. Majaliwa alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa TICAD VI uliofanyika tarehe 27 na 28 Agosti, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyeji na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa TICAD VI akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan. Kushoto ni Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe na kulia ni Naibu Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto
Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe nae akizungumza kwenye Kongamano hilo
Baadhi ya Marais, Mawaziri Wakuu na Makamu wa Rais wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Kongamano la Biashara la Afrika na Japan. Kushoto ni Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Viongozi akiwemo Mhe. Majaliwa wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Mjumbe kutoka Chiyoda kuashiria Makubaliano kati ya Tanzania na Shirika la Chiyoda ambalo litashirikiana na Tanzania katika kutoa mafunzo kwa Wahandisi kwenye masuala ya gesi na mafuta. Waliosimama kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe; Bw. Francis Mossongo, Afisa Mwandamizi wa Dawati la Japan, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mkurugenzi wa Shirika la Chiyoda.
============================================

Tanzania kushirikiana na Japan katika mafunzo kwa Wahandisi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameshiriki hafla iliyoashiria kusainiwa kwa makubaliano kati ya baadhi ya nchi za Afrika na Makampuni mbalimbali ya Japan iliyofanyika wakati wa Mkutano TICAD VI jijini Nairobi.

Hafla hiyo ambayo ilitanguliwa na Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan ilihusisha nchi 20 za Afrika ambazo zimeingia makubaliano ya kuimarisha uwekezaji na biashara na Makampuni makubwa 22 ya Japan.

Kwa upande wa Tanzania, Serikali imeingia Makubaliano na Shirika la CHIYODA kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wahandisi wa Tanzania kwa kuwapitia mafunzo kwenye masuala ya teknolojia ya gesi na mafuta.

Akizungumza wakati wa Kongamano hilo Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta alisema kuwa Kongamano hilo ni jukwaa muafaka wakati Afrika ikiwa katika jitihada za mageuzi ya kiuchumi. Hivyo aliziomba nchi za Afrika kutumia ujuzi na uzoefu mkubwa wa Japan katika kuiimarisha Sekta Binafsi ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia maendeleo.

Aidha, aliongeza kuwa Kenya ikiwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wenzake kuhakikisha kunakuwepo mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji kutoka nje hususan Japan. Pia aliishukuru Serikali ya Japan kwa ushirikiano mkubwa inaotoa kwa Afrika na kukaribisha uwekazaji kutoka sekta binafsi ya Japan kwenye maeneo ya uzalishaji wa nishati ya umeme na maeneo mengine.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe alisema kuwa Japan itaendelea kushirkiana na Afrika katika kuhakikisha inapiga hatua zaidi ya maendeleo. Aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano kati ya Afrika  na Japan Kampuni 22 na Vyuo Vikuu vya Japan zimefuatana nae ili kukamilisha mikataba 73 na nchi za Afrika. 

Aidha,  alieleza kuwa Kampuni za Japan zimetumia fursa ya Mkutano wa TICAD  VI kutangaza Azimio la Biashara ikiwa ni katika kuelezea nia na madhumuni yao katika kuchangia maendeleo ya Afrika.

Mbali na Tanzania nchi zingine za Afrika zilizoingia Makubaliano na Kampuni na Mashrika kutoka Japan ni pamoja na Kenya, Angola, Cameroon, Congo, Cote d’ Ivoire, DRC, Ethiopia, Misri, Ghana, Madagascar, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Rwanda, Seychelles, Afrika Kusini, Uganda na Zambia.

Wakati huohuo, Mkutano wa Sita wa Kilele wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD VI) umemalizika   Jijini Nairobi leo huku Wakuu wa Nchi na Serikali wakipitisha kwa kauli moja Azimio la Nairobi na Mpango Kazi  wa utekelezaji wake.

Azimio la Nairobi pamoja na mambo mengine linalenga katika kutekeleza mambo makuu matatu  ambayo ni: Kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchumi ili kuwa na vyanzo mbadala vya kuendesha uchumi huku mkazo ukiwekwa kwenye uanzishwaji wa viwanda vitakavyozalisha ajira kwa wingi kwa vijana wa Afria; Kujenga mifumo ya Huduma za Afya ambazo ni endelevu kwa maisha bora ikiwemo kuboresha huduma za afya, kuweka mikakati ya kukabiliana na magonjwa kama Ebola, kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na jamii nzima; na Kukuza na kuimarisha Utulivu na Ustawi wa Jamii.

Mbali na Mkutano wa Kilele wa TICAD VI, shughuli zingine zilizoenda sambamba na mkutano huo ni Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan; Maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan; na Mkutano wa Majadilino ya Kibiashara kati ya Viongozi Wakuu wa Serikali na Wakurugenzi Wakuu wa Makampuni Binafsi.

Mkutano wa TICAD VI ambao ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali zaidi ya 30 kutoka Afrika, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda pia uliyashirikisha Makampuni zaidi ya 100 kutoka Serikali ya Japan, Sekta Binafsi na kuhudhuriwa na zaidi ya Wajumbe 10,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani.

-Mwisho-



Waziri Mkuu akutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Jijini Nairobi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan, Mhe. Luteni Jenerali Barki Hassan Salih walipokutana Jijini na Nairobi wakati wa Mkutano wa TICAD VI kwa mazungumzo ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Mhe. Majaliwa akiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba(kushoto) na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Bi. Talha Waziri (wa pili kulia) na Bi. Irene Bwire, Mwandishi wa Waziri Mkuu wakifuatilia mazungumzo  kati yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan, Mhe. Lt. Gen. Salih na ujumbe wake hawapo pichani)
Mhe. Salih (wa tatu kushoto) akiwa na ujmbe aliofuatana nao wakati wa mazungumzo yake na Mhe. Majaliwa (hayupo pichani)