TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano
wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kufanyika Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitisha Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu
wa Nchi Wanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika Ikulu, Jijini
Dar es Salaam tarehe 09 Septemba, 2016.
Mkutano
huo ambao ulitanguliwa na vikao vya maandalizi vya Makatibu Wakuu na Mawaziri
vilivyofanyika Jijini Arusha utajadili agenda kuu nne ambazo ni:- Mahusiano ya
kibiashara na uwekezaji kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa
Ulaya (EU) kupitia Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara (EPA).
Agenda zingine ni Kupokea Taarifa
ya Mwezeshaji wa mazungumzo ya Amani nchini Burundi, Mhe. Benjamin William
Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania; Kupata taarifa ya hatua za kukamilisha
uanachama wa Sudan Kusini kwenye EAC; na
Kuapishwa
kwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Rwanda.
Akizungumzia
mkutano huo kwa Waandishi wa Habari, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa mkutano huu umeitishwa
kwa dharura ili kuzungumzia agenda hizo muhimu hususan ile ya nchi wanachama kukubaliana
kwa pamoja kusaini au kutosaini Mkataba wa EPA ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016.
Kuhusu
Mkataba wa EPA, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza
mazungumzo na Jumuiya ya Ulaya ya kushirikiana kibiashara kupitia EPA miaka 14
iliyopita na kuingia makubaliano ya awali mwaka 2014. Alieleza kuwa kwa mujibu
wa makubaliano hayo ya awali EU na EAC zilikubaliana Mkataba huo usainiwe kwa
pamoja na nchi zote za Jumuiyamwezi Julai 2016 kabla ya kuanza utekelezaji
wake.
Hata
hivyo Tanzania ilitangaza kutosaini makubaliano hayo kwa sababu mkataba huo
unaweza kukwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania
nchi ya Viwanda na Uchumi wa kati ifikapo 2025.
Aidha,
Tanzania inahitaji kujadiliana zaidi na nchi wanachama ili kujiridhisha kuwa
mkataba huo hautoathiri Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki hususan
hatua ya mwanzo ya mkataba ambayo ni Umoja wa Forodha.
Kuhusu
nchi nyingine wanachama Mhe. Mahiga alieleza kwamba, tayari Kenya na Rwanda zimesaini
mkataba huo huku Uganda ikisubiri majadiliano ya nchi wanachama kabla ya kusaini
na Burundi ikijitoa kusaini mkataba huo kwa vile tayari nchi za Ulaya zimeiwekea
vikwazo vya kiuchumi.
Imetolewa na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar
es Salaam,
07 Septemba 2016.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.