|
Waziri Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga
akipeana mkono na Balozi wa Cuba nchini anayemaliza muda wake, Mhe. Jorge Luis
Lopes Tormo wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika Jijini Dar es Salaam
|
===================================================================
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, ameipongeza Serikali ya Cuba kwa mchango wake wa maendeleo hapa nchini hususan katika sekta za elimu, afya na kilimo.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mahiga wakati wa hafla fupi ya kumuaga Balozi wa Cuba aliyemaliza muda wake wa kazi nchini, Mhe. Jorge Luis Lopes Tormo.
Katika hotuba yake Mhe. Mahiga alisema kuwa, nchi
ya Cuba imekuwa ikichangia na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini
katika sekta ya afya, elimu, kilimo na michezo ikiwa ni jitihada za nchi hiyo za kukuza na kudumisha uhusiano mzuri
na wa muda mrefu wa kidiplomasia uliojengeka baina ya nchi hizi mbili.
Mhe. Mahiga alieleza kuwa, takwimu
zinaonesha katika sekta ya elimu, kwa kipindi cha mwaka 2008 hadi 2014
jumla ya wanafunzi 64 kwa ngazi ya elimu ya juu walipata nafasi za kwenda kusoma
nchini Cuba katika tasnia mbalimbali.
Aidha alisema kwamba, Serikali ya Cuba inaendelea kufadhili mradi wa elimu kwa watu wazima
unaojulikana kama “NDIO NAWEZA” (“Yes I CAN”), ulioanzishwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na Cuba mwaka 2011 chini ya wataalamu kutoka
Wizara ya Elimu ya Tanzania na Cuba na kuzinduliwa mwaka 2014.
Mradi huu unaotekelezwa
nchini kwa awamu, sasa unatelezwa katika miji 7 ya Ilala, Temeke, Kinondoni, Manispaa ya Dodoma, Manispaa ya Songea Mwanga, Bagamoyo na Mkuranga. Mpaka sasa
jumla ya vijana na wazee 2670 wamenufaika na mradi, na inategemewa kuwa ifikapo
mwishoni mwa mwaka 2017 mradi utakuwa umewanufaisha jumla ya vijana na wazee 3,321,840.
Kwa
upande wake Mhe. Balozi Jorge Luis Lopes Tormo aliishukuru Serikali ya Tanzania
kwa ushirikiano mzuri aliopewa wakati wa kutekeleza majukumu yake kwa kipindi
cha miaka takrbani mitano aliyokuwepo nchini.
Pia
alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi madhubuti wa
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kusimamia vyema raslimali za taifa kwa
maendeleo ya watu wote.
Vilevile Balozi Tormo alitumia fursa hiyo kuihakikishia Serikali ya
Tanzania kuwa Cuba itaendelea kuwa mshirika mzuri wa shughuli za maendeleo ikiwemo
kuangalia maeneo mbalimbali na fusra ambazo Cuba inaweza kuwekeza nchini, kwa
lengo la kuongeza ajira kwa vijana, pato la taifa na kuongeza kasi ya ukuaji wa
teknolojia.
Uhusiano
wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba ulianzishwa mwaka 1962 ukiasisiwa na
viongozi wakuu wa nchi hizo Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati
Fidel Castro.
-Mwisho-