Friday, January 20, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA UTURUKI NCHINI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Uturuki nchini

Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 22 na 23 Januari 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Mhe. Rais Erdogan ambaye ataambatana na Mkewe, na kuongoza ujumbe wa watu 150 wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Maafisa kutoka Serikalini na Wafanyabiashara anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 22 Januari, 2017 jioni  na atapokelewa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uturuki na Tanzania pamoja ‎na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara  na uwekezaji.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Erdogan  atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa  na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili na baadaye Marais hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali. 

Siku hiyo ya tarehe 23 Januari, 2017, kutakuwa na Kongamano la Biashara kati ya Uturuki na Tanzania litakalowakutanisha Wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili. Kongamano hilolitahutubiwa na viongozi wa Tanzania na Uturuki.

Mhe. Rais Erdogan na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Mahusiano ya Uturuki na Tanzania

Mahusiano ya Tanzania na Uturuki ni mazuri. Ikumbukwe kuwa, kufunguliwa kwa mara nyingine kwa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini mnamo Mei 2009 kuliongeza kasi ya mahusiano baina ya nchi hizi mbili. Katika hatua nyingine Tanzania imetangaza kufungua Ubalozi wake nchini Uturuki na hivi leo Mhe. Rais atamwapisha Balozi Mteule, Prof. Elizabeth Kiondo atakayetuwakilisha Uturuki.
Pia kumekuwa na ziara za viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi hizi mbili ikiwemo ziara ya Rais mstaafu wa Uturuki, Mhe. Abdullah Gul  nchini mwaka 2009 ; ziara ya Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Uturuki mwaka 2010 na ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein mwaka 2011.
Tume ya Pamoja ya Biashara
Tanzania na Uturuki zinashirikiana pia kupitia Tume ya Pamoja ya Biashara ambayo ilianzishwa baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Ushirikiano kwenye masuala ya Biashara mwaka 2010. Kikao cha kwanza cha Tume hiyo kilifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Novemba 2012. Katika kikao hicho pande zote zilikubaliana kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, elimu, Kilimo, Nishati na Madini, Maendeleo ya viwanda na mawasiliano ya simu.

Kikao cha Pili cha Tume ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Uturuki kilifanyika tarehe 11 – 12 Januari 2017, Uturuki kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Makubaliano ya Kikao cha Kwanza na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya pande hizi mbili. Aidha, Mkutano huu pia ulikuwa na umuhimu wa kipekee kwa kuwa ulifanyika ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Kiserikali ya Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoğan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Januari, 2017.

Pande zote mbili zimekubaliana kuongeza nguvu katika kuhamasisha uwekezaji kwenye nchi zetu. Katika kutekeleza hili, Uturuki imepanga kuandaa Mkutano wa Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki ndani ya robo ya pili ya mwaka huu jijini Istanbul. Vile vile, nchi zote mbili zimekubaliana kubadilishana taarifa za fursa za uwekezaji kupitia Balozi zetu na Baraza la Biashara la Tanzania na Uturuki. 

Aidha, Taasisi zetu za Uwekezaji zimeelekezwa kuanza majadiliano ya kuingia Mkataba wa Ushirikiano ili kuhamasisha uwekezaji nchini. Hali kadhalika, Uturuki imemchagua Mwambata wa Biashara katika Ubalozi wao wa Dar es Salaam na Tanzania imeahidi kuteua Afisa Maalum ndani ya mwezi mmoja kushughulikia uhamasishaji wa uwekezaji na biashara kati ya nchi hizi mbili.

Mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki

Tangu kuanzishwa kwa Tume ya pamoja ya ushirikiano ya kiuchumi mafanikio ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili yameonekana ikiwemo:- Kuimarishwa kwa ushirikiano katika masuala ya Usafiri wa Anga ambapo Shirika la Ndege la Uturuki lilianzisha safari tatu  za moja kwa moja kutoka Istanbul hadi Dar es Salaam, Kilimanjaro na hivi karibuni Zanzibar. Kuanzishwa kwa safari hizi kumekuza biashara kati ya Uturuki na Tanzania  ambapo mwaka 2009  ukubwa wa biashara ulikuwa Dola za Marekani milioni 66 sawa na shilingi bilioni 145.2 lakini hadi kufikia Februari 2016 biashara kati  ya nchi hizi mbili iliongezeka kwa Dola za Kimarekani milioni 160 sawa na shilingi bilioni 352. 

Aidha, kuzinduliwa kwa Baraza la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki mwaka 2013 ambalo kumewezesha kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi za nchi hizi mbili na  Kuongezeka kwa Makampuni ya Uturuki yaliyowekeza nchini ambapo hadi sasa ni Kampuni 30 zimefanya uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 305.08 na zinatarajiwa kutengeneza ajira 2,959.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
20 Januari, 2017

Waziri Mahiga akutana na Balozi Korhonen wa Finland nchini



Waziri ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi Klaus Korhonen wa Finland walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo wamejadili masuala mbalimbali kuhusu biashara na kudumisha uhusiano wa kidplomasia baina ya Tanzania na Finland

Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifafanua jambo, wa kwanza kushoto ni Balozi wa Finland nchini Tanzania, Balozi Mhe.Pekka Hukka akifuatilia mazungumzo

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akimsikiliza Balozi Klaus Korhonen wa Finland

Mazungumzo yakiendelea
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kulia) akifuatilia Mazungumzo

Tuesday, January 17, 2017

Banda la Wizara ya Mambo ya Nje lilivyong'ara kwenye Tamasha la Tatu la Biashara Zanzibar.


Bw. Othman Maalim Othman (kulia), Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitoa maelezo kuhusu majukumu ya Wizara hiyo  kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein. Mwingine ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Amina Salum Ali.
Bi. Vivian Rutaihwa, Afisa Biashara kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki naye akitoa maelezo kwa Mhe. Rais ya namna ya wajasiriamali wa Tanzania watakavyoweza kufaidika kwa kutumia soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Naibu Waziri (OR) wa Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Khamisi Juma Mwalim anbaye aliwahi kuwa mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje akisaini Kitabu cha wageni katika Banda la Wizara hiyo.
Bi. Vivian Rutaihwa, Afisa Biashara kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitoa maelezo kwa Mhe. Rais wa Awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi ya namna ya wajasiriamali wa Tanzania watakavyoweza kufaidika kwa kutumia soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alhaji Ali Hassan Mwinyi akisaini Kitabu cha wageni katika banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi Silima Haji Kombo, Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar naye alitembelea banda la Wizara ya Mambo ya Nje.

Diwani wa Kata ya Magomeni huko Zanzibar akipata maelezo kutoka kwa Bw. Tahir Bakari, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje kuhusu masuala mbalimbali ya utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, Mhe. Amina Salum Ali akitoa hotuba ya kufunga Tamsaha la Tatu la  Biashara ambalo ni sehemu ya shamrashamra ya sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi.
Mhe. Waziri akikabidhi vyeti kwa baadhi ya washiriki waTamsaha la Tatu la  Biashara.

Monday, January 16, 2017

Naibu Waziri asaini kitabu cha maombolezo

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisaini kitabu cha maombolezo kwenye makazi ya Balozi wa Msumbiji nchini Mhe. Monica Patricio yaliyopo Jijini Dar es Salaam kufutia kifo cha mtoto wa Balozi huyo. 

Wednesday, January 11, 2017

Waziri Mahiga aipongeza Cuba kwa kuchangia maendeleo nchini


                               Waziri Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipeana mkono na Balozi wa Cuba nchini    anayemaliza muda wake, Mhe. Jorge Luis Lopes Tormo wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika Jijini Dar es Salaam
===================================================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, ameipongeza Serikali ya Cuba kwa mchango wake wa maendeleo hapa nchini hususan katika sekta za elimu, afya na kilimo.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mahiga wakati wa hafla fupi ya kumuaga  Balozi wa Cuba aliyemaliza muda wake wa kazi nchini, Mhe.  Jorge Luis Lopes Tormo.

Katika hotuba yake Mhe. Mahiga alisema kuwa, nchi ya Cuba imekuwa ikichangia na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini katika sekta ya afya, elimu, kilimo na michezo  ikiwa ni jitihada za nchi hiyo za kukuza na kudumisha uhusiano mzuri na wa muda mrefu wa kidiplomasia uliojengeka baina ya nchi hizi mbili.

Mhe. Mahiga alieleza kuwa, takwimu zinaonesha  katika sekta ya elimu, kwa kipindi cha mwaka 2008 hadi 2014 jumla ya wanafunzi 64 kwa ngazi ya elimu ya juu walipata nafasi za kwenda kusoma nchini Cuba katika tasnia mbalimbali.

Aidha alisema kwamba, Serikali ya Cuba inaendelea kufadhili mradi wa elimu kwa watu wazima unaojulikana kama “NDIO NAWEZA” (“Yes I CAN”), ulioanzishwa kwa pamoja baina ya  Serikali ya Tanzania na Cuba mwaka 2011 chini ya wataalamu kutoka Wizara ya Elimu ya Tanzania na Cuba na kuzinduliwa mwaka 2014. 

Mradi huu unaotekelezwa nchini kwa awamu, sasa unatelezwa katika miji 7 ya Ilala, Temeke, Kinondoni, Manispaa ya Dodoma, Manispaa ya Songea  Mwanga, Bagamoyo na Mkuranga. Mpaka sasa jumla ya vijana na wazee 2670 wamenufaika na mradi, na inategemewa kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017 mradi utakuwa umewanufaisha jumla ya vijana na wazee 3,321,840.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Jorge Luis Lopes Tormo aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri aliopewa wakati wa kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka takrbani mitano aliyokuwepo nchini.

Pia alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kusimamia vyema raslimali za taifa kwa maendeleo ya watu wote. 

Vilevile Balozi Tormo alitumia fursa hiyo kuihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa Cuba itaendelea kuwa mshirika mzuri wa shughuli za maendeleo ikiwemo kuangalia maeneo mbalimbali na fusra ambazo Cuba inaweza kuwekeza nchini, kwa lengo la kuongeza ajira kwa vijana, pato la taifa na kuongeza kasi ya ukuaji wa teknolojia.

Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba ulianzishwa mwaka 1962 ukiasisiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castro.

-Mwisho-






Balozi wa Cuba nchini Tanzania aagwa baada ya kumaliza muda wake



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisoma hotuba wakati wa hafla fupi ya kumuaga Balozi wa Cuba Nchini Tanzani Mhe. Jorge Luis Lopes Tormo iliyofanyika katika Hoteli ya Southern Sun Jijini Dar Salaam

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara Bi. Mindi Kasiga akiongea katika hafla hiyo

Toka kulia ni; Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Comrade Abdulahaman Kinana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Balozi wa Cuba Nchini anayemaliza muda wake Mhe. Jorge Luis Lopes Tormo, Mkurugenzi wa Idara ya Marekani na Ulaya Balozi Joseph Sokoine, na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Taifa Bw.Mlingi E. Mkucha wakifurahia jambo katika hafla hiyo
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara Bi. Mindi Kasiga akifuatilia jambo




Balozi wa Cuba Nchini anayemaliza muda wake Mhe. Jorge Luis Lopes Tormo akiongea katika hafla hiyo

Picha ya pamoja

Tuesday, January 10, 2017

Waziri Mahiga amuaga Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akijadili jambo na mgeni wake Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nyerere Jijini Dar es Salaam, wakati akijiandaa kuondoka baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi nchini. Wa kwanza kulia ni Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Lu Younqing 
Waziri Mahiga akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi


Waziri Mahiga na Waziri Wang Yi wakifurahia jambo wakati wa mazungumzo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe.Wang Yi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nyerere wakati akiondoka nchini mara baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi 

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Balozi Mbelwa Kairuki (katikati kulia) na Makuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara Bi. Mindi Kasiga wakipunga mikono kumuaga Warizi Mhe. Wang wa China. 

Monday, January 9, 2017

Waziri wa Mambo ya Nje wa China awasili nchini kwa ziara ya kikazi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akimpokea Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Wang Yi (wa kwanza kulia) mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juliusi Nyerere. Waziri Wang Yi yupo nchini kwa ziara ya siku moja.
Waziri Mahiga pamoja na Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia wakimtazama Waziri Wang Yi wakati akiteremka kwenye ndege aliyowasili nayo.
Waziri Mahiga akizungumza na mgeni wake Waziri Wang Yi mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kiamataifa wa Julius Nyerere
Balozi Kairuki (katikati), Balozi wa China nchini Tanzania Lu Younqing (wa kwanza kushoto), pamoja na Afisa Mambo ya Nje, Bw. Humphrey Shangarai (wa kwanza kulia) nao wakiwa katika mazungumzo hayo
Sehemu ya ujumbe alioambatana nao Mhe. Waziri Wang Yi

Friday, January 6, 2017

Waziri Mahiga akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Syria nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga(Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Syria nchini Tanzania Mhe. Abdulmonem Annan (kushoto) mwenye makazi yake nchini Kenya. Katika mazungumzo yao yaliyojikita katika kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Syria ambayo ni ya muda mrefu  pamoja na  Balozi Annan kutumia fursa hiyo kujitambulisha rasmi kwa Waziri Mahiga. 
Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo hayo. 
Balozi Annan akimweleza jambo Mhe. Mahiga wakati wa mazungumzo hayo.
Mazungumzo yakiendelea

Thursday, January 5, 2017

Waziri wa Mambo ya Nje wa China kufanya ziara nchini

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Bi. Mindi Kasiga akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu  ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China atakayoifanya hapa nchini tarehe 09 Januari, 2017.Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa  Mikutano wa Kimataifa wa JNICC Jijini Dar es Salaam leo.
Sehemu ya Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini wakati Bi. Mindi Kasiga (hayupo pichani) akiendelea kuzungumza nao.
Sehemu nyingine ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano.
Mkutano na Waandishi wa Habari ukiendelea.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China nchini
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. WANG Yi anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini tarehe 09 Januari 2017. Mhe. Waziri Wang Yi atapokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga.
  
Madhumuni ya  ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri na ya kihistoria baina ya China na Tanzania ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka hamsini tangu kuanzishwa kwake pamoja ‎na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na China.
Wakati wa ziara hiyo Mhe. Wang Yi atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa lengo la kumsalimia. 
Aidha, Mhe. Wang Yi atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Dkt. Mahiga kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na China na ushirikiano wa kimataifa.
Itakumbukwa kwamba mwezi Desemba 2015 kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na China, China iliichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi nne Barani Afrika zitakazowezeshwa kupiga hatua kwenye maendeleo ya viwanda. Kupitia mpango huo inatarajiwa viwanda takriban 200 vitajengwa au kuwekezwa nchini kutoka China kabla ya mwaka 2020.
Mpango huu unaenda sambamba na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/2020 na pia ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kujenga Tanzania ya viwanda. Ni matarajio yetu ni kuwa, Watanzania takriban laki mbili watanufaika na ajira kupitia mpango huu mahsusi wa kuendeleza viwanda.
Mbali na mpango wa uendelezaji wa viwanda, viongozi hawa wawili watazungumzia miradi mingine ya miundombinu ambapo China imeahidi kuisadia Tanzania ikiwa ni pamoja na maboresho makubwa ya Reli ya TAZARA; Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo pamoja na ujenzi wa Reli ya Kati.
Aidha, Mhe. Wang anatarajiwa kuzungumza na Mwenyeji wake kuhusu masuala ya ushirikiano wa kimataifa ikiwa ni pamoja na mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo China inaunga mkono msimamo wa Afrika na wa Tanzania wa kutaka Afrika ipewe viti viwili vya kudumu kwenye Baraza hilo na kura ya turufu. 
Vilevile viongozi hao watazungumzia masuala ya amani na usalama katika eneo la Afrika Mashariki pamoja na eneo la Bahari ya Kusini mwa China.
Mazungumzo hayo yatafuatiwa na Mkutano wa Mawaziri na Vyombo vya Habari (Joint Press Conference) ambapo wataeleza makubaliano waliyofikia kwenye mazungumzo yao.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
05 Januari, 2017



Wednesday, January 4, 2017

Waziri Mahiga akutana kwa mazungumzo na Balozi wa China nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Lu Youqing alipofika Wizarani kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na China.
Sehemu ya Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Mahiga na Balozi Lu (hawapo pichani). Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga, Maafisa Mambo ya Nje, Bw. Emmanuel Luangisa na Bw. Benedict Msuya.
Ujumbe kutoka Ubalozi wa China
Mhe. Dkt. Mahiga akiagana na  Balozi Lu mara baada ya mazungumzo yao.