AAHIDI USHIRIKIANO WENYE TIJA KWA MAENDELEO YA WANANCHI WOTE
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine
Mahiga ameahidi kusimamia uimarishwaji wa uhusiano wa kiuchumi na biashara kati
ya Tanzania na Korea Kusini ili wananchi wa pande zote mbili wapate manufaa.
Waziri
Mahiga ameyasema hayo alipokuwa anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu
ambapo siku ya mwisho aliitumia kikamilifu kukutana na taasisi za umma za
biashara na viwanda, Benki ya Exim ya Korea pamoja na makampuni binafsi
yanayojipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.
Amesema
kuwa miaka 25 ya kwanza ya uhusiano wetu na Jamhuri ya Korea ilijikita kwenye
kuweka misingi imara ya uhusiano wa kidiplomasia ambapo nchi zetu zilikuwa
zinajiimarisha kama mataifa huru. “Sasa ni wakati wa kushamiri kiuchumi tuone
sekta binafsi zinavyoshiriki katika kukuza uchumi, wananchi wa Tanzania waje
kwa wingi nchini Korea kujifunza masuala ya teknolojia, uhandisi na hata
usanifu na ubunifu. Huu ndio uhusiano wenye tija kwa mataifa yetu”. Mheshimiwa
Waziri alisema.
Akizungumza
na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea, Mheshimiwa
Mahiga mbali na kuishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kutoa mikopo na misaada
nchini Tanzania, Waziri Mahiga alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya
Mheshimiwa John Pombe Magufuli sasa imejikita kwenye mapambano dhidi ya rushwa
na ujenzi wa viwanda ili kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu. Kwasasa
Benki hiyo inatekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme na maji mikoa
mbalimbali ya Tanzania ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa
Mahiga alifafanua kuwa ajenda ya Mheshimiwa Magufuli ya viwanda, haiwezi
kukamilika bila kuwa na miundombinu ya msingi kama vile uzalishaji wa umeme wa
kutosha na ukuaji wa sekta ya uchukuzi na mawasiliano ambapo Korea Kusini ni
wabobezi kwenye masuala hayo.
Alitumia
fursa hiyo kumkaribisha Bw. Chang na timu yake kwenda Tanzania kufanya tathmini
ya miradi tunayoshirikiana nao, lakini pia miradi mipya kwenye sekta ya uchukuzi
kama ujenzi wa Standard Railway Gauge “SRG” kutoka Isaka hadi Kigali, n.k. ambayo
ni miradi ya kipaumbele kwa sasa kwa taifa letu.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Chang alisifu utendaji kazi wa Rais John Pombe
Magufuli, na Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania na kusema kuwa utendaji kazi
wa aina hii ni wa kupigiwa mfano barani Afrika, na umekuja wakati muafaka
tunapoingia kwenye hatua nyingine ya uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi zetu
mbili. Aidha aliongeza kuwa, wakati umefika sasa wa kufanya kazi, nay eye yuko
tayari kufanya kazi na Tanzania kwani Serikali yake, imetoa kipaumbele kwa nchi
hii.
Korea
Exim Bank ni taasisi ya Serikali inayosimamia mikopo na misaada ya Jamhuri ya
Korea inayotoa kwa nchi nyingine. Katika kipindi cha miaka minne (tangu 2016
hadi 2020), Korea Kusini kupitia taasisi hiyo, imeongeza mikopo ya maendeleo
kwa bara la Afrika kwa asilimia 20. Uamuzi wa Serikali iliyokuwa madarakani
mwaka 2016 wa kuichagua Tanzania kupokea kiasi kikubwa cha msaada huo kuliko
nchi nyingine ya Afrika, umeendelezwa na Serikali iliyopo sasa madarakani ya
Mheshimiwa Moon Jae-in, Rais wa Jamhuri ya Korea.
Ujumbe
wa Mheshimiwa Augustine Mahiga pia ulikutana na kufanya mazungumzo na Bw.
Judong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara na Viwanda ya Korea (Korea Chamber
of Commerce and Industries KCCI), ambapo Waziri Mahiga aliwasisitiza kuja Dar
es salaam kuangalia fursa zilizopo ili kuwashawishi wanachama wao kutafuta bidhaa
na masoko nchini Tanzania.
Akielezea
umuhimu wa KCCI kuzuru Tanzania na kujifunza soko la biashara, Bw. Edwin
Rutageruka Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE aliyeongozana na ujumbe wa Mheshimiwa
Waziri Mahiga, alisema njia nzuri ya kupata picha halisi ni kupitia Maonesho ya Biashara ya Saba Saba. Hivyo alitumia
fursa hiyo kualika ujumbe wa KCCI kushiriki kwenye maonesho ya 42 yanayotarajiwa
kuanza tarehe 28 Juni – 10 Julai, 2018.
Kabla
ya kuhitimisha ziara yake, Mheshimiwa Mahiga pia alikutana na kufanya
mazungumzo na watendaji wakuu wa makampuni ya DOHWA, ambao wamejikita kwenye
ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya reli n.k. Makampuni mengine ni KORAIL, STX
Engine, KTMI & STX Offshore pamoja na GS E&C, ambao wote wameonesha nia
ya kuwekeza au kufanya biashara nchini Tanzania. Ujumbe mkuu kwa taasisi na
makampuni hayo ulikua ni kupanua fursa za ushirikiano wa biaashara na uwekezaji,
ubadilishanaji wa ujuzi na ujengaji uwezo wa wafanyakazi ambao ndio nguvu kazi
ya taifa letu.
Pamoja
na kuzungumza na makampuni ya umma na sekta binafsi yaliyoorodheshwa hapo juu,
ziara ya Mheshimiwa Augustine Mahiga, ilimuwezesha kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano
la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini ambapo alihutubia mamia
ya wafanyabiashara wa Korea kuhusu utayari wa Tanzania kushirikiana na nchi
hiyo kibiashara.
Mkutano
huo uliopewa kauli mbiu ya “Eplore Tanzania” ulifuatiwa na mikutano midogo
midogo iliyowakutanisha baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzania na Korea Kusini
ili kuangalia kwa ukaribu maeneo ya ushirikiano. Balozi wa Tanzania nchini
Korea Kusini na mwenzake wa Korea Kusini nchini Tanzania wameazimia kuendeleza makongamano
hayo ya kila mwaka ili kuwa na ushirikiano wa karikiano wa karibu wa kibiashara
kwa mataifa hayo mawili kwa maendeleo ya wananchi wote.
Wajumbe
wengine walioongozana na Mheshimiwa Waziri Mahiga nao walipata fursa ya kuhutubia
hadhara hiyo kuhusu Tanzania ambapo Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa
Tanzania Investment Centre alitoa utangulizi kuhusu uwekezaji Tanzania; Kanali
(mstaafu) Joseph Simbakalia, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA alizungumzia maeneo ya kipaumbele
kwenye maeneo maalum ya uwekezaji nchini Tanzania. Naye Bi. Nasriya Nassor, Mkurugenzi
wa Promosheni wa Taasisi ya Uwekezaji Zanzibar alitoa taarifa fupi kuhusu
Zanzibar kama kivutio cha utalii ndani ya Tanzania na eneo linalopendelewa na
watalii wengi duniani.
Jamhuri
ya Korea, kama inavyojulikana rasmi na Umoja wa Mataifa, ni mojawapo ya nchi
zinazofanya vizuri zaidi duniani kiuchumi kwa sasa. Viashiria vya uchumi
vinaonyesha uchumi wa nchi hiyo utaendelea kukua kwa viwango kutokana na jitihada
za dhati za viongozi wa nchi hiyo za kufuta kabisa umaskini kwa wananchi wao. Kwa
sasa wastani wa pato kwa mtu “per capital income” inakadiriwa kuwa zaidi ya US$
34,000, ukilinganisha na US$ 22,670 mwaka 2012. Baada ya vita ya Korea kwenye
miaka ya mwanzo ya 1950, nchi ya Korea Kusini ilikua maskini kuliko nchi nyingi
barani Afrika ikiwemo Tanzania ambapo wastani wa pato kwa mtu ilikua na US$67.
Mheshimiwa
Mahiga anatarajiwa kurejea nyumbani baada yakuhitimisha ziara hiyo aliyosema
italeta faida sio tu kwa wafanyabiashara, ila kwa jamii kwa ujumla. “Nchi
hii ni tajiri sana kiuchumi; lakini utajiri wake mkubwa pia uko kwenye taaluma
ya rasilimali watu, hivyo kwa Tanzania kufanikiwa kufungua ubalozi hapa, sasa
tumefungua milango ya ushirikiano wa karibu, kuliko ilivyokuwa mwanzo.
Tuchangamke tuige mfano wa uchapa kazi wao, na sisi tutaondoka kwenye umasikini”
Waziri Mahiga alisema kwa kumalizia, kabla ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Incheon, uliopo mjini Seoul, Jamhuri ya Korea.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Seoul,
Korea Kusini,
|
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye mazungumzo na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini. Viongozi hao wawili walikutana kwenye ofisi za Benki hiyo Jijini Seoul Korea Kusini wakati wa ziara ya kikazi ya siku tatu ya Waziri Mahiga nchini humo. |
|
Exim Bank Business Meeting 4: Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na ujumbe wake kwenye mazungumzo na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini. Viongozi hao wawili walikutana kwenye ofisi za Benki hiyo Jijini Seoul Korea Kusini. |
|
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na ujumbe wake kwenye mazungumzo na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of Commerce and Industries (KCCI). |
|
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye picha ya pamoja na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of Commerce and Industries (KCCI). Mwingine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Matilda Masuka. |
|
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimkabidhi zawadi ya majani ya chain a kahawa za Tanzania Bw. Choi Jong-won, Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Dong Myeong ya Korea Kusini. |