Friday, February 16, 2018

Mhe. Rais Magufuli awaapisha Mabalozi wa Tanzania nchini Nigeria na Sweden


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akimwapisha Bw. Muhidin Ally Mboweto kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria. Hafla ya uapisho imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Februari, 2018


Balozi Mboweto akisaini mara baada ya kula kiapo cha kuiwakilisha Tanzania nchini Nigeria
Mhe. Rais Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Mboweto
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt.John Pombe Joseph Magufuli akimwapisha Dkt. Wilbroad Peter Slaa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden.
Balozi Slaa akisaini kiapo chake
Mhe. Rais Magufuli alimkabidhi Balozi Slaa vitendea kazi
Balozi Mboweto na Balozi Slaa kwa pamoja wakila kiapo cha Maadili ya Viongozi mbele ya Mhe. Rais Magufuli
Mhe. Rais Magufuli kwa pamoja na Balozi Mboweto na Balozi Slaa (walioketi) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba alipokuwa akitoa nasaha zake kwa Mabalozi hao mara baada ya kuapishwa.
 Wakuu wa Vyombo vya Usalama nchini na wageni wengine waalikwa wakimsikiliza Dkt.Kolimba (hayupo pichani)
Sehemu ya viongozi mbalimbali na wageni waalikwa  wakiwa kwenye hafla ya kuapishwa kwa Balozi Mboweto na Balozi Slaa (hawapo pichani). Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi


Mhe. Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mboweto mara baada ya kumwapisha
Mhe. Rais akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Slaa mara baada ya kumwapisha

 Mhe. Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi walioapishwa na viongozi wengine akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (wa pili kutoka kushoto), Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi (wa pili kulia) na  Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto)
 Mhe. Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi walioapishwa na viongozi wengine akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (wa pili kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto) na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Wizara ya Mambo aya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Thursday, February 15, 2018

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Wabunge wa EALA

                         
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt.Augustine Mahiga akizungumza na Wabunge wa EALA (hawapo pichani).
Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA)  leo wamekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt.Augustine Mahiga Wizarani mjini Dodoma. Wabunge wa EALA wamewasili mjini Dodoma wakiwa katika ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya Jumuiya inayotekelezwa na nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Masharaiki. 

Katika ziara hii Wabunge wanatembelea miradi inayotekelezwa katika ushoroba wa kati (central corridor) sambamba na kubaini changamoto zinazoikabili miradi hiyo na namna inavyorahisha utoaji huduma kwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika mazungumzo yao na Waziri Mahiga, Wabunge wa EALA wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayotokana na makubaliano ya Jumuiya kama vile ujenzi wa mizani za kisasa sambamba  na kupunguza idadi ya mizani hiyo ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, hudumu na watu ndani Jumuiya.

Hadi sasa Tanzania kwa upande wa ushoroba wa kati imefanikiwa kupunguza idadi ya vituo vya mizani kutoka  vituo saba hadi vitatu.

Kwa upande wake Waziri Mahiga, amewapongeza Wabunge wa EALA kwa kuona umuhimu wa kutembelea miradi ya Jumuiya inayotekelezwa na nchi Wanachama ambayo inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Aidha amesema katika ziara hii Wabunge wataweza kubaini changamoto zinazowakabili wananchi, hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kutatua changamoto hizo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao Bungeni.

Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Tanzania Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari walipotembelea ofisi za Wizara mjini Dodoma. Kulia ni  Mhe. Wanjiku Muhia  kutoka Kenya ambaye pia ni kiongozi wa msafara wa ziara hiyo
Mhe. Adam Kimbisa Mbunge wa EALA (Tanzania) akizungumza wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari



Mkutano ukiwa unaendelea

Tanzania yashinda Tuzo, Dubai

Mtukufu Shaikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ya Umoja wa Falme za Kiarabu) (UAE) na Balozi wa Tanzania, UAE, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kulia) wakiwa wameshikilia tuzo ya Teknolojia bora inayoibuka Serikalini (Winner of the Best Government Emerging Technologies Award) ambayo Tanzania imeshinda huko Dubai.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA YASHINDA TUZO YA TEKNOLOJIA KATIKA MKUTANO WA DUNIA WA SERIKALI (WORLD GOVERNMENT SUMMIT 2018)
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshinda Tuzo za Kilele cha Serikali duniani (World Government Summit Awards) katika kundi la Tuzo ya Teknolojia bora inayoibuka Serikalini (Winner of the Best Government Emerging Technologies Award).

Tuzo hiyo ilitolewa na Mtukufu Shaikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nchi, Ofisi ya Rais ya Umoja wa Falme za Kiarabu) (UAE) na kupokelewa na Balozi wa Tanzania, UAE, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk kwa niaba ya Serikali, wakati wa kilele cha Mkutano wa Dunia wa Serikali (World Government Summit) uliohitimishwa jijini Dubai tarehe 13 Februari 2018.

Tuzo hiyo ilitokana na juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Kilimo ya Mikocheni (Mikocheni Agricultural Research Institute kufanikiwa kulipatia ufumbuzi tatizo la maradhi ya zao la muhogo “Cassava Brown Creek Disease,” na “Cassava Mosaic Disease,” kwa kutumia chombo cha kisasa kinachoitwa “Portable DNA Sequencer”.  Maradhi hayo yanasumbua sana zao la muhogo ambalo ni zao muhimu kwa Tanzania na nchi mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa kutumia teknolojia hii mpya wataalamu wanaweza kugundua magonjwa mbalimbali ya zao la muhogo yanayosababishwa na wadudu, virusi, bacteria na fangasi (pathogens) kwa muda wa siku 2 tu kulinganisha na teknolojia ya zamani ambayo huchukua miezi kadhaa na ina gharama kubwa.

Zao la muhogo ni zao muhimu la chakula na biashara linalotegemewa sio tu na  Tanzania bali na nchi nyingine nyingi duniani.  Inakadiriwa kuwa watu wapatao millioni 800 duniani wanategemea zao la muhogo kwa chakula na biashara. Hivyo, teknolojia hii mpya itanufaisha nchi mbalimbali duniani katika kusaidia na kuendeleza zao hilo.

Nchi nyingine zilizopata Tuzo hiyo ni India na Australia.

Wakati huo huo, Watanzania wenye sifa wanahimizwa kuomba nafasi ya kazi iliyotangzwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya mazingira (UNEP). Nafasi inayotakiwa kujazwa ni ya Chief Biodiversity Unit. Maelezo kuhusu nafasi hiyo yanapatikana katika mawasiliano http://careers.un/bw/jobdetail.aspx?id=88749 na siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi ni tarehe 25 Februari 2018.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15 Februari 2018.

Wednesday, February 14, 2018

Wabunge wa EALA wafanya Ziara Nchi za Afrika Mashariki

Wabunge wa EALA wafanya ziara Nchi za Afrika Mashariki
Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wanafanya ziara ya siku 12 kwa ajili ya kupitia na kuangalia maendeleo na changamoto mbalimbali za Mtangamano pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya Mtangamano wa Jumuiya ya  Afrika Mashariki kupitia vyombo vya habari.
Ziara hiyo ilianza tarehe 12- 23 Februari,2018, katika ziara hiyo waheshimiwa Wabunge wamegawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza linafanya ziara katika ukanda wa kati ( Cetral Corridor) , ziara hii itahusisha Zanzibar na Mikoa ya Dar es salaam, Kilimanjaro, Pwani, Arusha, Dodoma, Shinyanga na Kagera,  kundi la pili watatembelea ukanda wa Kaskazini   ( North Corridor) ziara hiyo itaanzia Kenya, Uganda na kumalizikia Rwanda ambapo ndipo wanapotarajia kukutana kwa kwa ajili ya kikao cha  wiki mbili kwa ajili ya majumuisho ya ziara.
Waheshimiwa Wabunge wanaotemebelea Ukanda wa Kati walianzia safari yao Zanzibar ambapo walifanya ziara katika Bandari ya Zanzibar na pia kufanya mazungumzo na Uongozi wa Taasisi ya Kiswahili Kamisheni. Aidha, wakiwa Dar es salaam walipata fursa ya kutembelea Bandari ya Dar es salaam na kukutana na viongozi wa Bandari pamoja na wadau mbalimbali wanaotumia bandari. Akiongea katika mkutano huo Kaimu Meneja wa Bandari Bw. Feddy Liundi, alisema hadi sasa kuna mafanikio makubwa sana katika Bandari ya Dar es Salaam kwani bandari hiyo inahudumia zaidi ya nchi nane na kati ya hizo Rwanda na Malawi wanaongoza kwa matumizi ya bandari ya Dar es salaam.
Kwa upande wao Waheshiwa walisifia maboresho ya bandari na kusema ndio yamechangia bandari hii kuwa kinara na kivutio kwa wasafirishaji wa mizigo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Waheshimiwa Wabunge pia walipata nafasi ya kutembelea eneo la mradi wa maboresho ya bandari ya Dar es salaam wa Dar es salaam Maritime Gateaway Project (PMGP) pamoja na kitengo cha Kontena cha TICTS.
Waheshimiwa wabunge walipongeza uongozi wa bandari kwa maboresho makubwa yaliyofanyika na kuahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizoainishwa ambazo ni za Kimtangamano. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 21 kutoka nchi sita (6) za Jumuiya Ya Afrika Mashariki wanashiriki katika ziara hii kwa upande wa Ukanda wa kati(Cetral corridol).

========================================================================


 Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki ( EALA) wakiwa katika Mkutano na Uongozi wa Bandari ya Dar es salaam, kutoka kushoto ni Mhe.Maryam Ussi (Tanzania), Mhe. Wanjiku Muhia (Kenya) (ambaye pia ni kiongozi wa Msafara katika ziara hii) na wa mwisho kulia ni Kaimu Meneja wa bandariBw. Freddy Liundi, wakiwa katika Mkutano. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bandari, tarehe 13 Februari,2018.

 Mhe. Josephine Lemoyan (Tanzania) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya mkutano, wanaofuatilia ni Mhe. Wanjiku (kushoto), na Mhe. Musamali Paul Mwasa (Uganda)

    Waheshimiwa Wabunge na wadau wengine wakiwa katika Mkutano huo

 Wadau mbalimbali wakifuatilia Mkutano huo

Waheshimiwa Wabunge, wafanyakazi wa bandari pamoja na wadau wengine wakiwa katika picha ya pamoja.

Tuesday, February 13, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI -Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa Baraza la Wakimbizi Duniani


Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na waandishi wa habari kuhusu dhamira ya kuanzishwa kwa Baraza la Wakimbizi Duniani ambalo yeye ni Mwenyekiti Mwenza. Mweingine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga.



Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa Baraza la Wakimbizi Duniani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia Tanzania kutokana na mchango mkubwa wa kuwahudumia wakimbizi ambao imekuwa ikiutoa kabla na baada ya uhuru, licha ya uchumi mdogo ilio nao. 

Waziri Mahiga ametoa wito huo leo Jijini Dar Es Salaam katika kikao cha Baraza la Wakimbizi Duniani (World Refugees Council-WRF) kinachofanyika kwa siku mbili kuanzia jana kwenye Hoteli ya Hyatt Regecy, Kilimanjaro.

Waziri Mahiga alieleza kuwa Tanzania ilipokea wakimbizi kutoka Poland wakati wa vita ya pili ya dunia na mwaka 1959 ilipokea wakimbizi kutoka nchi ya Rwanda. Aidha, baada ya uhuru, Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi mara kwa mara na wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Tanzania ilipokea wakimbizi wengi zaidi duniani.

Aliendelea kueleza kuwa athari zinazotokana na kupokea wakimbizi wengi ni nyingi na kubwa hivyo, ni jukumu la Jumuiya ya Kimataifa kuzisaidia nchi zenye wakimbizi wengi, hususan zile zenya uchumi mdogo.

Katika kikao hicho, Waziri Mahiga alitoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa Serikali ya Tanzania kujitoa katika mpango wa kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo la wakimbizi duniani (Comprehensive Refugees Response Framework – CRRF). Alisema katika mpango huo wa CRRF, Serikali imesikitishwa na mapendekezo ya mpango huo ya kuitaka Tanzania ikope fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi na kugharamia ukarabati wa miundombinu iliyoharibika. 

Halikadhalika, CRRF inapendekeza kuwepo na utaratibu wa kuwapa uraia, ajira na ardhi wakimbizi wanaoingia nchini ili waweze kuwa huru na kujitegemea.

Alibainisha kuwa Serikali ilishatoa uraia kwa wakimbizi zaidi ya laki moja na nusu. Jumuiya ya kimataifa iliahidi kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia makazi na huduma nyingine kwa wakimbizi hao. Hata hivyo, Jumuiya ya Kimataifa haijatekeleza ahadi hiyo, badala yake inaitaka Serikali ichukue mkopo wenye riba kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi. 

“Misitu, ardhi, mazingira na miundombimu mingine inaharibika kwa sababu ya wakimbizi, halafu tuchukue mkopo na kulipa deni kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi, nadhani sio utaratibu mzuri” Dkt. Mahiga alilalamika.

Dkt. Mahiga alieleza kuwa amewasilisha ujumbe wa Serikali kwenye Baraza hilo ili lifikishe kilio cha Tanzania katika Jumuiya ya Kimataifa kwa matumaini kuwa wao wanasikilizwa zaidi. 

Kwa upande wake, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, alitoa maelezo kuhusu dhamira ya kuanzishwa kwa WRC. Alisema WRC ilianzishwa mwaka 2017 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Canada na Taasisi isiyo ya kiserikali ya nchi hiyo. Lengo la chombo hicho ni kuangalia sababu zinazopelekea wakimbizi kuongezeka,  matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na kutoa maoni ya namna ya kutatua tatizo la wakimbizi duniani.

Baraza hilo linaongozwa na jopo la watu wanne wenye uzoefu wa masuala ya wakimbizi duniani ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Canada ambaye ni Mwenyekiti, Mhe. Lyord Axworthy, Mwenyekiti Mwenza ni Rais wa zamani wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti ni Mwanadiplomasia wa zamani wa Canada, Mhe. Paul Heinbecker na Mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Pakistan ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza, Mhe. Hina Jilani. 

Baraza lilifanya kikao cha kwanza Geneva, Uswisi mwezi Juni 2017 na baadaye kutembelea nchi za Jordan na Ujerumani. Nchi hizo zimetembelewa kwa sababu Jordan ndio nchi inayopokea wakimbizi wengi kwa sasa duniani na Ujerumani kutokana na kuruhusu kupokea wakimbizi kulisababisha Serikali iliyopo madarakani kupata upinzani mkali katika uchaguzi uliopita.
Kikao cha pili kinafanyika Afrika na Tanzania imechaguliwa kutokana na uzoefu wake katika masuala ya wakimbizi. Aidha, kikao kijacho kitafanyika Bara la Asia katika nchi ya Thailand na kitafuatiwa na kikao kitakachofanyika Bara la Amerika Kusini. 

Katika kikao kinachoendelea nchini, Nchi mbalimbali za Afrika zimealikwa zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya ambazo zieleza uzoefu wao kuhusu matatizo na sababu za kutoa wakimbizi.

Baraza hilo linatarajiwa kukamilisha ripoti yake mwaka 2018 na kuiwasilisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya utekelezaji.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 13 Februari 2018




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akiongea na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa Tanzania kujitoa katika Mpango wa kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo la wakimbizi duniani.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akiongea katika kikao cha Baraza la Wakimbizi Duniani kinachofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - Fursa za Ufadhili wa Masomo kwa Watanzania na Tuzo ya Utalii kwa Tanzania


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika MAshariki Profesa Adolph Mkenda 



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

FURSA ZA UFADHILI WA MASOMO KWA WATANZANIA NA TUZO YA UTALII KWA TANZANIA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mapema mwezi Februari imepokea fursa za ufadhili wa masomo ya muda mfupi na muda mrefu katika kada mbalimbali kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea, Serikali ya Misri na Malaysia.

Kwa upande wa ufadhili wa masomo ya muda mfupi, Serikali ya Korea imetoa nafasi nne (4) kwa ajili ya Watumishi wa Umma katika Sekta ya Afya. Nafasi hizo ni kwa ajili ya Mafunzo ya Uganga (Clinical Experts) nafasi mbili (2), Utawala katika masuala ya Afya (Health Administrator)  nafasi moja (1) na Afisa Mwandamizi katika masuala ya Afya nafasi moja (1). 

Mafunzo hayo ambayo yanafadhiliwa na Korea Foundation for International Healthcare yapo chini ya program ya “Dr. Lee Jong-wook fellowship program” kwa mwaka 2018. Maombi ya nafasi hizo yaelekezwe Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambao ni waratibu wakuu katika sekta ya afya.

Kutoka Serikali ya Misri, Wizara imepokea nafasi mbili (2) za mafunzo ya muda mfupi kwa Watangazaji kutoka nchi za Afrika “19th Basic Training Course for the African Broadcasters”. Mafunzo yatafanyika Misri kuanzia tarehe 25 Februari, 2018 hadi 25 Machi, 2018. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Halikadhalika, Wizara imepokea nafasi mbili (2) za Mafunzo ya muda mfupi katika Teknolojia ya Uchakataji Madini (Minerals Processing Technology) yatakayofanyika nchini Misri kuanzia tarehe 18 hadi 29 Machi, 2018. Mratibu wa Mafunzo haya ni Wizara ya Madini.

Kutoka nchini Malaysia, Wizara imepokea mwaliko wa nafasi mbili (2) za kushiriki Mashindano ya 60 ya Kimataifa ya Kuhifadhi Quran ya 1439H/2018 yatakayofanyika Kuala Lumpur, Malaysia kuanzia tarehe 07 hadi 12 Mei, 2018. Mashindano hayo yanaratibiwa na Ofisi ya Mufti, zanzibar na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA).

Kuhusu mafunzo ya muda mrefu, Wizara imepokea  fursa za ufadhili wa masomo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu katika kozi mbalimbali kwa ajili ya Watanzania wote kutoka Jamhuri ya Korea.

Fursa hizo za masomo ambazo zinafadhiliwa na Wizara ya Elimu ya Korea zinapatikana kupitia tovuti ya    “2018 Global Korea Scholarship” ambayo ni http://www.studyinkorea.go.kr. Tovuti hii imeainisha taarifa na taratibu zote za namna ya kuomba. Tarehe ya mwisho ya kutuma maombi ni tarehe 15 Machi, 2018. Aidha,  nakala ngumu ya fomu za maombi ziwasilishwe Ofisi za Ubalozi wa Korea nchini mara baada ya kukamilisha maombi ya mtandaoni (online application).  Waombaji wanatakiwa kuwasilisha maombi yao mapema kabla ya tarehe tajwa hapo juu. Mratibu mkuu wa fursa hizi ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Katika hatua nyingine, Wizara imepokea nafasi tano (5) za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya kwanza na nafasi mbili (2) za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Helwan cha nchini Misri. Mafunzo ya Shahada ya kwanza yanatolewa kwenye fani za Utalii na masuala ya Hoteli, Biashara, Uhandisi, Kompyuta na Teknolojia. Aidha, ufadhili masomo ya shahada ya uzamili unatolewa kwenye fani za Sanaa na Muziki (Fine Arts and Music).   

Mafunzo  hayo yatafanyika kwa mwaka wa masomo 2018/2019. Maombi yote yaelekezwe Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania ambao ndio waratibu wakuu.

Wizara inatumia fursa hii kuwahimiza wale wote watakaoomba nafasi hizo kuhakikisha wanatimiza vigezo na masharti ya maombi hayo ili mamlaka zinazohusika na uchambuzi wa ubora ziweze kupata Watanzania wenye sifa kwa ajili ya kuwajengea uwezo na kuliletea taifa maendeleo.

Wizara inauhakikishia umma wa Watanzania kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha inasimamia upatikanaji wa fursa za ufadhili wa masomo na ajira mbalimbali zinazowasilishwa na nchi rafiki, Mashirika ya Kikanda na Kimataifa na kuhakikisha zinawafikia Watanzania ili wanufaike na fursa hizo. 

Wakati huohuo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea Tuzo kutoka Serikali ya Urusi kama mshindi wa pili wa mashindano ya  dunia katika kigezo cha nchi nzuri zaidi kutembelea duniani. 

Tuzo hizi ambazo hutolewa na National Geographic Traveler Awards ni tuzo mashuhuri zaidi nchini Urusi katika sekta ya uchukuzi na utalii. Aidha, kupitia Jarida Mtandao la Utalii la nchini Urusi, wasomaji 270,000 walipata nafasi ya kupiga kura na matokeo kutangazwa tarehe 30 Novemba, 2017.  

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka 6 ambapo wapiga kura nchini Urusi wanaichagua Tanzania kama nchi nzuri zaidi kutembelea. Mwaka 2011 Zanzibar ilipokea tuzo ya aina hii kwa nchi za Afrika.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
13 Februari, 2018