Thursday, February 15, 2018

Tanzania yashinda Tuzo, Dubai

Mtukufu Shaikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ya Umoja wa Falme za Kiarabu) (UAE) na Balozi wa Tanzania, UAE, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kulia) wakiwa wameshikilia tuzo ya Teknolojia bora inayoibuka Serikalini (Winner of the Best Government Emerging Technologies Award) ambayo Tanzania imeshinda huko Dubai.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA YASHINDA TUZO YA TEKNOLOJIA KATIKA MKUTANO WA DUNIA WA SERIKALI (WORLD GOVERNMENT SUMMIT 2018)
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshinda Tuzo za Kilele cha Serikali duniani (World Government Summit Awards) katika kundi la Tuzo ya Teknolojia bora inayoibuka Serikalini (Winner of the Best Government Emerging Technologies Award).

Tuzo hiyo ilitolewa na Mtukufu Shaikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nchi, Ofisi ya Rais ya Umoja wa Falme za Kiarabu) (UAE) na kupokelewa na Balozi wa Tanzania, UAE, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk kwa niaba ya Serikali, wakati wa kilele cha Mkutano wa Dunia wa Serikali (World Government Summit) uliohitimishwa jijini Dubai tarehe 13 Februari 2018.

Tuzo hiyo ilitokana na juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Kilimo ya Mikocheni (Mikocheni Agricultural Research Institute kufanikiwa kulipatia ufumbuzi tatizo la maradhi ya zao la muhogo “Cassava Brown Creek Disease,” na “Cassava Mosaic Disease,” kwa kutumia chombo cha kisasa kinachoitwa “Portable DNA Sequencer”.  Maradhi hayo yanasumbua sana zao la muhogo ambalo ni zao muhimu kwa Tanzania na nchi mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa kutumia teknolojia hii mpya wataalamu wanaweza kugundua magonjwa mbalimbali ya zao la muhogo yanayosababishwa na wadudu, virusi, bacteria na fangasi (pathogens) kwa muda wa siku 2 tu kulinganisha na teknolojia ya zamani ambayo huchukua miezi kadhaa na ina gharama kubwa.

Zao la muhogo ni zao muhimu la chakula na biashara linalotegemewa sio tu na  Tanzania bali na nchi nyingine nyingi duniani.  Inakadiriwa kuwa watu wapatao millioni 800 duniani wanategemea zao la muhogo kwa chakula na biashara. Hivyo, teknolojia hii mpya itanufaisha nchi mbalimbali duniani katika kusaidia na kuendeleza zao hilo.

Nchi nyingine zilizopata Tuzo hiyo ni India na Australia.

Wakati huo huo, Watanzania wenye sifa wanahimizwa kuomba nafasi ya kazi iliyotangzwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya mazingira (UNEP). Nafasi inayotakiwa kujazwa ni ya Chief Biodiversity Unit. Maelezo kuhusu nafasi hiyo yanapatikana katika mawasiliano http://careers.un/bw/jobdetail.aspx?id=88749 na siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi ni tarehe 25 Februari 2018.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15 Februari 2018.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.