Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika MAshariki Profesa Adolph Mkenda |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
FURSA
ZA UFADHILI WA MASOMO KWA WATANZANIA NA TUZO YA UTALII KWA TANZANIA
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki mapema mwezi Februari imepokea fursa za
ufadhili wa masomo ya muda mfupi na muda mrefu katika kada mbalimbali kutoka
Serikali ya Jamhuri ya Korea, Serikali ya Misri na Malaysia.
Kwa upande wa ufadhili wa
masomo ya muda mfupi, Serikali ya Korea imetoa nafasi nne (4) kwa ajili ya
Watumishi wa Umma katika Sekta ya Afya. Nafasi hizo ni kwa ajili ya Mafunzo ya
Uganga (Clinical Experts) nafasi mbili (2), Utawala katika masuala ya Afya
(Health Administrator) nafasi moja (1)
na Afisa Mwandamizi katika masuala ya Afya nafasi moja (1).
Mafunzo hayo ambayo yanafadhiliwa
na Korea Foundation for International
Healthcare yapo chini ya program ya “Dr. Lee Jong-wook fellowship program”
kwa mwaka 2018. Maombi ya nafasi hizo yaelekezwe Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambao ni waratibu wakuu katika sekta ya afya.
Kutoka Serikali ya Misri,
Wizara imepokea nafasi mbili (2) za mafunzo ya muda mfupi kwa Watangazaji
kutoka nchi za Afrika “19th Basic Training Course for the African
Broadcasters”. Mafunzo yatafanyika Misri kuanzia tarehe 25 Februari, 2018 hadi
25 Machi, 2018. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo.
Halikadhalika, Wizara
imepokea nafasi mbili (2) za Mafunzo ya muda mfupi katika Teknolojia ya
Uchakataji Madini (Minerals Processing Technology) yatakayofanyika nchini Misri
kuanzia tarehe 18 hadi 29 Machi, 2018. Mratibu wa Mafunzo haya ni Wizara ya
Madini.
Kutoka nchini Malaysia,
Wizara imepokea mwaliko wa nafasi mbili (2) za kushiriki Mashindano ya 60 ya
Kimataifa ya Kuhifadhi Quran ya 1439H/2018 yatakayofanyika Kuala Lumpur,
Malaysia kuanzia tarehe 07 hadi 12 Mei, 2018. Mashindano hayo yanaratibiwa na
Ofisi ya Mufti, zanzibar na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA).
Kuhusu mafunzo ya muda
mrefu, Wizara imepokea fursa za ufadhili
wa masomo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu katika kozi mbalimbali kwa
ajili ya Watanzania wote kutoka Jamhuri ya Korea.
Fursa hizo za masomo
ambazo zinafadhiliwa na Wizara ya Elimu ya Korea zinapatikana kupitia tovuti
ya “2018
Global Korea Scholarship” ambayo ni http://www.studyinkorea.go.kr.
Tovuti hii imeainisha taarifa na taratibu zote za namna ya kuomba. Tarehe ya mwisho
ya kutuma maombi ni tarehe 15 Machi, 2018. Aidha, nakala ngumu ya fomu za maombi ziwasilishwe
Ofisi za Ubalozi wa Korea nchini mara baada ya kukamilisha maombi ya mtandaoni
(online application). Waombaji
wanatakiwa kuwasilisha maombi yao mapema kabla ya tarehe tajwa hapo juu.
Mratibu mkuu wa fursa hizi ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Katika hatua nyingine,
Wizara imepokea nafasi tano (5) za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya
kwanza na nafasi mbili (2) za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya
uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Helwan cha nchini Misri. Mafunzo ya Shahada ya
kwanza yanatolewa kwenye fani za Utalii na masuala ya Hoteli, Biashara,
Uhandisi, Kompyuta na Teknolojia. Aidha, ufadhili masomo ya shahada ya uzamili
unatolewa kwenye fani za Sanaa na Muziki (Fine Arts and Music).
Mafunzo
hayo yatafanyika kwa mwaka wa masomo 2018/2019. Maombi yote yaelekezwe
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania ambao ndio waratibu wakuu.
Wizara inatumia fursa hii
kuwahimiza wale wote watakaoomba nafasi hizo kuhakikisha wanatimiza vigezo na
masharti ya maombi hayo ili mamlaka zinazohusika na uchambuzi wa ubora ziweze
kupata Watanzania wenye sifa kwa ajili ya kuwajengea uwezo na kuliletea taifa
maendeleo.
Wizara inauhakikishia umma
wa Watanzania kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika
kuhakikisha inasimamia upatikanaji wa fursa za ufadhili wa masomo na ajira
mbalimbali zinazowasilishwa na nchi rafiki, Mashirika ya Kikanda na Kimataifa
na kuhakikisha zinawafikia Watanzania ili wanufaike na fursa hizo.
Wakati
huohuo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea
Tuzo kutoka Serikali ya Urusi kama mshindi wa pili wa mashindano ya dunia katika kigezo cha nchi nzuri zaidi
kutembelea duniani.
Tuzo hizi ambazo hutolewa
na National Geographic Traveler Awards
ni tuzo mashuhuri zaidi nchini Urusi katika sekta ya uchukuzi na utalii. Aidha,
kupitia Jarida Mtandao la Utalii la nchini Urusi, wasomaji 270,000 walipata
nafasi ya kupiga kura na matokeo kutangazwa tarehe 30 Novemba, 2017.
Hii ni mara ya pili katika
kipindi cha miaka 6 ambapo wapiga kura nchini Urusi wanaichagua Tanzania kama
nchi nzuri zaidi kutembelea. Mwaka 2011 Zanzibar ilipokea tuzo ya aina hii kwa
nchi za Afrika.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje Na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
13 Februari, 2018
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.