Monday, September 24, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUTOKA MATAIFA MBALIMBALI NA BALOZI ZA TANZANIA



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUTOKA MATAIFA MBALIMBALI NA BALOZI ZA TANZANIA NJE YA NCHI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kupokea salamu za rambirambi kutoka kwa marais, mawaziri wakuu wa mataifa mbalimbali duniani kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere iliyotokea kwenye Ziwa Victoria, Mkoani Mwanza tarehe 20 Septemba, 2018 na  kusababisha vifo, majeruhi na upotevu wa mali.

Baadhi ya salamu zilizopokelewa ni pamoja na kutoka kwa Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, Rais wa Urusi, Mheshimiwa Vladmir Putin, Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Ujerumani, Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier, Rais wa Saharawi, Mheshimiwa Brahim Ghali, Mtawala wa Kuwait, Mtukufu Sheikh Sabah Al-Ahmad al Jaber Al-Sabah, Baba Mtakatifu, Papa Francis, Rais wa Italia, Mheshimiwa Sergio Mattarella, Rais wa Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Finland, Mheshimiwa Sauli Niinistö, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mheshimiwa Joseph Kabila Kabange na Rais wa Jamhuri ya Sudan, Mheshimiwa Omar Hassan Ahmed Al-Bashir.  

Viongozi wengine ni Waziri Mkuu wa Israel, Mheshimiwa Benjamin Netanyahu, na Waziri Mkuu wa Sweden, Mheshimiwa Stefan Löfven.

Viongozi hao wameeleza kusikitishwa kwao na taarifa za vifo vilivyosababishwa na  ajali hiyo na kuwatakia majeruhi kupona haraka.

Sehemu ya nukuu za salamu hizo zinasema “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nilipokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyosababisha vifo vya watu wengi, majeruhi na wengine kutojulikana walipo. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Kenya naomba upokee na kufikisha salamu zetu za rambirambi kwa wafiwa na wananchi wote wa Tanzania kufuatia ajali hiyo na tunawaombea majeruhi wote wapone haraka” ni sehemu ya nukuu ya salamu kutoka kwa Mheshimiwa Rais Kenyatta
“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nilishtushwa na taarifa za ajali hiyo mbaya iliyotokea Mkoani Mwanza. Kwa niaba ya Serikali ya China, wananchi na mimi binafsi natoa pole kwa wafiwa wote na majeruhi” inasema sehemu ya salamu kutoka kwa Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping.
Naye Rais wa Urusi, Mheshimiwa Putin amesema “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, tafadhali naomba upokee salamu zangu za rambirambi kufuatia ajali iliyotokea. Naomba salamu hizi ziwafikie wafiwa wote na ninawaombea majeruhi wapone haraka”

Aidha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea salamu za rambirambi kutoka kwa balozi mbalimbali zinazowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini, ikiwemo ubalozi wa Marekani, ubalozi wa Ufaransa, ubalozi wa Sudan Kusini, Ubalozi wa Falme za Kiarabu (UAE), Serikali ya Brazil, Ubalozi wa Cuba, ubalozi wa Nigeria na salamu kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Kimataifa nchini.

Wakati huohuo, Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka kwa mabalozi wanaowakilisha Tanzania kwenye nchi mbalimbali. Salamu zilizopokelewa zinatoka kwa mabalozi wote wa Tanzania  katika nchi za Qatar, Ufaransa, Uingereza, Uholanzi, Afrika Kusini, Sweden, Nigeria, Burundi, Uganda, Kenya, Ubelgiji, Zambia, Msumbiji, China, Japan, Brazil, Comoro, Algeria, Sudan,  Canada,

Kadhalika tumepokea salamu kutoka kwenye balozi zetu zilizoko Marekani, Uturuki, Rwanda, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Kuwait, Saudi Arabia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe, Malawi, Uswisi, India, Italia, Jamhuri ya Korea, Urusi, Israel, Ethiopia, Ujerumani, Oman na Malaysia.

Baadhi ya nukuu ya salamu za rambirambi za mabalozi hao zinasomeka kama ifuatavyo “Inna Lillah Wainna Illah Rajiuon.  Kwa  niaba  ya  Ubalozi  Abuja  na  Watanzania  waliopo  katika  eneo  letu  la  uwakilishi,  tunatoa  pole  kwa  Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  familia  na  Watanzania  kwa  ujumla  kwa  msiba  mkubwa  uliotufika.  Mwenyezi  Mungu  atupe  subira  na  faraja  katika  kipindi  hiki  cha  majonzi  na  aziweke  roho  za  marehemu  mahali  pema  na  majeruhi  wapone  haraka, Amin  Amin,”  ni kauli yake Mheshimiwa Muhidin Ally Mboweto, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mheshimiwa Dkt. Wilbroad Slaa anasema “kwa niaba ya wenzangu katika kituo cha Stockholm tunatoa pole za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu na familia zote zilizoguswa na msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na kuwatia nguvu na ujasiri ndugu wote walioguswa na msiba huu”.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Balozi Modest Mero alisema haya; “Ubalozi wa New York tunatoa pole kwa ajali mbaya ya Meli ya MV Nyerere iliyopelekea wengi kupoteza maisha na wengi kuumia.  Tunawaombea marehemu pumziko la milele na wote waliojeruhiwa wapone haraka.”

Balozi wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki alieleza masikitiko yake kwa kusema kuwa “nasi huku Beijing tunaungana na wenzetu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Watanzania na wanafamilia walioguswa msiba huu mzito. Mwenyezi Mungu awape nguvu na awajalie moyo wa subira wakati wote mnaposhughulika na msiba huo.

Japan na diaspora yetu tunatoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote kwa msiba huu uliotokana na kuzama kwa kivuko. Mungu atupe nguvu wote tuliobaki na awape pumziko la amani wenzetu waliotutangulia. Kwa majeruhi tunawaombea wapone haraka na wavumilie mstuko huu mkubwa katika maisha yao. Marehemu wapumzike kwa amani”. Hizi ni salamu kutoka kwa Mheshimiwa Mathias Chikawe, balozi wa Tanzania nchini Japan.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Abu Dhabi alisema haya; “Ubalozi wa Tanzania Abu Dhabi, tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali ya MV Nyerere.Kwa niaba ya watumishi wote wa Ubalozi, tunatoa mkono wa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wenzetu wote kwa msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu awajaalie marehemu wapumzike mahali pema na awajaalie majeruhi kupona mapema. Amin”.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Dkt. Asha-Rose Migiro akieleza kuguswa na ajali hiyo alitoa kauli hii “Ubalozi wa Tanzania London unajumuika na Watanzania wenzetu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, familia na ndugu wa wale wote waliopatwa na msiba kutokana na ajali hii. Tunawaombea majeruhi wapone haraka na warejee katika shughuli zao za kujikimu na kulijenga taifa letu”.

Kwa upande mwingine, Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka Baraza la Diaspora wa Tanzania ulimwenguni kote (TDC Global) ambao wameeleza masikitiko makubwa kufuatia ajali hiyo mbaya. Sehemu ya ujumbe wao unasomeka kama ifuatavyo; “TDC Global, kwa masikitiko makubwa, inatoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wote, ndugu, jamaa na marafiki kwa vifo vilivyotokana na ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere kinachofanya safari zake kati ya visiwa vya Bugorora na Ukara katika Ziwa Victoria. Kama TDC Global, tunaungana na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huu mzito kwa taifa letu. Pia tunatoa pole kwa majeruhi wote na kuwaombea wapone haraka”.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dodoma.
24 Septemba, 2018


Saturday, September 22, 2018

Ubalozi wa Tanzania nchini India wahitimisha maonesho maalum ya utalii

Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania, Bibi Devotha Mdachi akizungumza wakati wa kuhitimisha maonesho maalum ya utalii yaliyofanyika  nchini India kwenye baadhi ya miji mikubwa ya New Delhi, Mumbai, na Ahmedabad. Maonesho hayo ambayo yalifanyika kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini India yalilenga kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ikiwemo Hifadhi za Taifa za Wanyama kama Ngorongoro, Serengeti, fukwe zilizopo Zanzibar na Mlima Kilimanjaro. Pia wakati wa maonesho hayo Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Baraka Luvanda alitumia fursa hiyo kutangaza kuanza rasmi kwa safari za Shirika la Ndege la Tanzania mjini Mumbai mwezi Novemba 2018. 
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akizungumza na mmoja wa wadau  kutoka India aliyeshiriki maonesho hayo maalum ya utalii

Afisa kutoka Tanzania akitoa ufafanuzi kwa wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ya India walioshiriki maonesho
ya maalum ya utalii yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini humo kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania

Wadau mbalimbali wa sekta ya utalii wakijadili masuala mbalimbali kuhusu sekta hiyo na kubadilishana uzoefu 

Mtaalam kutoka Tanzania akitoa ufafanuzi kwa mdau wa sekta ya utalii wa nchini India

Balozi Luvanda akiwa na mmoja wa wadau walioshiriki maonesho hayo


Friday, September 21, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Mjukuu wa  Malkia wa Uingereza nchini, (Prince William)

Mjukuu wa Malkia wa Uingereza “Prince” William anatarajiwa kufanya ziara nchini kuanzia tarehe 26 hadi 29 Septemba 2018.  Ziara hiyo inakuja kufuatia maombi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alipofanya naye mazungumzo wakati wa mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Uingereza mwezi Aprili 2018.
“Prince” William atakapowasili nchini pamoja na mambo mengine atafanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Aidha, atatembelea kikosi cha Maji cha Jeshi la Polisi; Bandari ya Dar es Salaam; Jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House); Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo mkoani Tanga na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mweka kilichopo mkoani Kilimanjaro.
“Prince” William ni mmoja wa wanaharakati duniani wanaopinga biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori na Uingereza imekuwa ikisifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na vitendo vya ujangili.
“Prince” William ataondoka nchini tarehe 29 Septemba 2018 kuelekea nchini Kenya.

                                                        -Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 21 Septemba 2018

Thursday, September 20, 2018

Maonesho Maalum ya Utalii yaendelea nchini India

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki maonesho maalum  ya kutangaza vivutio vya utalii na kuanza kwa safari za Air Tanzania nchini India. Maonesho hayo yalifanyika mjini Gujarat. Ubalozi huo kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) umeandaa maonesho maalum kwenye miji mbalimbali ya India huku tayari maonesho ya aina hiyo yakiwa yamefanyika mjini New Delhi tarehe 17 Septemba, 2018. Safari za shirika la ndege la Tanzania kupitia ndege yake mpya ya Dreamliner zitaanza safri mjini Mumbai mwezi Novemba, 2018 kwa lengo la kurahisisha usafiri kwa watalii, wafanyabiashara na wanafunzi kutoka India kuja nchini.

Monday, September 17, 2018

Ubalozi wa Tanzania nchini India watangaza kuanza rasmi kwa safari za Air Tanzania nchini humo

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akizungumza wakati wa maonesho maalum ya utalii yaliyofanyika  katika Hoteli ya Roseate, Aerocity jijini New Delhi, India tarehe 17 Septemba, 2018. Mhe. Balozi Luvanda pamoja na mambo mengine alitumia fursa hiyo kutangaza kuanza rasmi kwa safari za Shirika la Ndege la Tanzania mjini Mumbai mwezi Novemba 2018. maonesho hayo yatafanyika kwenye miji mingine miwili ya India ambayo ni Ahmedabad na Mumbai.
Mhe. Balozi Luvanda akitangaza rasmi kuanza kwa safari za Shirika la Ndege la Tanzania nchini India huku  picha ya Ndege ya Shirika hilo aina ya Dreamliner ikionekana. Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii nchini (TTB), Bi. Devotha  Mdachi ambaye yupo nchini India kushiriki maonesho hayo aliyoshiriki kuandaa anaonekana akichukua kumbukumbu ya tukio hilo
Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi Devotha Mdachi naye akizungumza wakati wa maonesho yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini India kwa kushirikiana na Bodi hiyo.

===============================================================================

Ubalozi wa Tanzania nchini India kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania na Shirika la Ndege Tanzania umeandaa Maonesho Maalum ya Utalii na kutambulisha rasmi kuanza kwa safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania zitakazofanyika Mjini Mumbai nchini humo kuanzia mwezi Novemba, 2018.


Maonesho hayo ambayo yatafanyika kwenye miji mikubwa mitatau ya India yaani New Delhi, Ahmedabad na Mumbai yanalenga kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nnchini.

Akizungumza wakati wa maonesho hayo yaliyofanyika katika Hoteli ya Roseate, Aerocity jijini New Delhi, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alisema kuwa anaona fahari kubwa kushiriki maonesho hayo muhimu kwa Tanzania na India na alitumia fursa hiyo kutangaza rasmi kuanza wa safari za kwanza za ndege ya shirika la ndege la Tanzania mjini Mumbai. 

Balozi Luvanda alisema kuwa safari za ndege hiyo nchini India ni fahari kubwa kwa Tanzania kutokana na ukweli kwamba nchi hizi mbili zina mahusiano ya kihistoria kwani mbali na kuunganishwa na Bahari ya Hindi, Tanzania na India ni marafiki na zimekuwa zikishirikiana katika Nyanja mbalimbali zikiwemo biashara, utamaduni na mawasiliano ya mtu mmoja mmoja.

Mhe. Balozi Luvanda alisisitiza kuwa, safari za ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania nchini India hususan katika mji wa Mumbai zitaimarisha sekta ya utalii nchini kwa kuongeza idadai ya watalii kutoka nchini humo ambao kwa sasa takribani watalii 40,000 kutoka nchini humo wanatembelea Tanzania kwa mwaka. Pia zitarahisha safari za wanafunzi wa kitanzania wanaosoma kwenye vyuo vikuu mbalimbali vya India ambao idadi yao  imeongezeka na kufikia 2500 kwa mwaka.
“Ninayo furaha kubwa kuwajulisha kuwa shirika letu la ndege yaani Air Tanzania limefufuka. Na kuthibitisha hilo Shirika litaanza safari zake mjini Mumbai mwezi Novemba, 2018. Nawaomba msisite kutumia ndege yetu kwa safari zenu za utalii, biashara hata kwenda kusalimia ndugu zenu waliopo Tanzania na wale waliopo Tanzania kuja kusalimia ndugu huku India” alisisitiza Balozi Luvanda.

Mhe. Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wageni walioshiriki maonesho hayo ushirikiano, amani na usalama pale watakapokuwa Tanzania na kwamba Tanzania ni chaguo sahihi kwa utalii na wasisite kuja kwa shughuli mbalimbali za manufaa kwa nchi hizi mbili.


Uzinduzi wa ziara ya kitabibu Wilayani Kondoa




Dkt. Gwajima azindua ziara ya kitabibu Wilayani Kondoa

Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima akihutubia kwenye uzinduzi wa ziara ya Madaktari Wauguzi kutoka taasisi binafsi ya Health Education Development (HEAD INC) ya watanzania waishio nchini Marekani ya kutoa huduma za kitabibu  kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa. Dkt. Gwajima alitumia fursa hiyo kuwapongeza taasisi hiyo kwakuona umuhimu wa kuja nyumbani kutoa huduma za afya kwa watanzania wenzao. Dkt. Gwajima hakusita kuipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Idara ya Diaspora kwa kuwezesha kufanikisha Ziara ya Madaktari na Wauguzi hao kutoka Nchini Marekani ambapo inaonyesha namna mwitikio wa Watanzania waishio nje ya nchi katika kuchangia maendeleo nchini.  Madaktari na Wauguzi hao watakuwa kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kwa siku nne (4) wakitoa huduma za Afya kwa wagonjwa mbalimbali. 
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makutta (wa kwanza kushoto), na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Anisa Mbega wakimsikiliza kwa makini Dkt. Gwajima alipokuwa akihutubia kwenye ufunguzi wa ziara ya Madaktari na Wauguzi kutoka (Head Inc)
Sehemu ya Watumishi kutoka wilaya ya Kondoa wakimsikiliza kwa makini Dkt. Gwajima alipokuwa akihutubia kwenye ufunguzi wa Ziara ya Madaktari na wauguzi 
Sehemu ya Wananchi waliojitokeza kwenye Ufunguzi huo wakimikiliza kwa makini Dkt. Gwajima
Mkuu wa Wilaya Kondoa Mhe. Sezaria Makutta naye alipata fursa ya kuwakaribisha Madaktari na Wauguzi hao kwenye Wilaya ya Kondoa na kuwaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha kwa kipindi chote cha siku nne watakachokuwa wanatoa huduma za Afya katika Hospitali hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya NJe na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Anisa Mbega naye alipata Fursa ya kuwasalimia wananchi wa Wilaya ya Kondoa walio jitokeza kwenye Uzinduzi wa Ziara hiyo ya Madaktari na Wauguzi, pia alitumia fursa hiyo Kuwashukuru wanadiaspora kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya nchini kwa namna mbali mbali ikiwemo kuleta ujuzi wao,  kuwekeza kwenye sekta mbalimbali. Pia aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Kondoa kupitia Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makutta kwa maandalizi na mapokezi mazuri ya ziara hiyo. 

 Juu na chini sehemu ya wananchi wakiendelea kusikiliza hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa kwenye uzinduzi huo.

 Juu na chini sehemu ya wananchi wakianza kupata huduma za kiafya mara baada ya kufanyika kwa uzinduzi huo

Picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ufunguzi
Balozi Anisa Mbega akiagana na Dkt. Gwajima mara baada ya kumaliza ufunguzi wa Ziara ya Madaktari na Wauguzi.










Sunday, September 16, 2018

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Mabalozi wa India na Qatar waliopo nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini, Mhe. Sandeep Arya. Katika mazungumzo yao wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala mbalimbali ya manufaa kwa nchi zote mbili.

Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda alikutana na Balozi wa Qatar nchini na kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Qatar.

Maadhimisho ya Saba ya Siku ya Mara (Mara Day) yafanyika Kenya

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Maadhimisho ya Saba ya Siku ya Mara (Mara Day)

Bonde la mto Mara linalounganisha Tanzania na Kenya linashikilia uhai sio wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee, bali uhai wa nchi za Sudan, Ethiopia na Misri nazo kwa kiasi kikubwa unategemea bonde hilo.

Kauli hiyo ilitolewa na viongozi mbalimbali walioshiriki sherehe za maadhimisho ya saba ya Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika katika Kaunti ya Narok, Kenya siku ya Jumamosi tarehe 15 Septemba 2018. 

Maadhimisho ya Siku ya Mara ambayo kwa mwaka huu yalikuwa na kaulimbiu "Mto Mara unatuunganisha wote" hufanyika kwa kupokezana kati ya Tanzania na Kenya kila mwaka tarehe 15 Septemba kwa madhumuni ya kuhamasisha matumizi endelevu ya bonde la mto Mara.
 “Siku ya Mara hailengi chochote, isipokuwa kutukumbusha jukumu letu la kutunza mazingira”, Gavana wa kaunti ya Narok, Mhe Samuel Oletunai alisema katika maadhimisho hayo.

Mhe. Samuel Oletunai aliwaasa Wakenya kutunza msitu wa Mau ambao ndio chanzo kikuu cha maji yanayotiririka mto Mara na kuiomba Serikali ya Kenya kuhakikisha kuwa mgogoro katika msitu huo unapatiwa ufumbuzi haraka. 

Mwakilishi wa Serikali ya Tanzania katika maadhimisho hayo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb) alieleza kuwa maji hayana mbadala kama chakula ambapo ukikosa wali utakula ugali, hivyo aliwahakikishia wadau waliohudhuria sherehe hizo kuwa Serikali ya Tanzania haitakuwa kikwazo cha harakati za kuhifadhi ikolojia ya mto Mara.

Utunzaji wa ikolojia ya mto huo ilielezwa kuwa ni muhimu kwa shughuli mbalimbali ikiwemo utalii na shughuli nyingine za kiuchumi ambapo Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) katika sherehe hizo alisema kuwa Tanzania na Kenya zinapata zaidi ya Dola milioni 300 kwa mwaka kutokana  na shughuli za kiuchumi katika mto Mara.

Tukio kubwa linalovutia watalii wengi duniani ni uhamaji wa wanyamapori aina ya nyumbu zaidi ya milioni 1.2 baina ya mbuga ya Serengeti nchini Tanzania na Masai Mara nchini Kenya katika kipindi cha Julai hadi Oktoba ambapo mara zote wanyama hao hukatiza mto Mara.

Mwakilishi huyo wa USAID alitaja sababu zinazoharibu ikolojia ya mto huo kuwa ni pamoja na uharibifu wa misitu, matumizi makubwa ya maji, ujenzi wa miundombinu mbalimbali na mmomonyoko wa udongo. Hivyo, aliahidi kuwa USAID itaendelea kushirikiana na wadau kukabiliana na changamoto hizo kwa kusaidia miradi ya maji na utunzaji wa mazingira. Alisema mto huo lazima uhifadhiwe kwa sababu ni mali ya watu waliopita, wasasa na wajao.

Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika sherehe hizo, Mhe. Simon Chelugui aliwahakikishia waliohudhuria maadhimisho hayo kuwa Serikali ya Kenya imejizatiti kulinda na kuhifadhi ikolokia ya mto Mara kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Kenya, alizitaja kuwa ni pamoja na kuanzisha miradi ya maji na usafi katika mashule na aliutaja mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na benki ya maendeleo ya Afrika kwenye mpaka wa Isebania ambao utawanufaisha pia Watanzania wanaoishi maeneo ya Sirari.

Sherehe hizo zilipambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo maonesho ya bidhaa na huduma ambao uzalishaji wake unazingatia uhifadhi wa mazingira.

Aidha, kulikuwa na burudani za ngoma, michezo ya mpira wa miguu  mashairi, tunzo na ngojera ambazo zote zililenga kutoa ujumbe wa kuhimiza utunzaji wa mazingira. 
  
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Narok, kenya
16 Septemba 2018
Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya, Mhe. Simon Chelugui ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya saba ya Siku ya Mara akitoa hotuba ya ufunguzi ambayo ilielezea mikakati mbalimbali inayochukuliwa ili kukabiliana na vihatarishi vya kutokomeza ikolojia ya Mto Mara.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Mara yaliyofanyika kaunti ya Narok nchini Kenya
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana akitoa salamu katika maadhimisho ya Siku ya Mara.

Gavana wa akaunti ya Narok, Mhe. Samuel Oletunai akihutubia watu mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya Siku ya Mara ambayo yalifanyika katika kaunti yake ya Narok.

Watu mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Mara wakifuatilia hotuba za viongozi.

Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) akivalishwa vazi la kimasai kabla hajatoa hotuba yake katika maadhimisho hayo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima akitoa neno la mkoa katika maadhimisho hayo.

Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Pindi Chana; Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula; Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso; Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya, Mhe. Simon Chelugui wakipata maelezo kutoka moja ya banda la maonesho ya Siku ya Mara kuhusu utunzaji wa mazingira.

Mstari wa kulia kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Pindi Chana; Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula; Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso; Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya, Mhe. Simon Chelugui wakipata maelezo kutoka mmoja wa washiriki wa maonesho ya siku ya Mara namna anavyoshiriki katika shughuli za kutunza mazingira.

Kaimu Murugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Kijamii, Bw. Eliabi Chodota akiteta jambo na Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula.

Sehemu ya umati wa watu waliohudhuria maadhimisho ya saba ya Siku ya Mara wakisikiliza hotuba za viongozi.

Burudani kutoka kwa wanafunzi wakihimiza umuhimu wa kutunza mazingira.

Mmoja wa wanaharakati wa kutunza Mazingira akipokea cheti cha kutambua mchango wake kutoka kwa Gavana wa kaunti ya Narok, Mhe. Samuel  Oletunai. katikati ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Ally Said Matano.

Friday, September 14, 2018

Prof. Mkenda na Balozi wa Kenya wakutana kujadili utatuzi wa changamoto za biashara mipakani

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu walipokutana jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya. Pamoja na mambo mengine walijadili changamoto za biashara hususan tukio la hivi karibuni la kukwamishwa kwa bidhaa za Tanzania kuingia Kenya kwa sababu mbalimbali ikiwemo vinywaji, mchele na unga wa ngano. Katika kikao hicho ilikubalika Tanzania kuitisha kikao cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki na Biashara na Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Tanzania na Kenya. Pia walikubaliana kuendelea kuratibu ziara za viongozi wa juu kati ya nchi hizi mbili kwa lengo la kukuza mahusiano.

Prof. Mkenda na Balozi Kazungu wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo yao.