TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUTOKA MATAIFA
MBALIMBALI NA BALOZI ZA TANZANIA NJE YA NCHI
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea
kupokea salamu za rambirambi kutoka kwa marais, mawaziri wakuu wa mataifa
mbalimbali duniani kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha
MV Nyerere iliyotokea kwenye Ziwa Victoria, Mkoani Mwanza tarehe 20 Septemba,
2018 na kusababisha vifo, majeruhi na
upotevu wa mali.
Baadhi ya salamu zilizopokelewa ni pamoja na kutoka kwa Rais wa
Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, Rais wa Urusi, Mheshimiwa Vladmir Putin, Rais
wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Ujerumani, Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier, Rais wa Saharawi,
Mheshimiwa Brahim Ghali, Mtawala wa Kuwait, Mtukufu Sheikh Sabah Al-Ahmad al
Jaber Al-Sabah, Baba Mtakatifu, Papa Francis, Rais wa Italia, Mheshimiwa Sergio
Mattarella, Rais wa Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Finland,
Mheshimiwa Sauli Niinistö, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mheshimiwa Joseph Kabila
Kabange na Rais wa Jamhuri ya Sudan, Mheshimiwa Omar Hassan Ahmed Al-Bashir.
Viongozi wengine ni Waziri Mkuu wa Israel, Mheshimiwa Benjamin
Netanyahu, na Waziri Mkuu wa Sweden, Mheshimiwa Stefan Löfven.
Viongozi hao wameeleza kusikitishwa kwao na taarifa za vifo
vilivyosababishwa na ajali hiyo na
kuwatakia majeruhi kupona haraka.
Sehemu ya nukuu za salamu hizo zinasema “Mheshimiwa Rais Dkt.
John Pombe Magufuli, nilipokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za
ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyosababisha vifo vya watu wengi, majeruhi na
wengine kutojulikana walipo. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Kenya naomba
upokee na kufikisha salamu zetu za rambirambi kwa wafiwa na wananchi wote wa
Tanzania kufuatia ajali hiyo na tunawaombea majeruhi wote wapone haraka” ni
sehemu ya nukuu ya salamu kutoka kwa Mheshimiwa Rais Kenyatta
“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nilishtushwa na
taarifa za ajali hiyo mbaya iliyotokea Mkoani Mwanza. Kwa niaba ya Serikali ya
China, wananchi na mimi binafsi natoa pole kwa wafiwa wote na majeruhi” inasema
sehemu ya salamu kutoka kwa Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping.
Naye Rais wa Urusi, Mheshimiwa Putin amesema “Mheshimiwa Rais
Dkt. John Pombe Magufuli, tafadhali naomba upokee salamu zangu za rambirambi
kufuatia ajali iliyotokea. Naomba salamu hizi ziwafikie wafiwa wote na
ninawaombea majeruhi wapone haraka”
Aidha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
imepokea salamu za rambirambi kutoka kwa balozi mbalimbali zinazowakilisha nchi
zao hapa nchini pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini, ikiwemo
ubalozi wa Marekani, ubalozi wa Ufaransa, ubalozi wa Sudan Kusini, Ubalozi wa
Falme za Kiarabu (UAE), Serikali ya Brazil, Ubalozi wa Cuba, ubalozi wa Nigeria
na salamu kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Kimataifa nchini.
Wakati huohuo,
Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka kwa mabalozi wanaowakilisha
Tanzania kwenye nchi mbalimbali. Salamu zilizopokelewa zinatoka kwa mabalozi
wote wa Tanzania katika nchi za Qatar,
Ufaransa, Uingereza, Uholanzi, Afrika Kusini, Sweden, Nigeria, Burundi, Uganda,
Kenya, Ubelgiji, Zambia, Msumbiji, China, Japan, Brazil, Comoro, Algeria,
Sudan, Canada,
Kadhalika
tumepokea salamu kutoka kwenye balozi zetu zilizoko Marekani, Uturuki, Rwanda,
Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Kuwait, Saudi Arabia, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo (DRC), Zimbabwe, Malawi, Uswisi, India, Italia, Jamhuri ya Korea,
Urusi, Israel, Ethiopia, Ujerumani, Oman na Malaysia.
Baadhi
ya nukuu ya salamu za rambirambi za mabalozi hao zinasomeka kama ifuatavyo “Inna Lillah Wainna Illah Rajiuon.
Kwa niaba ya Ubalozi Abuja na
Watanzania waliopo katika eneo letu la
uwakilishi, tunatoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, familia na Watanzania
kwa ujumla kwa msiba mkubwa uliotufika.
Mwenyezi Mungu atupe subira na faraja katika
kipindi hiki cha majonzi na aziweke
roho za marehemu mahali pema na
majeruhi wapone haraka, Amin Amin,” ni kauli yake Mheshimiwa Muhidin Ally
Mboweto, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mheshimiwa
Dkt. Wilbroad Slaa anasema “kwa niaba ya wenzangu katika kituo cha Stockholm
tunatoa pole za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu na familia zote zilizoguswa na
msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na
kuwatia nguvu na ujasiri ndugu wote walioguswa na msiba huu”.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Balozi Modest Mero alisema haya;
“Ubalozi wa New York tunatoa pole kwa ajali mbaya ya Meli ya MV Nyerere
iliyopelekea wengi kupoteza maisha na wengi kuumia. Tunawaombea marehemu
pumziko la milele na wote waliojeruhiwa wapone haraka.”
Balozi wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa
Mbelwa Kairuki alieleza masikitiko yake kwa kusema kuwa “nasi huku Beijing
tunaungana na wenzetu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Watanzania na wanafamilia walioguswa msiba huu mzito. Mwenyezi Mungu
awape nguvu na awajalie moyo wa subira wakati wote mnaposhughulika na msiba
huo.
“Japan na diaspora yetu tunatoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote kwa msiba huu uliotokana na kuzama kwa
kivuko. Mungu atupe nguvu wote tuliobaki na awape pumziko la amani wenzetu
waliotutangulia. Kwa majeruhi tunawaombea wapone haraka na wavumilie mstuko huu
mkubwa katika maisha yao. Marehemu wapumzike kwa
amani”. Hizi ni salamu kutoka kwa Mheshimiwa
Mathias Chikawe, balozi wa Tanzania nchini Japan.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Abu Dhabi alisema
haya; “Ubalozi wa Tanzania
Abu Dhabi, tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali ya MV Nyerere.Kwa
niaba ya watumishi wote wa Ubalozi, tunatoa mkono wa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wenzetu
wote kwa msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu awajaalie marehemu wapumzike mahali
pema na awajaalie majeruhi kupona mapema. Amin”.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Dkt.
Asha-Rose Migiro akieleza kuguswa na ajali hiyo alitoa kauli hii “Ubalozi wa Tanzania London unajumuika na Watanzania
wenzetu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, familia
na ndugu wa wale wote waliopatwa na msiba kutokana na ajali hii. Tunawaombea
majeruhi wapone haraka na warejee katika shughuli zao za kujikimu na kulijenga
taifa letu”.
Kwa upande mwingine, Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka
Baraza la Diaspora wa Tanzania ulimwenguni kote (TDC Global) ambao wameeleza
masikitiko makubwa kufuatia ajali hiyo mbaya. Sehemu ya ujumbe wao unasomeka
kama ifuatavyo; “TDC Global, kwa masikitiko makubwa, inatoa salamu za
rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wote, ndugu, jamaa na marafiki kwa vifo
vilivyotokana na ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere kinachofanya safari
zake kati ya visiwa vya Bugorora na Ukara katika Ziwa Victoria. Kama TDC
Global, tunaungana na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huu mzito kwa
taifa letu. Pia tunatoa pole kwa majeruhi wote na kuwaombea wapone haraka”.
Imetolewa na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dodoma.
24
Septemba, 2018
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.