TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUTOKA KWA
VIONGOZI WA MATAIFA MBALIMBALI NA MASHIRIKA YA KIMATAIFA NA KIKANDA
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea
kupokea salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi wa mataifa na mashirika
mbalimbali ya kikanda na kimataifa kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kufuatia ajali ya
kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere iliyotokea kwenye Ziwa Victoria, Mkoani Mwanza
tarehe 20 Septemba, 2018 na kusababisha vifo, majeruhi na upotevu wa mali.
Baadhi ya salamu zilizopokelewa zinatoka kwa Katibu Mtendaji wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mheshimiwa Dkt. Stergomena
Lawrence Tax na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyopo Kisumu, Mheshimiwa Dkt. Ali Said Matano
Salamu zingine zimetoka kwa Waziri wa Nchi wa Uingereza, Mheshimiwa
Harriett Baldwin na Ofisi ya Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga.
Viongozi hao wameeleza kusikitishwa kwao na taarifa za vifo
vilivyosababishwa na ajali hiyo na
kuwatakia majeruhi kupona haraka.
Sehemu ya nukuu za salamu hizo zinasema “Mheshimiwa Rais Dkt.
John Pombe Magufuli, kwa niaba ya Sekretarieti ya SADC na mimi binafsi naomba kwa
dhati upokee salamu zetu za pole kwako wewe Mheshimiwa Rais, Serikali, Wananchi
wa Tanzania na familia zilizopoteza wapendwa wao. Tunaomboleza na Watanzania na
tunaomba Mungu awape nguvu familia zilizoathirika na tukio hilo na roho za
marehemu zipate pumziko la amani milele. Ninawaombea majeruhi uponyaji wa
haraka” ni sehemu ya nukuu ya salamu kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Stergomena.
Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria
Kisumu, Mhe. Dkt. Matano, ametoa pole kwa Watanzania na kukumbusha umuhimu wa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujenga Kituo cha Uratibu na Uokoaji Majini (MRCC)
iliyokubalika ijengwe jijini Mwanza.
Imetolewa na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dodoma.
25
Septemba, 2018
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.