Wednesday, September 12, 2018

Tanzania ilivyoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara nchini Msumbiji

Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mheshimiwa Rajabu Luhwavi, (katikati), akikaribishwa katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 54 ya FACIM yaliyofanyika tarehe 27 Agosti hadi 2 Septemba 2018 Maputo nchini Msumbiji. Wengine ni Bw. Albert Philipo, Afisa wa Wizara, Idara ya Diaspora (kushoto) na ndugu Nelson Nkini, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania (Diaspora) wanaoishi nchini Msumbiji  Ushiriki wa wafanyabiashara kutoka Tanzania uliratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Carlos Agostinho do Rosário wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 54 ya FACIM alipotembelea banda la Tanzania na kukaribishwa na Bi. Getrude Ngweshemi, Kaimu Meneja - Masoko ya Ndani wa TanTrade na Bw. Albert Philipo, Afisa Idara ya Diaspora, Wizara ya Mambo ya Nje ambapo alipatiwa maelezo kuhusu bidhaa za viwandani pamoja na vivutio vya utalii wa Tanzania.
                                                                                                         

Balozi Rajabu Luhwavi akifafanua jambo kwa wafanyabiashara na washiriki kutoka mataifa mengine (hawapo pichani) waliofika katika banda la Tanzania wakati maonesho ya biashara ya 54 ya FACIM yakiendelea.  Wafanyabiashara wa Tanzania walikutana na wafanyabiashara wenzao kutoka mataifa zaidi ya 20 ambapo walibadilishana mawazo na kuzitangaza bidhaa na huduma za Tanzania katika maonesho hayo.
Balozi Rajabu Luhwavi akipokea maelezo kutoka kwa Afisa wa Wizara, Bw. Albert Philipo kuhusu bidhaa za Tanzania zilizoletwa na wafanyabiashara mbambali kutoka Tanzania wakati wa maonesho ya biashara ya kimataifa ya 54 ya FACIM Maputo, Msumbiji. Wengine katika picha hiyo ni wafanyabiashara kutoka Kampuni mbalimbali nchini Tanzania.

Mheshimiwa Balozi Luhwavi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kutoka Tanzania walioshiriki katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 54 ya FACIM mjini Maputo.
Gavana wa Nampula, Mheshimiwa Victor Borges akiwa na Mheshimiwa Balozi Rajabu Luhwavi kushoto kwake wakikata utepe wakati wa kufungua Maonyesho ya Biashara Nampula tarehe 20 Agosti 2018. Maonesho hayo yalihusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na wenyeji wa Msumbiji. 
Mheshimiwa Balozi Rajabu Luhwavi akitoa maelezo mafupi wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Biashara Nampula yaliyohusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania. Kwa upande wake Balozi Luhwavi, alieleza kuwa maonesho haya ni ya kimkakati kwa ajili ya kukuza na kuimarisha umoja, mshikamano na mahusiano ya kiuchumi yaliyojengwa na waasisi wetu hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; hayati Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa rais wa kwanza wa Zanzibar na hayati Samora Moises Machel, aliyekuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Msumbiji. Maonesho haya yalifungua fursa za masoko kwa bidhaa za viwanda vya Tanzania pamoja na kuendeleza juhudi za utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa vitendo na kukuza uchumi, hususan uchumi wa viwanda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ndugu Juma Ali Juma aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa kilele cha maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania mjini Nampula akiwa pamoja na Balozi Rajabu Luhwavi na Katibu Mkuu wa Jimbo la Nampula, Bi. Veronica Langa wakipata maelezo kuhusu teknolojia ya ufugaji samaki kutoka kampuni ya Dokaman ya nchini Tanzania.
Kutoka kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mheshimiwa Rajabu Luhwavi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ndugu Juma Ali Juma, Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara TanTrade, Bi. Anna Bulondo wakipata maelezo kutoka kwa wawakilishi wa kampuni ya A - Z Textile Mills. 

Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mheshimiwa Rajabu Luhwavi akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Ndugu Juma Ali Juma wakipokea maelezo kuhusu bidhaa zinazotengenezwa na Kampuni ya Tanzania M/s Darsh Industries wakati wa maonesho ya bidhaa za viwanda mjini Nampula, Msumbiji. 





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.