Monday, September 3, 2018

Waziri Mkuu ahamasisha uwekezaji kutoka Jimbo la Jiangsu la China


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Meya wa Jimbo la Jiangsu la nchini China, Bw.Guo Yuan Qiung mara alpowasili kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini China kwa ajili ya mazungumzo rasmi. Mhe. Waziri Mkuu yupo nchini humo kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la ushirikiano kati ya Afrika Nna China (FOCAC) utakaofanyika tarehe 03 na 04 Septemba, 2018.
 
Mhe. Waziri Mkuu akizungumza na Bw. Qiung mara baada ya kumkaribisha Ubalozini
Mhe. Waziri Mkuu akimtambulisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Augustine Mahiga kwa Naibu Meya Qiung wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Waziri Mkuu na Naibu Meya

Mhe. Waziri Mkuu na ujumbe wa Tanzania wakizungumza na Naibu Meya wa Jiangsu na ujumbe wake walipofika Ubalozini. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda.
Naibu Meya Qiung (wa tatu kulia) akiwa na ujumbe aliofuatana nao wakimsikiliza Waziri Mkuu hayupo pichani

Mazungumzo yakiendelea

Mazungumzo yakiendelea. Wa pili kulia ni Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki

============================================================

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema Tanzania inahitaji wawekezaji wa uhakika kwenye sekta ya kilimo hususan watakaowekeza kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, kuongeza thamani na kutafuta masoko.

Mhe. Majaliwa aliyasema hayo wakati wa mazugumzo yake na Naibu Meya wa Jimbo la Jiangsu nchini China, Bw. Guo Yuan Qiung aliyoyafanya tarehe 03 Septemba, 2018 katika Ubalozi wa Tanzania nchini humo ikiwa ni mwendelezo wa program yake ya kukutana na wadau muhimu wa maendeleo kabla ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) utafanyika jijini Beijing kuanzia tarehe 01 hadi 04 Septemba, 2018.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Waziri Mkuu alimweleza Naibu Meya huyo kuwa, Tanzania inaendelea kuboresha sekta ya kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kwamba jimbo la Jiangsu ni moja ya mdau muhimu ambaye anaweza kuchangia maendeleo ya Tanzania kwa kutumia teknolojia ya viwanda vya uchakataji mazao ili kuongeza thamani na kupata masoko ya uhakika kwa mazao hayo. Alisema kuwa kwa kuwa jimbo la Jiangsu ni miongoni mwa majimbo yaliyopiga hatua kubwa ya maendeleo ya teknolojia na viwanda duniani. Hivyo kushirikiana na Tanzania katika sekta za kilimo na viwanda kutaiwezesha nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020 na nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Pia alisema kuwa, anathamini mchango wa Jimbo hilo katika uchumi wa Tanzania ambapo sasa kuna Kampuni mbili kubwa za uwekezaji kutoka jimboni humo ikiwemo kampuni ya kuchambua pamba na kutengeneza nyuzi ya mjini Shinyangana na Kiwanda cha Urafiki cha jijini Dar es Salaam. Hata hivyo alisema bado mchango wa jimbo hilo unahitajika katika uendelezaji viwanda hususan katika masuala ya teknolojia ya viwanda; kuimarisha utafiti kwenye sekta ya kilimo na kuisaidia Tanzania kupata masoko ya mazao kama mbaazi, mhogo na soya.

“Tanzania inapongeza kazi nzuri unayoifanya na tunathamini sana mchango wako katika maendeleo ya nchi yetu. Hadi sasa tunavyo viwanda viwili kutoka Juangshu. Tunaomba uendelee kuhamasisha kampuni nyingi zaidi kutoka jimboni kwako kuja kuwekeza nchini kwenye maeneo mbalimbali pamoja na kutusaidia kupata masoko ya mazao kama mbaazi, mhogo na soya” alisisitiza Mhe. Majaliwa.

Katika hatua nyingine walikubaliana na Naibu Meya huyo kuangalia uwezekano wa kufanya mapitio kuhusu changamoto  za uendeshaji wa Kiwanda cha Urafiki ili kutafuta suluhu ya haraka kwa kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na kuwaagiza wataalam wa pande mbili kukutana kuainisha changamoto hizo.

Kwa upande wake, Bw. Qiung alimhakikishia ushirikiano wa hali ya juu Mhe. Waziri Mkuu hususan katika uwekezaji wa viwanda na kwamba ni Imani yake kuwa mkutano wa FOCAC utatoa dira kwa maendeleo si kwa  Tanzania pekee bali kwa Bara zima la Afrika.

Aidha aliongeza kuwa, mbali na ushirikiano katika masuala ya kilimo na uendelezaji viwanda, jimbo lake lipo tayari kushirikiana na Tanzania katika masuala ya elimu ambapo jimbo hilo lina vyuo vikuu zaidi ya 60,000 vinvyotoa kozi mbalimbali na kuwakaribisha wanafunzi kutoka Tanzania kwenda jimboni humo.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.