Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewakaribisha
wafanyabiasha na wawekezaji kutoka China kuja Tanzania kuwekeza kutokana na mazingira rafiki ya uwekezaji na hali ya amani
na utulivu iliyopo nchini.
Waziri
Mkuu alitoa rai hiyo wakati akifungua Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na
China lililowashirikisha wafanyabiashara zaidi ya 80 kutoka nchi hizi mbili.
Mhe. Majaliwa ambaye yupo nchini China kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la
Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) alitumia fursa hiyo kukutana na
wafanyabiashara hao ili kuwaeleza hali ya uwekezaji nchini katika
Mhe.
Majaliwa alisema kuwa, Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuvutia
wawekezaji ambazo kwa kiasi kikubwa zimezaa matunda ambapo katika Ripoti ya
uwekezaji duniani kwa mwaka 2018 imeitaja Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji kwa
ukanda wa Afrika Mashariki ambapo imewekeza takribani dola za marekani bilioni
1.2.
Mhe.
Majaliwa aliongeza kuwa, Tanzania inamazingira mazuri sana ya uwekezaji ikiwemo
ardhi nzuri kwa kilimo cha mazao mbalimbali kama miwa, mpunga, ngano, mahindi,
Mhogo na katani. Alisema kuwa, jumla ya hekta milioni 44 za ardhi zinafaa kwa
kilimo na zaidi ya hekta milioni 29 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Akizungumzia
sekta ya madini, Mhe. Majaliwa alisema kuwa ni moja ya sekta muhimu
inayochangia pato la taifa na kuwahamashisha wawekezaji kuchangamkia sekta hiyo
hususan kwenye uchimbaji na uchakataji wa madini ya chuma na uchimbaji wa
madini ya urani.
Kuhusu
utalii, Mhe. Waziri Mkuu alisema kuwa Tanzania imekuwa ikifaidika kwa kiasi
kikubwa kutokana na kujaliwa vivutio vingi vya utalii ikiwemo fukwe zilizopo
Zanzibar, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Ngororngoro. Hata hivyo alisema bado
sekta hii inahitaji wawekezaji hususan kwenye ujenzi wa miundombinu ya utalii
kama vile hoteli na sekta ya huduma kwa watalii kwa ujumla.
Masuala
mengine aliyowaeleza wawekezaji hao ambayo ni fursa kwao ni pamoja na eneo la
teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo kwa sasa soko ni kubwa kutokana na ongezeko la watumiaji wa simu na
mitandao hususan watu wanaoishi vijijini. Aliwakaribisha wawekezaji kuwekeza
katika sekta hii katika maeneo ya ukarabati na utengenezaji wa vifaa vya
mawasiliano na kujenga viwanda vya kuunganisha simu.
Mhe.
Waziri Mkuu alihitimisha kwa kuhimiza wawekezaji kuja nchini na kusisitiza
kuwa, “ukitaka kuwekeza Afrika karibu Tanzania”
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.