Mhe. Waziri Mkuu akizungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Syngning Guangzhou ya nchini China, Bw. WU Haineng. Kampuni ambao wana nia ya kufanyabiashara na Tanzania katika zao la mhogo
======================================================== WAZIRI MKUU AKUTANA NA WATENDAJI WA KAMPUNI KUBWA ZA CHINA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Watendaji Wakuu wa Kampuni kubwa za China
kwa lengo la kujadiliana nao kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Kampuni
hizo.
Mhe. Majaliwa ambaye yupo nchini
China akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaaa la
Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) utakaofanyika tarehe 3 na 4
Septemba, 2018, ametumia fursa hiyo kukutana na Watendaji hao katika hatua za kuhamasisha
uwekezaji, biashara na maendeleo nchini.
Katika mkutano wake na Rais wa
Kampuni ya NORINCO (China North Indust Bw. Zhang Gaunjie, Mhe. Waziri Mkuu
amepongeza uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini hususan kwa kuwa na miradi na Jeshi
la Wananchi wa Tanzania na kuikaribisha kuwekeza zaidi katika maeneo mengine
hususan ujenzi wa miundombinu hasa ya Makao Makuu ya nchi. Mhe. Waziri Mkuu
alimweleza Rais huyo kuwa, Tanzania inahitaji teknolojia ya kisasa ili
kuwezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya makazi hususan kwa
Watumishi wa Serikali ambapo sasa Serikali imehamishia Makao Makuu Dodoma.
Kwa upande wake Bw. Zhang Ghaujie
alieleza kuwa Kampuni ya NORINCO ambayo
imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miradi ya Jeshi la Wanachi Tanzania, sasa
ipo tayari kushiriki kwenye miradi mingi Zaidi nchini hususan ile ya ujenzi na
kwamba kutokana na uwezo na uzoefu
mkubwa wa Kampuni hiyo katika sekta ya ujenzi itashirikiana na Tanzania kwenye
miradi ya ujenzi wa makao makuu na bomba la mafuta.
“NORENCO ipo tayari kuongeza maeneo ya ushirikiano na
Tanzania na inao uwezo wa kushiriki katika kazi za ujenzi hususan kwenye miradi
kama bomba la mafuta na Makao Makuu ya nchi” alisema Rais huyo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekutana
na kufanya mazugumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya HEGNYA Cement, ambayo
imeonesha nia ya kuja nchini kuwekeza kwenye ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha
saruji na Eneo la Viwanda (Indusrial Park) Mkoani Tanga. Kukamilika kwa mradi
huo kutaongeza uzalishaji wa saruji nchini kwa tani milioni 7 kwa mwaka na
kuzalisha ajira kwa Watanzania 4000.
Waziri Mkuu pia alipata fursa ya
kukutana na Rais wa Kampuni ya Zinjin Gold Mine, Bw. George Fang. Katika
mazungumzo yao, Mhe. Waziri Mkuu alimkaribisha kuja kuwekeza kwenye uchimbaji
na viwanda vya uchakataji wa madini hususan Tanzanite. Mhe. Waziri Mkuu
alimweleza kuwa madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana Tanzania pekee
yanahitaji mwekezaji makini ambaye atachimba, kuchakata na kuongeza thamani
madini hayo kwa faida ya Tanzania.
“Tanzanite inapatikana Tanzania
pekee. Tunatafuta mwekezaji makini wa kuchimba na kuchakata madini hayo ili
kuona faida ya madini hayo muhimu kwa Tanzania” alisema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Bw. Fang alimweleza
Waziri Mkuu kuwa, kampuni ya Zijin ambayo imewekeza kwenye uchimbaji mkubwa wa
madini ya dhahabu, shaba na zinki ipo tayari kuja nchini kuwekeza kwenye
uchimbaji wa madini hayo chini ya Sheria Mpya ya Madini ya Tanzania. Pia
alifurahishwa na taarifa ya Waziri Mkuu kuhusu uchimbaji wa madini ya Tanzanite
na kumhakikishia kuwa kampuni yake inao uwezo wa kutafiti, kuchimba, kuchakata,
kuongeza thamani na kutafuta masoko kwa madini yoyote ikiwemo Tanzanite.
“Kampuni ya Zijin Gold Mine ni
Kampuni kubwa, inamiliki migodi katika majimbo 20 nchini China na imewekeza
kwenye nchi 9 duniani. Ni ya pili katika uzalishaji wa madini ya Zinki na inashikilia nafasi ya tatu
katika uzalishaji wa shaba. Tunaona ni fursa muhimu kuja kuwekeza katika sekta
ya madini nchini Tanzania. Tunahitaji ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya
madini ambao utafuata misingi ya uwazi kwa faida ya kila mmoja” alisisitiza
Rais huyo.
Wakati huohuo, Mhe. Waziri Mkuu
alizungumza na kumshukuru kwa kazi nzuri Rais wa Kampuni ya CCECC, ambayo
inatekeleza miradi ya maendeleo nchini ukiwemo mradi wa Ubungo Interchange,
ukarabati wa Reli ya Kati na Mradi mkubwa wa maji kwenye Wilaya ya Mwanga
mkoani Kilimanjaro. Pia alimtaka kukamilisha miradi haraka na kuongeza miradi
zaidi kwenye ujenzi wa maeneo ya viwanda kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya
kilimo hususan kwenye zao la korosho. Rais huyo alimhakikishia Waziri Mkuu
kuwa, Kampuni yake itakamilisha miradi yote kwa wakati kama ilivyokubaliana na
Serikali ukiwemo Mradi wa Ubungo, ambao utakamilika ifikapo mwezi Juni 2020.
Aidha, kampuni hiyo imeahidi
kuongeza uwekezaji Tanzania huku wakitoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzaia na
kutumia rasilimali za Tanzania ili kutoa mchango mkubwa wa maendeleo ya nchi.
Kampuni ya CCECC imewekeza Tanzania miradi yenye thamani ya takribani dola za
Marekani bilioni 1.5 na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania zaidi ya 4000.
Katika mkutano wake na Mwenyekiti wa
Kampuni ya GNSG (Guangdong New South Group) ambayo ina nia ya kuwekeza kwenye
ujenzi wa Eneo ya Viwanda (Industrial Parks) nchini, Mhe. Waziri Mkuu alimhakikishia kuwepo kwa
maeneo ya uwekezaji wa aina hiyo katika mikoa yote ya Tanzania na kumwagiza
Mkurugenzi Mkuu wa Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA), Bw. Joseph Simbakalia
kuhakikisha anaipatia Kampuni hiyo taarifa kamili za maeneo ya uwekezaji wa
viwanda nchini ili kuwawezesha kufanya maamuzi haraka ya kuja nchini.
-Mwisho-
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.