Wednesday, March 13, 2019

Prof. Kabudi apokea Salamu za Pongezi kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa China

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Prof. Kabudi apokea Salamu za Pongezi kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa China

Mheshimiwa Prof. Palamagamba J. Kabudi (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, leo tarehe 13 Machi, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa WANG Ke, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China.

Mheshimiwa WANG Ke pamoja na masuala mengine amewasilisha kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki barua ya pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China kufuatia Prof. Kabudi kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Aidha Prof. Kabudi kupitia kwa Mheshimwa Balozi ameshukuru kwa salamu hizo za pongezi alizopokea.

Katika mazungumzo yao, Prof. Kabudi na Balozi WANG Ke, wameahidi kufanya kazi kwa pamoja ili kuimarisha ushirikiano wa kihistoria baina ya nchi hizo mbili. Na kwa pamoja wamesisitiza umuhimu wa kuendelea na jitihada za kuimarisha mahusiano ya kisiasa, kijamii, kiuchumi hususan kwenye maeneo la uwekezaji, biashara, utalii na miundombinu.
                                                                      
Prof. Kabudi ametumia fursa hiyo kuishukuru Jamhuri ya Watu wa China kwa misaada ya kimaendeleo wanayoendelea kuitoa na kwamba Serikali inafurahishwa na Jinsi China inavyounga mkono jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo na kujenga uchumi.

Tanzania na China zimekuwa na mahusiano ya kidiplomasia tangu mwaka 1964 na mwaka huu zinatarajia kuadhimisha miaka 55 ya ushirikiano huo.

Mheshimiwa Wang amekuwa Balozi wa kwanza kuonana na Mhe. Kabudi tangu kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
13 Machi 2019
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akipokea barua ya pongezi kutoka kwa Balozi wa China nchini, Mhe. WANG Ke. Balozi wa China aliwasilisha barua hiyo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. WANG Yi ambapo anampongeza Prof. Kabudi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mhe. Prof. Kabudi akisoma barua ya pongezi kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa China ambayo iliwasilishwa wizarani na Balozi wa China nchini.

Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China mara baada ya kupokea barua ya pongezi.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Prof. Kabudi kushiriki Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika

Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anatarajiwa kuondoka nchini tarehe 14 Machi, 2019 kuelekea Windhoek, Namibia kwa lengo la kuhudhuria Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya  ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika kuanzia tarehe 15 hadi 17 Machi 2019.

Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mawaziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Mawaziri wa Fedha pamoja na Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama wote wa SADC. Mkutano huu utatanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Machi 2019 ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe anashiriki.

Aidha, mkutano huu utajadili  masuala mbalimbali ikiwemo: Taarifa ya utekelezaji wa mipango na mikakati ya SADC; Taarifa ya Kamati ya Fedha na Kamati ya Usimamizi wa Rasilimali watu; Hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Visiwa vya Comoro kujiunga na SADC na Mpango wa Kuanzisha Chuo cha Uhawilishwaji cha SADC (SADC University of Transformation).

Masuala mengine yatakayojadiliwa ni; Utekelezaji wa Mkakati wa Kanda wa Mawasiliano; Mabadiliko ya Kitaasisi katika Umoja wa Afrika; na Majadiliano ya Ubia Mpya Baina ya Nchi za Kundi la Afrika, Carribean na Pasifiki (ACP) na Umoja wa Ulaya (EU) baada ya mkataba wa sasa wa Cotonou kumalizika mwaka 2020.

Mhe. Prof. Kabudi ambaye ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo, atatumia fursa hiyo kuendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha utangamano na ushirikiano katika Kanda na kufanya Jumuiya ya SADC kuwa chanzo muhimu cha maendeleo kwa wananchi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, 13 Machi 2019.



Nafasi za masomo na ajira

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nafasi za masomo na ajira

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuwahimiza Watanzania wenye sifa kuomba fursa za masomo na ajira zinazotolewa na wadau mbalimbali duniani. Fursa zilizopokelewa mwezi Machi 2019 ni kama ifuatavyo:

i.       Mafunzo ya Shahada ya Uzamili yanayotolewa na Chuo Kikuu cha British nchini Misri (British University – Egypt) kwa kipindi cha mwaka wa masomo 2019/2020. Fursa hizi zinaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na maombi yanafanyika kwa njia ya  mtandao kupitia tovuti, http://www.bue.edu.eg/;

ii.    Mafunzo ya Shahada ya Kwanza na Uzamili yanayotolewa na Taasisi ya Elimu ya Urusi (Russian Education Institute)                                               kwa kipindi cha mwaka wa masomo 2019/2020 na 2020/2021. Fursa hizi zinaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Maelezo ya namna ya kuomba fursa hizo yanapatikana katika Wizara zinazoratibu mafunzo hayo. Mwisho wa kufanya maombi kwa mwaka wa masomo 2019/2020 ni tarehe 25 Machi 2019 na tarehe 25 Juni 2020 kwa mwaka wa masomo 2020/2021;

iii. Mafunzo ya Shahada ya Uzamili katika fani ya Usuluhisihi katika Mchakato wa kutafuta Amani (Mediation in Peace Processes) yatakayotolewa nchini Uswisi katika kipindi cha mwaka wa masomo 2019/2021.  Maombi yanafanyika kwa njia ya mtandao kupitia tovuti, http://www.mas-mediation.ethz.ch/.  Mwisho wa kufanya maombi ni tarehe 21 Aprili 2019;

NAFASI ZA AJIRA
iv. Nafasi ya ajira ya Afisa Tathmini (Evaluation Officer, P-3) katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Kudhibiti Matumizi ya Silaha za Kemikali (The Secretariat of the Organization for the Prohibition of Chemical Weapons-OPCW). Maelezo ya jinsi ya kuomba yanapatikana katika tovuti, https://opcw-career.talent-soft.com/job/job-officer-industry-p-3_11.aspx. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 15 Machi 2019; na

v.    Nafasi ya ajira ya Afisa Usalama wa Masuala ya Habari (Information Security Officer, P – 3) katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Kudhibiti Matumizi ya Silaha za Kemikali (The Secretariat of the Organization for the Prohibition of Chemical Weapons-OPCW). Maelezo ya jinsi ya kuomba yanapatikana katika tovuti, https://opcw-career.talent-soft.com/job/job-information- security-officer-industry-p-3_18.aspx. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 26 Machi 2019.
         

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
13 Machi 2019

Balozi wa Canada atembelea Wizara ya Mambo ya Nje

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Balozi wa Canada atembelea Wizara ya Mambo ya Nje 

Bw. Jestas A. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O’Donnell tarehe 11 Machi 2019.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salam yamelenga kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Canada. Mataifa haya mawili, kwa kipindi kirefu yamekuwa yakishirikiana kwenye masuala ya afya, elimu, ukuzaji wa uchumi, Utawala Bora pamoja na biashara na uwekezaji.

Katika mazungumzo hayo, Balozi wa Canada amemhakikishia Kaimu Mkurugenzi kuwa, Serikali ya Canada inaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano katika kuleta Maendeleo na kuondoa umaskini na kwamba Canada itatekeleza kwa ufanisi miradi iliyopo inayotekelezwa kupitia Serikali , Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Asasi zisizo za Kiserikali(NGOs).

Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi alimkaribisha Balozi huyo mpya nchini na kuishukuru Serikali ya Canada kwa ushirikiano mzuri na wakihistoria uliodumu baina ya Tanzania na Canada .

Aidha, aliishukuru Serikali ya Canada kwa kuisaidia Tanzania katika miradi muhimu na ya kipaumbele hususan miradi ya afya, elimu na ukuzaji wa uchumi. Alimhakikishia ushirikiano thabiti wa Wizara na Serikali kwa jumla katika kuhakikisha miradi iliyopo inatekelezwa kwa ufanisi na mingine mipya inaibuliwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
13 Machi 2019

Bw. Jestas A. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika akimkaribisha Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O’ Donnell

Bw. Jestas A. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O’Donnell.


Bw. Jestas A. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika akiendelea kufanya majadiliano na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O’ Donnell.

Prof. Kabudi akutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Prof. Palamagamba J. Kabudi (Mb)  amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Mikhail Bogdanov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi katika Ofisi Ndogo ya Wizara Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Waheshimiwa Mawaziri 
wamezungumzia masuala mbalimbali yaliyolenga kuboresha na kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya mataifa haya mawili, hususan, katika Nyanja ya kidiplomasia, nishati, biashara na uwekezaji. Naibu Waziri huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku  mbili. 
Waheshimiwa Mawaziri wanaendelea na mazungumzo hayo, huku ujumbe aliofuatana nao Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi ukifuatilia mazungumzo hayo


Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Mej. Jenerali mstaafu Simon Mumwi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestas Nyamanga, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mhe. Yuri Popov na Afisa wa Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania wakifuatilia mazungumzo ya Waheshimiwa Mawaziri.

Tuesday, March 12, 2019

Prof. Kabudi na Dkt. Mahiga wakabidhiana majengo ya ofisi za Wizara zao Mtumba

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akimkabidhi Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, mchoro wa jengo la Ofisi za Wizara ya Mambo ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zinazojengwa kwenye Mji wa Serikali uliopo Mtumba, Dodoma. Makabidhiano hayo yalifanyika tarehe 12 Machi 2019. Baada ya kukabidhiwa Prof. Kabudi alipongeza jitihada za Wizara chini ya usimamizi wa Mhe. Dkt. Mahiga kwa hatua kubwa iliyofikiwa kwenye ujenzi huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome akitoa maelezo mafupi kwa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria walipofika  kwenye ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria zinazojengwa kwenye mji wa Serikali uliopo, Mtumba jijini Dodoma kwa ajili ya makabidhiano.
Mhe. Prof. Kabudi na Mhe. Dkt. Mahiga wakiwa kwenye moja ya chumba cha jengo la  ofisi za Wizara  zinazojengwa Mtumba


Mhe. Prof. Kabudi akisalimiana na mmoja wa Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alipotembelea ofisi za Wizara zinazojengwa Mtumba
Mhe. Prof. Kabudi akiongozana na Mhe. Dkt. Mahiga kuelekea kwenye jengo la Wizara, Mtumba
Mhe. Prof. Kabudi akisaini kitabu cha wageni na kutoa maoni yake kuhusu maendeleao ya ujenzi  wa ofisi hizo 
Mhe. Prof. Kabudi na Mhe. Dkt. Mahiga wakiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo na mafundi wanaojenga jengo la ofisi za Wizara zilizopo Mtumba
Muonekano wa jengo la ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki linalojengwa kwenye mji wa Serikali uliopo Mtumba, Dodoma











Prof. Kabudi na Dkt. Mahiga wakabidhiana ofisi

Waziri wa Katiba na Sheria ambaye awali alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akikabidhi Taarifa ya Makabidhiano ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.  Prof. Palamagamba Kabudi ambaye awali alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Makabidhiano hayo yalifanyika jijini Dodoma tarehe 12 Machi 2019.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi (kushoto) akimkabidhi Taarifa ya Makabidhiano ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akiweka saini Kitabu cha mahudhurio mara baada ya kukabidhiwa ofisi jijini Dodoma.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi mara baada ya makabidhiano ya ofisi.
Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakishuhudia makabidhiano ya ofisi kati ya Waziri wa Katiba na Sheria na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akiongea na Wakuu wa Idara na Vitengo (hawapo pichani) baada ya kukabidhiwa ofisi na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga.
Wakuu wa Idara na Vitengo wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (hayupo pichani).
Wakuu wa Idara na Vitengo wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiongea na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi Savera Kazaura akitoa maelezo kwa  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Waziri wa Katiba na Sheria kabla zoezi la makabidhiano kuanza.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na baadhi ya watumishi mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Anayemkaribisha  ni mmoja wa watumishi hao, Bw. Shaban Mtambo.
Bi. Chiku Kiguhe akisalimiana na Mhe. Prof. Kabudi.
Bw. Habibu Ibrahim akisalimiana na Mhe. Waziri.
Bw. Maulidi Mkenda akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiongea na baadhi ya watumishi waliojitokeza kumpokea mara alipowasili kwa mara ya kwanza katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Dodoma.
Bw. Caesar Waitara akisalimiana na Mhe. Prof. Kabudi



Monday, March 11, 2019

Balozi wa Tanzania nchini India awasilisha Hati za Utambulisho nchini Bangladesh

Balozi wa Tanzania nchini India anayewakilisha pia nchini Bangladesh, Mhe. Baraka Luvanda akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Bangladesh, Mhe. Md. Abdul Hamid katika hafla iliyofanyika hivi karibuni katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Dhaka.
Mhe. Balozi Luvanda akizungumza na Mhe. Rais Md. Abdul Hamid mara baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais huyo
Mhe. Balozi Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Rais Md. Abdul Hamid mara baada ya mazungumzo baina yao
Mhe. Balozi Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Rais Md. Abdul Hamid mara baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho. Kushoto ni Dkt. Kheri Goloka, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania ambaye alifuatana na Balozi Luvanda kwenye hafla hiyo

Mhe. Balozi Luvanda akiwa mbele ya gwaride la heshima mara baada ya kuwasili Ikulu ya Dhaka,  Bangladesh

Mhe. Balozi Luvanda akipita katikati ya gwaride la heshima mara baada ya kuwasilis Ikulu kwa ajili ya kuwasilisha hati za utambulisho

Sunday, March 10, 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha kwenye ajali ya ndege iliyotokea Ethiopia

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea kwa masikitiko makubwa, taarifa kuhusu ajali ya ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Ethiopia, iliyotokea tarehe 10 Machi 2019 nchini Ethiopia na kusababisha vifo vya watu wote 157 waliokuwemo kwenye ndege hiyo.

Ndege hiyo ya abiria, aina ya  Boeing 737 yenye namba za usajili ET 302 iliyokuwa inafanya safari zake za kawaida kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, mjini Addis Ababa, Ethiopia kuelekea mjini Nairobi, Kenya, ilikuwa imebeba abiria 149 kutoka mataifa mbalimbali na wafanyakazi wa kwenye ndege wapatao 8.

Kwa mujibu wa taarifa kuhusu ajali hiyo, iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Ethiopia, ikiwemo orodha ya abiria na mataifa wanayotoka, hakuna Mtanzania aliyekuwemo kwenye ndege hiyo.

Orodha ya nchi na idadi ya raia (kwenye mabano) waliokuwa kwenye ndege hiyo  ni kama ifuatavyo: Kenya (32), Canada (18), Ethiopia (9), China (8), Italia (8), Marekani (8), Ufaransa (7), Uingereza (7), Misri (6), Ujerumani (5), India (4), Slovakia (4), Austria (3), Urusi (3), Sweden (3), Hispania (2), Israel (2), Morocco (2) na Poland (2).

Nchi zingine ni Ubelgiji (1), Djibouti (1), Indonesia (1), Ireland (1), Msumbiji (1), Norway (1), Rwanda (1), Saudi Arabia (1), Sudan (1), Somalia (1), Serbia (1), Togo (1), Uganda (1), Yemen (1), Nepal (1), Nigeria (1) na raia aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Umoja wa Mataifa (1).

Mamlaka husika zimeanza uchunguzi ili kujua  chanzo cha ajali hiyo.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaungana na wote walioguswa na msiba huu mzito kutoa pole kwa mataifa yote yaliyopoteza raia wake kwenye ajali hiyo.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.

10 Machi 2019