Prof. Kabudi kushiriki Mkutano wa Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki anatarajiwa kuondoka nchini tarehe 14 Machi, 2019
kuelekea Windhoek, Namibia kwa lengo la kuhudhuria Mkutano wa Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) utakaofanyika kuanzia tarehe 15 hadi 17 Machi 2019.
Mkutano
huu unatarajiwa kuhudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mawaziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji na Mawaziri wa Fedha pamoja na Makatibu Wakuu kutoka nchi
wanachama wote wa SADC. Mkutano
huu utatanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Machi 2019 ambapo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.
Faraji Kasidi Mnyepe anashiriki.
Aidha, mkutano huu utajadili masuala mbalimbali ikiwemo: Taarifa ya
utekelezaji wa mipango na mikakati ya SADC; Taarifa ya Kamati ya Fedha na
Kamati ya Usimamizi wa Rasilimali watu; Hatua zilizofikiwa katika mchakato wa
Visiwa vya Comoro kujiunga na SADC na Mpango wa Kuanzisha Chuo cha
Uhawilishwaji cha SADC (SADC University of Transformation).
Masuala mengine yatakayojadiliwa ni; Utekelezaji wa
Mkakati wa Kanda wa Mawasiliano; Mabadiliko ya Kitaasisi katika Umoja wa
Afrika; na Majadiliano ya Ubia Mpya Baina ya Nchi za Kundi la Afrika, Carribean
na Pasifiki (ACP) na Umoja wa Ulaya (EU) baada ya mkataba wa sasa wa Cotonou
kumalizika mwaka 2020.
Mhe. Prof. Kabudi ambaye ataongoza ujumbe wa
Tanzania kwenye mkutano huo, atatumia fursa hiyo kuendelea kusisitiza umuhimu
wa kuimarisha utangamano na ushirikiano katika Kanda na kufanya Jumuiya ya SADC
kuwa chanzo muhimu cha maendeleo kwa wananchi wa nchi wanachama wa jumuiya
hiyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, 13 Machi 2019.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.