Mazungumzo yakiendelea.
=====================================================================================
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Mhe. Prof. Kabudi akutana kwa mazungumzo
na Balozi wa UAE nchini
Mhe.
Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Khalifa Abdulrahman
Al-Marzooqi, Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini.
Katika
mazungumzo yao yaliyofanyika tarehe 20 Machi 2019 kwenye ofisi ndogo za Wizara
zilizopo Dar es Salaam, Prof. Kabudi alimshukuru Mhe. Balozi Al-Marzooqi kwa
kupata fursa ya kukutana naye na kwamba, Tanzania inathamini mahusiano na
ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za
Kiarabu.
Aidha,
alimweleza Balozi huyo kuwa, Wizara chini ya uongozi wake itaendelea na
jitihada za kuhakikisha kuwa, mahusiano yaliyopo kati ya nchi hizi mbili
yanaimarishwa.
Kwa
upande wake, Mhe. Balozi Al-Marzooqi ametumia mazungumzo hayo kumpongeza Mhe.
Prof. Kabudi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki na kumhakikishia ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha mahusiano
yaliyopo yanaimarishwa.
Mhe. Balozi Al-Marzooqi aliongeza kuwa, Umoja
wa Falme za Kiarabu una nia ya kuimarisha mahusiano yaliyopo na umepanga
kufungua Ubalozi mdogo (Consulate General) Zanzibar. Pia, Mhe. Balozi
alimuarifu Mhe. Waziri kwamba ana mpango
wa kuutembelea Mkoa wa Dodoma ili pamoja na masuala mengine, kujionea eneo
walilopewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za ubalozi na makazi kwa
lengo la kujipanga kuliendeleza.
Kadhalika,
Prof. Kabudi na Mhe. Balozi Al-Marzooqi wamekubaliana kuendeleza ushirikiano
kwenye maeneo ya uwekezaji ambapo Balozi huyo ameonesha nia ya kuendelea
kushawishi wawekezaji kutoka nchini kwake kuja kuwekeza nchini hususan kwenye sekta
za utalii, hoteli, viwanda na utoaji wa huduma. Pia ameahidi kuwashawishi
wafanyabishara wakubwa na wadogo kutoka UAE kuja nchini ili kujionea fursa za biashara
zilizopo.
Prof.
Kabudi amemuhakikishia Balozi Al-Marzooqi kuwa, Tanzania ni eneo bora la
uwekezaji na biashara na kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara zingine zitaendelea kuweka
mazingira mazuri ya kupokea wawekezaji na wafanyabiashara kutoka maeneo yote
duniani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
20 Machi 2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.