Saturday, March 9, 2019

Serikali ya awamu ya tano haichukii wawekezaji, Dkt. Magufuli

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya awamu ya tano haichukii wawekezaji, Dkt. Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema Serikali ya awamu ya tano anayoiongoza inathamini wawekezaji, tofauti na dhana ya baadhi ya watu kuwa wawekezaji katika awamu ya tano wanaonekana kuwa ni maadui.

Mhe. Rais Magufuli alisema hayo wakati wa sherehe ya kufungua mwaka 2019 ya wanadiplomasia (sherry party) iliyofanyika Ikulu jijini Dar Es Salaam tarehe 08 Machi 2019, na kuhudhuriwa na Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yaliyopo hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli alisema uamuzi aliochukua hivi karibuni wa kuunda Wizara maalum ya uwekezaji ni ishara ya wazi kuwa Serikali ya awamu ya tano inathamini wawekezaji, na kuwasihi wanadiplomasia kuitumia wizara hiyo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ameifanyia mabadiliko.

Rais Magufuli alisema, Serikali yake imeshaanza mpango kabambe wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kutoa wito kwa wale wenye dhamira ya dhati ya kuwekeza nchini, waende mamlaka husika ili wahudumiwe.  “Mwenye dhamira ya dhati ya kuwekeza nchini, aende Wizara ya Uwekezaji au Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akikwamishwa huko aje kwangu ili nimkwamue huyo aliyekwamisha”, Rais Magufuli alisema.

Wanadiplomasia walioshiriki hafla hiyo, walisisitizwa kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, madini na viwanda vya nguo. “Serikali inahimiza uwekezaji katika sekta zinazotumia malighafi zinazopatikana nchini na zitakazotoa ajira za kutosha kwa vijana wa kitanzania kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi”.  Rais Magufuli alisema.

Kuhusu utalii, Rais Magufuli alieleza kuwa, Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, zikiwemo fukwe, uoto wa asili, malikale, mbuga za Wanyama na kwamba Serikali imejipanga kutangaza vivutio hivyo, hususan, vile vinavyopatikana kanda ya kusini. Mhe.  Rais aliitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa uamuzi wake wa kuanzisha channel maalum ya kutangaza vivutio vya utalii.

Kwa upande wa sekta ya madini, Serikali imejipanga kudhibiti wizi, biashara ya magendo, kuanzisha masoko ya kuuza madini na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata madini, ili sekta hiyo iwe na mchango mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi.

Aidha, Rais Magufuli alitumia hafla hiyo kuwaeleza wanadiplomasia, mafanikio ya Serikali ya mwaka 2018, mafanikio hayo ni Pamoja na Serikali kuendelea kulinda na kudumisha amani ya nchi; kukuza uchumi wa nchi ambapo katika nusu ya kwanza ya mwaka 2018, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tano barani Afrika, uchumi wake umekua kwa kasi ikizidiwa na Ethiopia pekee.

Tanzania pia iliweza kudhibiti mfumuko wa bei na iliongoza katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 1.18.

Mafanikio mengine ni Pamoja na ujenzi wa Miundombinu ikiwemo: ujenzi unaondelea wa reli ya kiwango cha Kimataifa kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma; ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme wa Mega Watts 2100 katika Mto Rufiji; ujenzi na upanuzi wa barabara mbalimbali nchini; ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria; upanuzi wa bandari za Dar Es Salaam, Mtwara na Tanga na kuboresha viwanja vya ndege mbalimbali nchini ikiwemo ujenzi wa Terminal 3 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Serikali pia imepiga hatua katika kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika sekta ya afya, elimu na maji. Kwa upande wa afya, bajeti ya sekta hiyo imeongezeka kutoka bilioni 31 hadi kufikia bilioni 270 ambapo ujenzi wa vituo vya afya 305 umekamilika na ujenzi wa hospitali 67 za Wilaya unaendelea, ukilenga kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kuhusu elimu, Serikali imeendelea na mpango wake wa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuongeza bajeti ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Aidha, Miundombinu ya maji imeimarishwa ambapo upatikanaji wa maji kwa maeneo ya mijini umefikia asilimia 80 na asilimia 65 kwa maneo ya vijijini.
Rais Magufuli alieleza kuwa mafanikio ambayo Serikali ya awamu ya tano inaendelea kuyapata yanatokana na Ushirikiano na mchango mkubwa kutoka kwa wanadiplomasia, na kuahidi kuwa Serikali yake itaendelea kudumisha Ushirikiano huo.

Alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa, watumishi wengi wa Serikali walishahamia Makao Makuu ya Serikali jijini Dodoma na kuelezea matumaini yake kuwa, baadhi ya Balozi zitakuwa zimeshaanza mchakato wa kuhamia Dodoma, ukizingatia kuwa Serikali imetoa viwanja bure kwa ofisi zote za balozi.  
  
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania

09 Machi 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini katika Sherehe za kufungua Mwaka 2019 (sherry party) zilizofanyika Ikulu, Dar Es Salaam jana. Sherehe hizo zimehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe na Wakuu wa Idara na Vitengo.
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiendelea kuzungumza wakati wa sherehe hizo.
Mabalozi wakimpongeza Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli 
Rais Magufuli akiendelea kuzungumza na wanadiplomasia

Kiongozi wa Mabalozi ambaye ni Balozi wa Comoro nchini, Mhe. Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed naye akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa.
Sehemu ya Mabalozi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (kulia)
Mshereheshaji kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Bertha Makilagi akisherehesha kwenye Shughuli hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na Balozi wa Namibia, Mhe.Theresa Samaria mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na Balozi wa Oman hapa nchini, Mhe. Ali A. Al Mahruqi mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Mhe. Sarah Cooke mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na Balozi wa India hapa nchini, Mhe. Sandeep Arya mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (kulia) akisalimiana na Balozi wa Ufaranza nchini, Mhe. Frederic Clavier mara baada ya kumalizika kwa sherehe za mwaka 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaoziwakilisha nchni zao hapa nchini, mara baada ya kumalizika kwa Sherehe za kufungua Mwaka 2019 (Diplomatic Sherry Party).




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.